Wakenya kufurahia jua kiasi mvua ikipungua kwa siku sita
MAENEO mengi ya nchi yatashuhudia kupungua kwa mvua kuanzia Jumanne, Aprili 29 hadi Jumamosi, Mei 3 2024, Idara ya Hali ya Hewa Kenya imetangaza.
Tangazo hilo lilitolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Hali ya Hewa, David Gikungu, kupitia taarifa Jumatatu, Aprili 28.
Wakazi wa kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka, na Nairobi wanatarajiwa kushuhudia anga yenye mawingu ambayo yatatoweka na kutoa nafasi kwa jua nyakati za asubuhi siku za Jumanne, Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi. Hata hivyo, kuna uwezekano wa mvua kunyesha Jumatano asubuhi katika maeneo machache.
Maeneo machache katika kaunti hizo pia yanatarajiwa kupokea mvua nyepesi kuanzia Jumanne hadi Jumamosi nyakati za alasiri na usiku, huku usiku wa Jumatano ukitarajiwa kuwa na mawingu kiasi.
Joto la juu zaidi katika maeneo haya linatarajiwa kuwa nyuzi joto 20 za Selsiasi, huku joto la chini zaidi likitarajiwa kuwa nyuzi joto 6.
Maeneo mengi ya kaunti za Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado, Taita Taveta, pamoja na sehemu za ndani za Kaunti ya Tana River, yanatarajiwa kuwa na vipindi vya jua asubuhi na alasiri.
Hata hivyo, maeneo haya huenda yakapokea mvua nyepesi Jumamosi alasiri na usiku wa Jumatano na Alhamisi.
Joto la juu zaidi katika maeneo haya litakuwa nyuzi joto 32, huku la chini zaidi likiwa nyuzi joto 13.
Wakazi wa kaunti za Mombasa, Kilifi, Lamu, na Kwale, pamoja na sehemu za pwani za Tana River, wanatarajiwa kupata vipindi vya jua asubuhi. Maeneo haya yanatarajiwa kupokea mvua nyepesi Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi nyakati za alasiri na usiku.
Kaunti za Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia, na West Pokot zitashuhudia vipindi vya jua asubuhi, huku mvua zinazofuatana na radi zikitarajiwa maeneo mengi siku nzima hadi usiku.
Wakazi wa kaunti za Turkana na Samburu watashuhudia vipindi vya jua mchana katika kipindi hiki. Joto la juu zaidi katika kaunti hizi linatarajiwa kuwa nyuzi joto 37, huku la chini likiwa nyuzi joto 8.