Habari

Kaa chonjo kwa Mvua, jua na manyunyu hapa na pale wiki nzima

Na BENSON MATHEKA November 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAKENYA wametakiwa kujiandaa kwani baadhi ya sehemu zitapokea mvua, jua na manyunyu wiki nzima.

Hii ni kulingana na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa.

Katika utabiri huo, miji na kaunti kama Nairobi, Kiambu, Kisumu, Nakuru, Machakos, Meru, na Kitui, miongoni mwa zingine, zinatarajiwa kupata mvua na manyunyu kuanzia Jumanne, Novemba 18 hadi Jumamosi, Novemba 22.

Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka na Nairobi zitakuwa na jua, isipokuwa Jumanne, Jumatano na Alhamisi mchana ambapo maeneo kadhaa yanaweza kupata manyunyu. Usiku, hali ya mawingu inatarajiwa kutawala.

Hata hivyo, manyunyu na mvua yanatarajiwa kwa siku nyingi za wiki katika kaunti za Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado na Taita Taveta, pamoja na maeneo ya ndani ya Kaunti ya Tana River, wakati wa mchana na usiku, isipokuwa Jumamosi asubuhi ambapo kutakuwa na jua.

Kwa mujibu wa utabiri huo, maeneo ya Mombasa, Kilifi, Lamu, Kwale na sehemu za Tana River yatapata manyunyu katika baadhi ya maeneo, hasa wakati wa mchana. Usiku  kutakuwa na na mawingu, isipokuwa Alhamisi usiku ambapo mvua inatarajiwa.

Wakazi wa Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia na West Pokot wanaweza kupata mvua na manyunyu mara kwa mara yakifuatana na radi, hasa wakati wa mchana.
Jumatano asubuhi na Jumamosi kutakuwa na jua. Usiku, mawingu yanatarajiwa isipokuwa Alhamisi na Ijumaa ambapo mvua inaweza kunyesha.

Kaunti za Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa na Isiolo zinatarajiwa kupata manyunyu ya mchana kutwa hadi Alhamisi, huku Ijumaa na Jumamosi kukiwa na jua. Usiku, mawingu yatakuwa mengi.
Turkana na Samburu zitakuwa na jua mchana kutwa wiki nzima, huku usiku kukitarajiwa hali ya mawingu.