Kaunti 20 hazikutumia hata shilingi moja kwa maendeleo, ripoti yafichua
KAUNTI 20 hazikutumia hata ndururu kwa miradi ya maendeleo katika robo ya kwanza ya mwaka wa kifedha wa sasa kati ya Julai na Septemba 2025.
Hii ni kulingana na ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti (CoB) imefichua.
Kaunti za Isiolo, Kirinyaga na Murang’a ndizo zilizoongoza kwa kutumia asilimia kubwa zaidi ya bajeti zao za maendeleo, huku jumla ya Sh3.69 bilioni pekee zikitumika kwa maendeleo.
Ripoti hiyo, inayochora taswira ya kusikitisha ya miradi iliyokwama katika kaunti, inaonyesha matumizi makubwa ya pesa katika shughuli za kawaida chini ya magavana, jambo linalozua maswali makubwa kuhusu vipaumbele vya ugatuzi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kaunti za Kericho, Tana River, Turkana, Bomet, Siaya, Trans Nzoia, Baringo, Kilifi, Kwale, Kajiado, Kisumu, Mombasa, Vihiga, Busia, Pokot Magharibi, Bungoma, Uasin Gishu, Wajir, Laikipia na Kisii ziliripoti matumizi ya sifuri kwa bajeti zao za maendeleo katika robo ya kwanza ya mwaka wa kifedha utakaoisha Juni 30, 2026.
Kaunti ya Wajir aidha haikutumia fedha zozote katika kipindi hicho au ilishindwa kuwasilisha ripoti yake kwa Mdhibiti wa Bajeti.
Haya yamo katika Ripoti ya Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali za Kaunti kwa robo ya kwanza ya mwaka wa kifedha hadi Juni 30, 2026, iliyozinduliwa Jumatatu na Mdhibiti wa Bajeti, Bi Margaret Nyakang’o.
Ripoti hiyo kali ilifichua kuwa kaunti 27 zilizosalia kwa pamoja zilitumia Sh3.69 bilioni pekee kwa maendeleo katika kipindi cha miezi mitatu, sawa na kiwango cha matumizi cha asilimia mbili ya bajeti ya maendeleo ya mwaka mzima ya Sh218.99 bilioni.
Cha kushangaza, kaunti zote 47 zilitumia zaidi ya Sh51 bilioni kwa matumizi ya kawaida, ikiwemo Sh43.7 bilioni kwa mishahara ya wafanyakazi na Sh7.76 bilioni kwa shughuli na ukarabati.
Hali ni mbaya zaidi ikizingatiwa kuwa Sh3.69 bilioni ni kiwango cha chini ikilinganishwa na Sh6.71 bilioni zilizotumiwa na kaunti katika kipindi kama hicho mwaka wa kifedha ulioisha Juni 30, 2025, ambapo jumla ya bajeti ya maendeleo ilikuwa Sh205.33 bilioni.
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa, serikali za kaunti zilitumia takriban mara 11 zaidi kwa mishahara ya wafanyakazi kuliko maendeleo katika robo hiyo, mwelekeo unaoendelea kudhoofisha utoaji wa huduma na imani ya umma kwa ugatuzi.
“Mdhibiti wa Bajeti anashauri serikali za kaunti kuongeza matumizi ya bajeti za maendeleo kwa kipindi kilichosalia cha mwaka wa kifedha wa 2025/26,” inasema ripoti hiyo.
“Hatua hii itasaidia kuboresha kiwango cha matumizi ya fedha za maendeleo na kukuza maendeleo ya jumla ya kaunti.”
Kifungu cha 107(2)(b) cha Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma ya 2012 kinazitaka serikali za kaunti kutenga angalau asilimia 30 ya bajeti zao kwa matumizi ya maendeleo kwa muda wa kati.
Kanuni ya 25(1)(g) ya Kanuni za Usimamizi wa Fedha za Umma (Serikali za Kaunti) za 2015 pia inahitaji matumizi halisi kuendana na kiwango hicho, kigezo ambacho kaunti nyingi bado hazijatimiza.
Kaunti za Murang’a (Sh181.7 milioni), Makueni (Sh179.4 milioni), Machakos (Sh252 milioni), Mandera (Sh269 milioni) na Kitui (Sh221 milioni) zilitumia takriban asilimia tano ya bajeti zao za maendeleo za mwaka mzima.
Kaunti ya Isiolo chini ya Gavana Abdi Guyo pia iliongoza kwa matumizi ya jumla ya bajeti kwa kutumia asilimia 21 ya bajeti yake ya mwaka katika kipindi hicho.
Ilifuatiwa na Kitui kwa asilimia 18, na Machakos, Nyeri na Uasin Gishu kila moja kwa asilimia 14.
Kwa upande mwingine, Turkana na Laikipia zilirekodi kiwango cha chini kabisa cha matumizi ya jumla cha asilimia tano kila moja, zikifuatwa na Tana River, Nyandarua na Kericho kwa asilimia nne kila moja.
Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata alieleza kuwa utawala wake umeelekeza rasilimali katika miradi ya kuboresha miji iwe ya kisasa , ikiwemo lami kwenye masoko, mipango ya kuwawezesha vijana, na ununuzi wa mbegu na mbolea zilizoidhinishwa kusaidia wakulima.
Kaunti zilizoripoti kutotumia chochote kwa maendeleo, zilionyesha matumizi makubwa ya shughuli za kawaida, huku idadi ya miradi iliyokwama ikiongezeka na kugharimu mabilioni ya shilingi.
Kaunti ya Bungoma chini ya Gavana Ken Lusaka iliongoza kwa kutumia Sh2 bilioni kwa mishahara ya wafanyakazi na Sh125.1 milioni kwa shughuli na ukarabati bila hata senti moja kuelekezwa kwa maendeleo.
Kaunti ya Kisumu chini ya Gavana Anyang’ Nyong’o ilitumia Sh1.25 bilioni kwa mishahara na Sh61.8 milioni kwa shughuli, huku Kilifi ikitumia Sh1.2 bilioni kwa wafanyakazi na Sh272.9 milioni kwa shughuli na ukarabati bila matumizi ya maendeleo.
Kaunti ya Mombasa chini ya Gavana Abdulswamad Nassir ilitumia Sh1.12 bilioni kwa mishahara na Sh62 milioni kwa shughuli, bila chochote kwa maendeleo.
Kaunti ya Uasin Gishu ilitumia Sh1.14 bilioni kwa mishahara, huku Kaunti ya Kwale chini ya Gavana Fatuma Achani ikitumia Sh962.2 milioni kwa mishahara na Sh89.6 milioni kwa shughuli, ilhali inakabiliwa na miradi ya maendeleo iliyokwama ya thamani ya Sh281 milioni, ambapo Sh116 milioni pekee zimelipwa.
Kaunti ya Siaya chini ya Gavana James Orengo ilitumia Sh712.4 milioni kwa mishahara ilhali ina miradi mitatu ya maendeleo iliyokwama ya thamani ya Sh46.8 milioni.
Katika kaunti ya Tana River, hii ni mara ya pili mfululizo kutotumia fedha zozote kwa maendeleo licha ya kutumia Sh404.8 milioni kwa mishahara katika kipindi hicho.
Kaunti ya Pokot Magharibi chini ya Gavana Simon Kachapin pia haikutumia chochote kwa maendeleo kwa mara ya pili mfululizo.
Kaunti ya Trans Nzoia chini ya Gavana George Natembeya haikutumia fedha zozote kwa maendeleo licha ya kuwa na miradi iliyokwama ya thamani ya takriban Sh80 milioni.
Kaunti ya Turkana haikutumia chochote kwa maendeleo, ikitumia Sh923.7 milioni kwa shughuli za kawaida licha ya kuwa na miradi 19 ya maendeleo iliyokwama ya thamani ya Sh162 milioni.
Kaunti ya Baringo ilitumia Sh649.9 milioni kwa mishahara huku ikikabiliwa na miradi 16 ya maendeleo iliyokwama ya thamani ya Sh217.44 milioni.
Kaunti ya Bomet pia ilitumia zaidi ya Sh630 milioni kwa shughuli za kawaida bila kuzingatia maendeleo.
Kaunti ya Busia chini ya Gavana Paul Otuoma ilitumia Sh1 bilioni kwa mishahara na Sh136.6 milioni kwa shughuli na ukarabati bila chochote kwa maendeleo.