Kimataifa

China nayo yajibu Rais Trump kwa kuongeza ushuru

Na REUTERS April 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

 CHINA Ijumaa ilimjibu Rais Donald Trump kwa kuongeza ushuru kwa bidhaa inazoagiza kutoka Amerika kwa asilimia 125, huku ubabe wa kibiashara kati ya nchi hizo ukiendelea kutikisa ulimwengu kibiashara.

Rais Trump alikuwa amepandisha ushuru kwa bidhaa ambazo Amerika inaagiza kutoka China hadi asilimia 145 wiki hii. China na Amerika zimekuwa na ubabe wa kibishara tangu Trump aingie mamlakani Januari, na kusababisha thamani za sarafu mbalimbali duniani kushuka.
“Hatua ya Amerika inakiuka kanuni za kibiashara ulimwenguni. Huu ni udikteta wa kibiashara,” ilisema Wizara ya Masuala ya Kigeni ya China.

Kiongozi huyo wa Amerika wiki hii aliweka ushuru kwa mataifa mbalimbali lakini baadaye akaghairi nia na kuzisitisha kwa muda wa siku 90. Hata hivyo, ushuru ambao uliwekewa bidhaa za China haukuondolewa.
“Hatua ya Amerika kuweka ushuru wa juu, inakiuka kanuni za kibiashara za ulimwenguni. Huu ni udikteta wa kibiashara,” ikasema wizara ya masuala ya kigeni ya China.
Rais Xi Jinping naye alisema kuwa hakuna mshindi katika vita vya kibiashara huku akipigia upato ushirikiano wa kibiashara kati ya taifa lake na Muungano wa Bara Ulaya (EU) ambao una mataifa 27 kama wanachama.