Uingereza pia yaamrisha raia wake waondoke Sudan Kusini.
NA MASHIRIKA
LONDON, UINGEREZA
UINGEREZA imewashauri raia wake wanaoishi Sudan Kusini wafanye hima na kuondoka nchini humo kufuatia taharuki ambayo inaendelea kushuhudiwa taifa hilo la Afrika Mashariki.
“Kama upo Sudan Kusini na unaona utovu wa usalama unaoendelea, unastahili kuondoka sasa hivi,” ikasema wizara ya masuala ya kigeni ya Uingereza.
Tayari Amerika, Uingereza na Ujerumani zimefunga ubalozi wao Sudan Kusini na pia kupunguza shughuli zao nchini humo. Sudan Kusini inashuhudia taharuki kutokana na uhasama wa kisiasa kati ya Rais Salva Kiir na Makamu wa Rais wa kwanza Riek Machar.
Mnamo Alhamisi, chama cha Machar kilisema kuwa kifungo cha nyumbani ambacho kiongozi huyo alikuwa amewekewa kunaonyesha kuporomoka kwa mkataba walioutia saini hapo awali.
Mkataba huo ndio ulizima vita vya kijamii ambavyo vilikuwa vimedumu kati ya 2013-2018 ambavyo vilisababisha mauaji ya mamia ya watu.
“Viongozi wa Sudan Kusini lazima waridhiane kupunguza taharuki,” akachapisha Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Uingereza David Lammy kwenye mtandao wake wa X.
Umoja wa mataifa (UN) na mataifa mengine ya Magharibi pia yametoa wito kwa Rais Kiir na Machar waridhiane ili kuzuia wafuasi wao kurejea vitani.
Tafsiri na Cecil Odongo