Kimataifa

Waasi wa M23 waingia katikati ya Goma raia wakitoroka

Na REUTERS January 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

GOMA, DRC

WAASI wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, Jumatatu  January 27,  waliingia hadi katikati mwa jiji kubwa la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, walioshuhudia walisema.

Hii ni ongezeko la hivi karibuni la miongo kadhaa ya vita katika eneo ambalo tayari linakabiliwa na moja ya mizozo mbaya zaidi duniani ya kibinadamu.

Muungano wa waasi, unaoongozwa na wanamgambo wa kabila la Watutsi wanaoongozwa na M23, ulisema umeteka mji mzima wa kando ya ziwa, lakini hilo halikuweza kuthibitishwa.

Milio ya risasi ilisikika karibu na uwanja wa ndege, katikati mwa jiji kwenye mpaka na Rwanda, huku wakaazi wawili wakiripoti mapigano yanayoendelea kati ya wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali na wapiganaji wa M23.

“Kuna mkanganyiko mjini. Hapa karibu na uwanja wa ndege, tunaona wanajeshi. Bado sijaona M23,” mkazi mmoja aliambia Reuters kwa simu, akiomba kutotajwa jina.

“Pia kuna baadhi ya matukio ya uporaji wa maduka.”

Waasi wa  M23, ambao ni  kundi la hivi punde zaidi katika msururu mrefu wa waasi wanaoongozwa na Watutsi wanaoungwa mkono na Rwanda, waliteka Goma mwaka 2012 lakini wakajiondoa siku chache baadaye baada ya makubaliano yaliyosimamiwa na mataifa jirani.

Congo ina zaidi ya makundi 100 yenye silaha, hasa mashariki mwa taifa hilo la Afrika ya kati lenye watu milioni 100 ambalo lina ukubwa wa takribani Ulaya Magharibi na lina utajiri wa madini.

Corneille Nangaa, kiongozi wa Congo River Alliance,  muungano wa waasi unaojumuisha M23, aliambia Reuters siku ya Jumatatu kwamba vikosi vyake vinadhibiti Goma na kwamba wanajeshi walikuwa wakiweka silaha chini.

“Wameanza kujisalimisha, lakini inachukua muda,” alisema. “Ni kawaida kwamba wao (wakazi) bado wanaona askari.”

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na familia zao walikuwa wakiondoka kuelekea Rwanda Jumatatu asubuhi, ambapo mabasi 10 yalikuwa yakisubiri kuwachukua.

Video ambazo hazijathibitishwa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha wakazi wa eneo hilo wakipora bidhaa   bohari la forodha nje ya uwanja wa ndege na watu wenye silaha nzito, wanaoaminika kuwa wapiganaji wa M23, wakipita katika vitongoji vya kaskazini mwa jiji.

Wanajeshi 26 wa Congo na afisa mmoja wa polisi walikuwa wamevuka mpaka na kujisalimisha, wanajeshi wa Rwanda waliambia Reuters.

Maelfu ya wakazi wa mji wa mpakani wa Rwanda wa Gisenyi walikimbia kuelekea mashariki, kuelekea mji mkuu Kigali, huku sauti za milipuko kutoka Goma zikiongezeka, ripota wa Reuters alisema.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA