Kimataifa

Wanafunzi 23 waliofumaniwa wakishiriki ngono wafukuzwa chuoni

April 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na DAILY MONITOR

CHUO Kikuu cha Kiislamu nchini Uganda kimefukuza kwa muda wanafunzi 23 kwa tuhuma za  kushiriki mahusiano ya kimapenzi kinyume na sheria za taasisi hiyo.

Uamuzi dhidi ya wanafunzi hao ulitangazwa na kamati ya nidhamu chuoni humo. Wanafunzi watuhumiwa wanasomea kozi mbalimbali katika bewa la Mbale.

Mshirikishi wa chuo hicho Dkt Sulait Kabali, ambaye pia ni katibu wa kamati hiyo ya nidhamu aliliambia gazeti la ” The Daily Monitor” Jumatatu kwamba wanafunzi hao walipatikana na hatia ya kukiuka sheria na kanuni za chuo.

“Wanafunzi hao walipatikana na hatia ya kushiriki ngono chuoni, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za taratibu za chuo,” Dkt Kabali akasema.

Aliongeza kuwa wanafunzi wengine walipatikana na hatia ya wizi wa mali, unywaji pombe na matumizi ya mihadarati, uja uzito na kushiriki fujo chuoni.

Kulingana na barua ya kuwafukuza wanafunzi hao iliyoandikwa Aprili 14, 2018, ambayo “The Daily Monitor” iliona, wanafunzi hao walipatikana wakiwa wamejificha sehemu mbalimbali chuoni wakila uroda.

“Kamati ya nidhamu iliwapata na hatia baada ya kuwahoji na kuchanganua utetezi wenu ambapo mliungama kuwa mlipatikana mkishiriki mapenzi. Vitendo kama hivyo vinakiuka sheria za chuo zilizotajwa hapo juu,”   ilisema barua iliyoandikiwa wanafunzi hao.

 

Nje mwaka mzima

Dkt Kabali alisema wanafunzi hao watakaa nyumbani kwa muda wa mwaka mmoja, akisema adhabu hiyo inafaa kuchukuliwa kama onyo kwa wanafunzi wengine wenye tabia kama hizo.

Alisema chuo hicho hakitasita kumfukuza mwanafunzi yeyote ambaye atadiriki kukiuka sheria na kanuni zake kuhusu maadili.

Wanafunzi waathiriwa, wanaojumuisha wanafunzi wa mwaka wa mwisho, walikuwa wakikaribia kufanya mitihani yao ya mwisho wa kozi, ambayo ilianza Jumatatu.

Hata hivyo, wanafunzi hao 23 walipewa muda wa wiki mmoja kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Afisa wa uhusiano mwema Bi Rehema Katono alisema kuwa baada ya wiki moja kamati ya nidhamu itafanya kikao kingine kuchunguza rufaa zozote ambazo zitakuwa zimwasilishwa.

 

Adhabu kali

Mwanafunzi mmoja aliyeathirika, na ambaye hakutaja jina lake litajwe kwa hofu ya kuathiri rufaa yake, alisema kamati hiyo ilitoa uamuzi mkali dhidi yao.

“Nashangaa kwamba kamati hiyo iliyotoa uamuzi wake kwa msingi wa kosa ambalo nilitenda miaka miwili iliyopita nilipojiunga na chuo hicho. Adhabu hiyo ni kali mnamo mno,” akasema.

Chuo hicho cha Kiislamu kina mabewa mengi na kinaongozwa chini ya sheria za kiisalamu, maarufu kama “sharia”.

Inafundisha kozi za astashahada (certificate), stashahada (diploma), shahada ya digrii ya kwanza, uzamili na uzamifu.

Kulingana na Bi Katono, mwanafunzi yeyote ambaye anataka kushiriki mahusiano ya kimapenzi anapaswa kutuma ombi kwa kamati ya Dawah, ambayo itampa ruhusa ya kuoa rasmi.

Lakini hata kama wachumba, wanafunzi hawaruhusiwi kupigana pambaja, kubusiana au kuketi wawili (wanafunzi wa jinsia tofauti) kwa zaidi ya dakika 10, bila kuwepo kwa mwenzao wa tatu.

Vile vile, hamna maingiliano kati ya wanafunzi wa kike na wa kiume madarasani au ndani ya chuo.