Habari

Machozi ya mamba wabunge wakikosoa SHA waliyounga mkono

Na JOSEPH OPENDA January 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LICHA ya kuonekana kushabikia Bima ya Afya ya Jamii (SHA) mbele ya Rais William Ruto, wabunge Alhamisi walichomoa meno ya kukemea mpango huo wakihisi kuwa hautafaa Wakenya na kuna mengi yanayostahili kufanyika kuimarisha ufaafu wake.

Katika kikao na Katibu wa Huduma za Kimatibabu Harry Kimtai na maafisa wa Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA), wabunge walitilia shaka kufaulu kwa mpango huo huku wakionekana kuegemea upande wa umma ambao umezua malalamishi kuhusu bima hiyo mpya.

Aidha, wabunge walimchemkia Mwenyekiti wa SHA Abdi Mohamed kwa kuwajibu kimadharau kuwa maelezo zaidi kuhusu bima hiyo yapo kwenye tovuti na mitandaoni.

Bw Abdi pamoja na Afisa Mkuu Mtendaji wa SHA Robert Ingasira walikuwa kwenye kikao hicho kilichofanyika Naivasha ambako wabunge wamekuwa na kongamano la kutathmini utendakazi wao wa katikati mwa muhula wao.

Wabunge walitaka majibu kuhusu utekelezaji usioridhisha wa mpango huo wa afya, magonjwa ambayo matibabu yake yanagharimiwa na SHA na kwa nini mtandao wa SHA umekuwa ukifeli mara kwa mara na kuwapa wagonjwa wakati mgumu kuhudumiwa.

Mbunge wa Nyeri Mjini Duncan Mathenge achemkia Katibu wa Wizara ya Afya Harry Kimtai akimtaka kufafanua kuhusu mfumo wa Afya ambao Wakenya wengi wanalalamikia ufaafu wake. Picha|Boniface Mwangi

Wabunge walimchemkia Bw Mohamed na wakataka wahutubiwe na katibu au afisa mkuu mtendaji ambao waliwaona kama wenye ujuzi kuhusu SHA kuliko mwenyekiti huyo.

“Mawasilisho na majibu ya Bw Mohamed yanaonyesha wale wanatekeleza SHA hawajui chochote au hawaielewi. Mwenyekiti hawezi kutuambia maelezo yapo kwenye tovuti. Mbona usizungumze vizuri na Wakenya?” akahoji Bw Ichung’wah.

Mbunge wa Ruaraka TJ Kajwang pia alikasirishwa na jibu la Bw Mohamed.

“Inaonekana katibu ana maelezo bora kuliko mwenyekiti kuhusu SHA. Nani atawaambia Wakenya ukweli kuhusu huduma na manufaa ya SHA?” akauliza Bw Kajwang’.

Taifa Leo ilibaini kuwa, maelezo duni yalitokana na tofauti kati ya wanaosimamia SHA ambao ni kati ya miradi mikuu ya utawala wa Rais Ruto.

“Kuna tofauti kati ya mwenyekiti na afisa mkuu mtendaji ndiyo maana kuna maelezo haba ambayo yaliwasilishwa kwenye kikao na wabunge,” duru kutoka Jumba la Afya likaeleza.

Licha ya kuonekana kushabikia SHA mbele ya Rais Ruto na kupitisha sheria ya kuondoa iliyokuwa Hazina ya Bima ya Taifa ya Afya (NHIF), wabunge wenyewe walionekana hawaielewi na wakatoa wito kufanywe uhamasisho kuhusu bima hiyo mpya huku wakijifanya kujali wananchi.

Kikao cha jana pia kiligubikwa na kuzomewa kwa Bw Kimtai wabunge wakitaka majibu kuhusu kunyakwa kwa Grace Njoki maarufu kama ‘Simba jike wa SHA.

Bi Njoki alikuwa kwenye kundi la wanawake waliofika Jumba la Afya kutaka majibu kuhusu mtandao wa SHA kufeli walipokuwa wakisubiri watibiwe katika Hospitali ya Kenyatta.

Ilibidi Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangúla kuingilia kati na kuwatuliza wabunge huku Bw Kimtai akiomba msamaha kuhusu kufeli kwa mtandao wa bima hiyo na akukubali kuondoa kesi dhidi ya Bi Njoki mahakamani.

“Naomba msamaha kuhusu mtandao wetu kuwa chini siku hiyo na hilo ndilo lilisababisha wanawake hao kuvamia jumba la Afya. Kwa sababu wizara ndiyo mlalamishi, tutaondoa kesi inayomkabili Bi Njoki kortini,” akasema.

Bi Njoki alikamatwa wiki jana na kufikishwa mahakamani kwa kuzua ghasia kwenye afisi ya serikali na akaachiliwa kwa dhamana ya Sh10,000 pesa taslimu.

Awali wabunge walimpa msomo Bw Kimtai kuhusu kisa hicho na badala yake wakawataka maafisa wa SHA wakamatwe kuhusu kufeli kwa mtandao bima hiyo.

“Mbona mgonjwa ambaye ana umri wa miaka 61 akamatwe akidai haki yake? badala yake wangewakamata maafisa wa SHA kuhusu kufeli kwao kuwajibika na kuhakikisha kuna mtandao imara,” akasema Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo.