Habari

Sasa maseneta 22 wamwandikia Lusaka kupinga kutimuliwa kwa Murkomen na Kihika

May 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MASENETA 22 wa Jubilee wamemwandikia barua Spika wa Seneti Kenneth Lusaka wakipinga mabadiliko yaliyotekelezwa kwa uongozi wa chama hicho.

Wakiongozwa na Kipchumba Murkomen, aliyepoteza wadhifa wake wa kiongozi wa wengi, viongozi hao pia wamepinga muungano mpya uliobuniwa kati ya chama hicho na Kanu wakisema sio halali kwa sababu haujaidhinishwa na Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la chama hicho inavyohitajika na Katiba yake.

Maseneta hao wamesema Jumatatu kuondolewa kwa Bw Murkomen na Bi Susan Kihika kutoka nyadhifa zao za Kiongozi wa Wengi na Kiranja wa Wengi, mtawalia, kulifanyika kinyume cha sheria za Seneti nambari 19.

Kulingana na sheria hiyo, mabadiliko kama hayo sharti yaungwe mkono na nusu ya maseneta wanaohudhuria kikao ambako mabadiliko hayo yalifanywa.

Hii ina maana kuwa masenata 18 kati ya maseneta 35 wanafaa kupiga kura ya kuunga mkono kuondolewa kwa wawili hao.

Kulingana na taarifa kutoka Ikulu, mkutano ulioitishwa na Rais Uhuru Kenyatta ulihudhuriwa na maseneta 20.

Lakini haijulikani kama wote waliunga mkono mabadiliko hayo au kuna wale waliopinga.

“Tunamweleza Rais kuwa hawezi kuongoza taifa hili kupitia ulaghai. Huwezi kughushi sahihi za wenzetu. Helikopta nne zimetumwa kuwasafirisha baadhi ya maseneta ambao sahihi zao ziliigizwa na kuingizwa kwa njia haramu,” Murkomen akaambia wanahabari baada ya kuvuliwa wadhifa wake.

Barua ambayo aliandikiwa Spika Lusaka imetiwa sahihi na; Bw Murkomen, Bi Kihika, Araon Cheruiyot (Kericho), Millicent Omanga (Seneta Maalum), Samson Cherargei (Nandi), Christopher Langat (Bomet), Michael Mbito (Trans Nzoia), Mahamud Mohamed (Mandera) , Juma Wario (Tana River), Mary Senata (Seneta Maalum), Phillip Mpaayei (Seneta Maalum), Alice Milgos, Victor Prengei (Seneta Maalum, Kithure Kindiki (Tharaka Nithi), Mithika Linturi (Meru), Stephen Lelegwe, Margaret Kamar (Uasin Gishu), Iman Falhada, Naomi Waqo (Seneta Maalum), Anwar Loitiptip (Lamu), John Kinyua (Laikipia) na Christine Wawudi (Seneta Maalum).

Maseneta hao sasa wanadai kuwa hawakupokea mwaliko rasmi kwa mkutano huo ambao ajenda yake kuu ilikuwa ni kuondolewa kwa Murkomen na Bi Kihika.

“Kama maseneta wa Jubilee, hatukupokea mwaliko kwa mkutano wowote wenye ajenda ya kujadili kuondolewa kwa Kiongozi wa Wengi katika Seneti na Kiranja wa Wengi katika Seneti,” barua hiyo inasema.

Wamesuta sehemu fulani ya uongozi wa Jubilee kwa kujaribu kubuni mirengo ndani ya chama hicho kupitia mabadiliko haramu.