Watu 25 walikufa barabarani, madereva 42 wakinyakwa Jumanne
HUKU pilkapila za Krismasi zikiendelea leo, Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) imesema madereva 42 wasiokuwa na leseni wamekamatwa na magari 418 yasiyokuwa kwenye hali nzuri yametwaliwa kipindi hiki cha sherehe.
Kupitia taarifa iliyotolewa jana, NTSA ilisikitikia idadi nyingi ya ajali katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha mauti ya raia.
Ilizitaja kaunti za Kakamega, Bungoma, Nakuru, Nyeri, Siaya, Kiambu, Nairobi, Machakos, Narok, Kisii, Turkana na Uasin Gishu kama ambazo zimeshuhudia ajali nyingi msimu huu.
“Mnamo Desemba 23 pekee kulikuwa na ajali 16 ambapo watu 25 walipoteza maisha yao. Wanane walikuwa wanaotembea kwa miguu, wanane wengine abiria, watano wakiwa wahudumu wa bodaboda, dereva mmoja na watatu wakisafiri nyuma ya bodaboda,” ikasema.
“Tunatuma rambirambi kwa familia zilizoumia na kuwatakia walioumia kila la kheri. Taifa linapoendelea kushuhudia msimu wa sherehe, NTSA itaendelea kuhakikisha kuna usalama barabarani,” ikaongeza.
Mamlaka hiyo ilisema ajali nyingi zimetokea kwa sababu madereva wanayaendesha magari wakiwa walevi, magari kukosa vidhibiti mwendo, magari mabovu kuendeshwa barabarani, magari kuwabeba abiria kupita kiasi na baadhi ya magari pia hata hayana bima.
“Tunatumia kila rasilimali kuhakikisha kwamba tunalinda maisha ya wanaotumia barabara zetu. Tunawaomba madereva, abiria, waendeshaji pikipiki na wanaotembea kwa miguu watumie barabara vizuri na kuzingatia sheria za trafiki,” ikasema taarifa ya NTSA.