Habari za Kitaifa

Kalonzo aamuru wabunge wake kuangusha mawaziri wateule wa ODM wakiletwa kuidhinishwa

Na KITAVI MUTUA July 30th, 2024 2 min read

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amewaamrisha wabunge wa chama chake wakatae mawaziri wateule wa ODM ambao walitangazwa na Rais William Ruto wiki jana.

Bw Musyoka amesema kuwa chama chake kinapinga jinsi ambavyo viongozi wanne wa ODM walivyotunukiwa uwaziri hasa Kiongozi wa Wachache kwenye Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi.

Makamu huyo wa rais wa zamani alisema Muungano wa Azimio la Umoja ulimpa Bw Wandayi wadhifa wa kuuongoza na kutoa mwelekeo kwa vyama tanzu na si jambo jema kwa mbunge huyo wa Ugunja kutaliki kazi hiyo kisha kujiunga na serikali.

“Nimetoa mwelekeo unaoeleweka kuwa majina manne ya viongozi wa ODM yakifikishwa bungeni ili yaidhinishwe, wabunge wa Wiper wapige kura ya LA dhidi yao,” akasema Bw Musyoka akiwa eneo la Kyuso, Mwingi Kaskazini mnamo Jumapili.

Aliwaamrisha wabunge wa Wiper wayapinge mawaziri hao wateule wanne kutoka ODM wakati wa kuhojiwa kwao na kamati husika na pia wabunge wakipiga kura ya kuidhinisha au kupinga uteuzi wao.

Aidha Bw Musyoka alishutumu ODM kwa kuwasaliti Wakenya akimrejelea kiongozi wa upinzani Raila Odinga kama mwanasiasa ndumakuwili. Alisema kuwa miaka ya nyuma Raila amekuwa akipinga wanasiasa wa upinzani kuchukuliwa na utawala uliopo kwa kuwa hatua hiyo inaua demokrasia, ilhali mwenyewe sasa amewaruhusu wabunge wake waungane na serikali.

“Kama chama ambacho kina hadhi ndani ya Azimio, Wiper inastahili kuarifiwa na ODM kabla ya uamuzi wa kumteua kinara wa wachache bungeni kama waziri,” akasema Bw Musyoka.

Kando na Bw Wandayi ambaye ni waziri mteule wa kawi, viongozi wengine wa ODM ambao walitunukiwa vyeo ni Hassan Joho (wizara ya Madini), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika na Biashara ndogo ndogo) na mbunge maalum John Mbadi (wizara ya Fedha).

Bw Odinga japo alisema ODM haijaingia mkataba na Kenya Kwanza, aliwaidhinisha wanne hao wahudumu kwenye utawala wa Kenya Kwanza.

Kuendeleza upinzani wake dhidi ya ODM, Bw Musyoka alisema atafuatilia kuona jinsi wabunge wa ODM watapigia kura kwa mawaziri hao wateule. Katika Bunge la Kitaifa, Wiper ina wabunge 25.

“Kama watapiga kura ya kuwaunga wanne hao basi Wakenya watajua ODM ilikuwa ikiwahadaa,” akaongeza Bw Musyoka.

Alishanga ni vipi ODM sasa imekumbatia manifesto ya Kenya Kwanza ambayo walipinga mno wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Kando na Wiper, Narc Kenya na PNU pia zimetishia kujiondoa Azimio baada ya wabunge wa ODM kuteuliwa kama mawaziri serikalini.