Unyunyiziaji maji mashambani waleta matumaini tele eneo kame Bomet
MABADILIKO ya hali ya hewa ni miongoni mwa changamoto kuu zinazokumba wakulima kote nchini.
Katika maeneo kama Chepalungu, Kaunti ya Bomet, wakulima wamekuwa wakikabiliana na athari za ukame, ambazo zimeharibu mazao na kupunguza uzalishaji kwa miongo mingi.
Nehemiah Langat, mkulima na mtaalamu wa kilimo ambaye ni mkufunzi wa wakulima zaidi ya 500 katika eneo hili, anasisitiza kuwa changamoto hizi zimeathiri mazao ya kawaida kama vile mahindi na mboga.
“Ukame umeangamiza mimea yetu kwa kipindi kirefu, na kufanya maisha ya wakulima kuwa magumu. Hali hii ililazimu baadhi yetu kutafuta mbinu mbadala ili kuweza kuendelea na kilimo na kujikimu kimaisha,” akasema Langat.
Kama njia ya kutafutia suluhu masaibu haya, mradi wa unyunyiziaji maji mashambani, maarufu kama Nogirwet Irrigation Scheme, ulianzishwa kwa ushirikiano wa kaunti ya Bomet pamoja na Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross).
Mradi huu hutumia maji kutoka mto Nogirwet ili kuendeleza kilimo cha migomba na mazao mengine ya biashara, hasa katika kipindi cha kiangazi.
Mradi huu, ulioanzishwa mwaka 2017, umeleta mabadiliko makubwa kwa wakulima wa eneo hili.
Langat, ambaye pia ni mmoja wa wakulima, anasema kuwa mradi huu umesaidia kuleta suluhu kwa ukame.
“Kwa mfano, mimi mwenyewe ninalima ekari tatu za ndizi, na mradi huu unaniwezesha kuendeleza uzalishaji wangu licha ya ukame,” anaongeza Langat.
Katika mradi huu, wakulima walisaidiwa kwa kupata miche ya mboga na ndizi, ikiwa ni pamoja na kabeji, sukuma wiki, pilipili hoho, butternuts, vitunguu, tikitimaji, na maharagwe.
Kuasisiwa kwa kilimo cha migomba kulilenga kuongeza faida miongoni mwa wakulima.
“Kilimo hiki kimekuwa na manufaa makubwa, ambapo soko kuu la mazao ya ndizi liko katika miji ya Kericho, Nairobi, na katika kaunti nyingine za karibu.” anakiri Langat
“Ndizi huchukua kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja kukomaa, kutegemea aina ya ndizi inayolimwa. Mafunzo ya kitaalamu yanayotolewa na maafisa wa kaunti yamekuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa ndizi, kwani wanapata ujuzi wa kisasa wa kilimo cha migomba.”
Licha ya mafanikio ya mradi wa Nogirwet, bado kuna changamoto kubwa zinazokumba wakulima, hasa linapokuja suala la kukubali mbinu mpya za kilimo.
Langat anafichua, “Wakulima wengi bado hawajakubali kikamilifu mbinu hizi, kutokana na mila na utamaduni wao. Wengi bado wanajikita katika ufugaji wa ng’ombe kuliko kilimo cha mazao.”
Mtaalamu huyu anasema kuwa hii ni changamoto kubwa akieleza ufugaji wa ng’ombe pekee hauwezi kuwa na faida kubwa katika mazingira ya ukame.
Mradi wa Nogirwet umefaidi zaidi ya familia 500 katika eneo hili, na umejumuisha jumla ya hekta 380 chini ya mradi wa unyunyiziaji.
Hata hivyo, juhudi za kuwahamasisha wakulima kubadili mtindo wao wa maisha zinakumbana na vizuizi hasa katika jamii za mashambani ambapo imani za jadi zimekita mizizi.
Mto Nogirwet ni wa kudumu na kwa hivyo umeleta matumaini kwa wakulima wa Chepalungu na maeneo jirani.
Umewapa fursa ya kustawisha kilimo mwaka mzima mfululizo licha ya changamoto za ukame na mabadiliko ya hali ya hewa.
“Sisi kama wakulima, tuna uwezo wa kufaidi na kujikimu, lakini tunahitaji msaada wa kitaalamu na rasilimali ili kufanikisha malengo yetu,” anasema Langat.