Funzo alilopata Raila baada ya kushindwa uchaguzi wa AUC
MIGAWANYIKO baina ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhusiana na vita vinavyoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ni miongoni mwa sababu zilizochangia Kenya kushindwa katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Aidha, umoja wa mataifa yanayozungumza Kifaransa katika kuunga mkono Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti ulizima kabisa ndoto ya Raila Odinga kutwaa wadhifa huo.
Isitoshe, uamuzi wa dakika za mwisho wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) kumuunga mkono Youssouf, ilimhakikishia Waziri huyo wa Mashauri ya Kigeni wa Djibouti ushindi.
Bw Odinga alianza uchaguzi huo vizuri kwa kuishinda katika awamu ya kwanza na ya pili, kabla ya Youssouf kuanza kuongoza katika awamu ya tatu.
Awamu ya kwanza
Bw Odinga alipata kura 20, Bw Youssouf akapata kura 18 huku aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Madagascar Richard Randriamndrato akipata kura 10 katika awamu ya kwanza.
Katika awamu ya pili, Bw Odinga alipata kura 22, Bw Youssouf akapata kura 19 huku Randriamndrato akashuka kwa kupata kura saba.
Bw Youssouf alianza kuongoza katika awamu ya tatu alipopata kura 23, Odinga akipata kura 20 huku Randriamndrato akipata kura tano pekee.
Katika awamu ya nne, Youssouf aliendelea kuwa juu baada ya kura zake kuongezeka hadi 25 huku Odinga akiongeza kura moja zaidi akipata kuta 21. Bw Randriamndrato hakushiriki katika awamu hii baada ya kuondolewa baada ya awamu ya tatu.
Katika awamu ya tano, Youssouf alipata kura 26, Bw Odinga akisalia na kura zake 21, huku nchi mbili zikisusia upigaji kura.
Idadi ya kura za Youssouf ilisalia 26 katika awamu ya sita ya uchaguzi huo huku akiongeza kura moja zaidi hadi 22.
Baadaye Bw Odinga alijiondoa na Bw Youssouf alishiriki awamu ya saba pekee yake ambapo alipata kura 33 na kutangazwa rasmi kuwa mshindi.
Ukumbi wa Nelson Mandela
Kura ilipokuwa ikipigwa katika Ukumbi wa Nelson Mandela jijini Addis Ababa, Ethiopia, Februari 15, 2025, ilikuwa ni wazi kwamba hatua ya mataifa wanachama wa jumuiya mbalimbali kubadili misimamo ilimwathiri Bw Odinga.
Awali, kulikuwa na dalili kwamba Rais William Ruto kama mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) alikuwa akikabiliwa na wakati mgumu kuongoza mchakato wa kusitisha vita DRC.
Wataalamu walionya kuwa dhana kwamba anaunga mkono Rwanda inayoshutumiwa kufadhili waasi wa M23 huenda ilimnyima Odinga kura ya DRC.
“Hii ndiyo maana kuna uwezekano mkubwa kwamba DRC haikuunga mkono katika uchaguzi wa uenyekiti wa AUC. Aidha, Kenya imefeli kumaliza mzozo wa DRC kupinga mazungumzo yaliyokuwa yakiendeshwa jijini Nairobi chini ya usimamizi wa rais mstaafu Uhuru Kenya,” anasema Profesa Macharia Munene.
Rais Ruto alipoitisha mkutano wa kwanza wa marais wa mataifa wanachama wa EAC Jumatano Januari 29, 2025 kujadili njia ya kukomesha vita nchini DRC, Rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi aliususia.
Badala yake alihudhuria mkutano wa SADC wa kujadili suala hilo hilo, uliofanyika jijini Harare, Zimbabwe siku moja baadaye, Januari 30.
Aidha, kumekuwa na uhasama kati ya Afrika Kusini na Rwanda kuhusu mzozo nchini DRC.
Wanajeshi 14 wa Afrika Kusini
Baada ya wanajeshi 14 wa Afrika Kusini kuuawa katika Mkoa wa Kivu Kaskazini, baada ya wapiganaji wa M23 kuteka mji mkuu Goma, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alitoa taarifa kali akirejelea wanajeshi wa Rwanda kama “kundi la wapiganaji.”
Taarifa hiyo ilimkera Rais wa Rwanda Paul Kagame, aliyemrushia Ramaphosa maneno makali akiapa kuanzisha vita na Afrika Kusini.
Kulingana na Profesa Munene ni hali kama hii ambayo huenda ilichangia Bw Odinga kukosa uungwaji mkono kutoka baadhi ya mataifa wanachama wa SADC.
“Ilibainika kuwa hata baada ya mgombeaji kutoka Madagascar, taifa mwanachama wa SADC, kujiondoa, baadhi ya nchi hizo ziliamua kumuunga mkono Youssouf. Hatua hiyo, iliyochangiwa na uhasama kati ya Ramaphosa na Kagame, ilimwathiri pakubwa Odinga,” anaeleza.
Hatua ya Rais Ruto kuunga mkono Israel katika vita kati yake na kundi la Kipalestina Hamas, mnamo 2024 pia ilichangia mataifa ya Kiislamu kumkataa Bw Odinga.
Isitoshe, duru zinasema kuwa uwezo mkubwa wa Kenya na hadhi ya Bw Odinga katika rubaa za kimataifa huenda iliogofya baadhi ya viongozi wa mataifa wanachama wa AU na wasita kumpigia kura kiongozi huyo.