Lugha, Fasihi na Elimu

Mabadiliko ya kitenzi ‘-w-‘ katika semi (Sehemu 1)

Na ENOCK NYARIKI January 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TAARIFA kuhusu Wakenya waliotapeliwa mamilioni ya pesa na kampuni fulani kwa kuahidiwa kazi ughaibuni ilimshangaza hata mtangazaji wayo ambaye alitahadharisha; *“Wakenya lazima tukuwe macho!”

Kinyota katika kauli hiyo kinaonesha kosa la sarufi.

Kabla ya kubainisha kosa hilo, ni muhimu kutaja kuwa vitenzi vya silabi moja aghalabu hukosewa katika sentensi yamkini kwa kutomakinikiwa kwa masuala kadhaa:

Kwanza, kutofahamu wakati wa kujumuishwa au kudondoshwa kwa kiambishi {ku} ambacho hutekeleza dhima ya kijalizo katika vitenzi hivyo. Kimsingi, kiambishi hicho si sehemu ya mizizi ya vitenzi vya silabi moja ila hupachikwa ili kuvipa maumbo yatakayorahisisha matamshi.

Pili, kutofahamu mabadiliko yanayovikumba vitenzi hivyo vinapokanushwa katika nyakati mbalimbali.

Suala la tatu na linalokaribiana na la pili linatokana na kutotofautishwa kwa dhima za kiambishi {ku} cha ukanushaji wa wakati uliopita na kile ambacho kinatumiwa kama kijalizo.

Ili kuipambanua hoja ya pili na tatu, nitanukuu kauli ya mwandishi wa safu fulani katika gazeti la Taifa Leo. Hivi ndivyo alivyosema: ‘…hajakuwa akikubaliana kimahubiri na maombi ya EACC…’.

Kimsingi, uyakinishaji wa neno la kwanza – waama linapaswa kuwa la pili kwa kuwa mdokezo unaonesha kuepukwa kimakusudi kwa neno la kwanza – ulipaswa kuwa ‘amekuwa’.

Neno ‘amekuwa’ limeundwa kwa viambishi vinavyotekeleza dhima mbalimbali kisarufi. Kiambishi {a} kinawakilisha nafsi ya tatu umoja ilhali {me} ni cha hali timilifu. Kiambishi {ku} tulivyotaja hapo juu ni kijalizo ambacho dhima yake kuu ni kurahisisha matamshi kwa kuwa isingeyumkinika kusema ‘amewa’.

…YATAENDELEA
[email protected]