Makala

Mwimbaji wa benga asimulia jinsi mumewe alimtema, akaoa bintiye kisha tena akapita na mjukuu

Na MARY WANGARI November 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MWANAMUZIKI tajika wa nyimbo za benga kwa lugha ya Agikuyu amewastaajabisha wafuasi wake na watumiaji mitandao ya kijamii kwa jumla kwa kufichua jinsi aliyekuwa mumewe alivyomvizia bintiye na mjukuu wake.

Bi Florence Wangari almaarufu kama Wangari wa Kabera kwa lakabu yake ya kisanii, alisimulia jinsi mumewe waliyetengana, alivyomtema na kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na bintiye.

Katika mahojiano yaliyosambazwa mno kwenye mitandao ya kijamii na yaliyofikia Taifa Leo Dijitali, msanii huyo alisema aligundua kisadfa kuhusu uhusiano huo wa kimapenzi kati ya mumewe, aliyemtambulisha kama Chege wa Amerika na bintiye.

“Huwa siaibiki nikisema. Chege wa Amerika alinifanyia maajabu. Nilihisi kama moyo wangu au ini lingeanguka tumboni,” alisimulia Bi Kabera.

Kulingana na mwimbaji huyo, yote yalianza alipopokea picha ya aliyekuwa mumewe akiwa uchi wa mnyama, akishiriki mazungumzo ya kimapenzi na binti yake.

Alirekodi video

“Alikuwa ameweka simu yangu kwa namna kwamba, tukipiga simu, au kujipiga picha, inatangulia kufika kwake kwanza, na yeye pia akipiga, inatumwa kwangu kwanza,” alisema.

“Alirekodi video kwa kutumia mtandao uliokuwa ukiitwa Imo, wakizungumza na binti yangu akiwa uchi kabisa, ikatangulia kufika kwangu. Nilishtuka kuona huyu ni binti yangu na huyu ni Chege. Niliihamisha upesi ili akiifuta isalie kwenye simu yangu.”

Bi Kabera alisema tukio hilo lilimtikisa mno kiasi kwamba alilazimika kumfahamisha mama yake mzazi na tangu hapo akaanza kudhoofika kiafya.

“Nilipigwa na butwaa. Hiyo picha ilikuwa mbaya sana kwa sababu nilianguka na hata nikamwonyesha mama yangu.

“Kumbe nilipokonywa mtu kitambo na binti yangu! Nilianza kuzorota kiafya kuanzia hapo.”

Anasema alipomkabili bintiye kuhusu tukio hilo, alimjibu kwa cheche za matusi zilizosambaratisha uhusiano kati yao.

Hata hivyo, anasema bintiye alilazimika kumwomba radhi majuzi baada ya mwanamme huyo anayeishi Amerika, kumtendea vivyo hivyo alivyomfanyia, kwa kumwoa mjukuu wake.

‘Alinitusi vibaya’

“Nilipomuuliza binti yangu alinitusi vibaya sana isipokuwa majuzi alikuja kuniomba msamaha. Lakini alikuja kuomba radhi kwa sababu ya aliyotendewa na Chege yuyo huyo. Alimpokonya bintiye. Saa hii tunapozungumza nawe yuko (Chege) pamoja na mtoto wa binti yangu.”

Bi Kabera alielezea machungu aliyonayo kwa aliyekuwa mumewe akisema amemwachia Mola.

“Nasikia sasa amemkodishia nyumba Ruiru. Huyo mtu huwa nahisi nipange auliwe lakini naona nitapata adhabu ya Maulana huwa ninaomba maombi mabaya sana. Nina uchungu sana kwanza nikikumbuka mjukuu wangu ameitwa jina langu. Kule aliko ulaya Maulana amtazame.”

Hata hivyo, Bi Kabera aliyefichua katika mahojiano ya awali kuwa amefunga ndoa mara 15, alisema baada ya masaibu yote aliyopitia, Mola alimjaalia barafu ya moyo wake aliyemwoa.