Makala

RIPOTI MAALUM: Trump anavyoendelea kuzua taharuki Amerika

Na DOUGLAS MUTUA January 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

UTAWALA mpya wa Rais Donald Trump unazidi kuwatia hofu wahamiaji ambao hawana vibali vya kuishi nchini Amerika kutokana na msako mkali wa kuwakamata na kuwarejesha makwao unaoendelea wakati huu.

Hata hivyo, Waamerika wazaliwa pia wameanza kuhisi joto kali la Trump; amewapa wafanyikazi wote wa serikali, ambao ni jumla ya watu milioni mbili, fursa ya kujiuzulu na akaahidi kuwalipa mishahara ya miezi minane ijayo.

Ingawa hiyo si amri ya kuwalazimisha kujiuzulu, hivyo ndivyo mambo yanavyofanyika siku hizi. Unapewa fursa ya kujiuzulu, lau sivyo ufutwe bila malimbikizi ya manufaa ya miaka ambayo umefanya kazi.

Trump amewashtua zaidi wafanyikazi kwa kuwa tayari ameandika mfano wa barua ya kujiuzulu ambayo itatumiwa wafanyakazi wote wa serikali ikiwaeleza kwamba hawahitaji kufanya chochote ila kujibu kwa neno moja tu, ‘kujiuzulu’, ikiwa wanakubali kuondoka mapema.

Vinginevyo, barua hiyo inasema, wasiotaka kujiuzulu wanaingia mkataba wa kuitumikia serikali ya Trump kwa uaminifu katika mtindo mpya wa utendakazi.

Kuhusu uhamiaji, Trump hafanyi utani. Anawakamata na kuwarejesha watu makwao kikweli. Kote nchini Amerika, jumla ya watu 1,200 walikamatwa mnamo Jumapili pekee.

Imedaiwa kwamba baadhi ya Wakenya wameathirika, lakini hakuna ithibati wala takwimu za hakika kuthibitisha madai hayo.

Shirika la kuwakamata na kuwafukuza wahamiaji (ICE) limesema linawalenga Wakenya 1,282 walio na matatizo ya uhamiaji na makosa mengine yanayosababisha wafukuzwe, lakini halijasema iwapo limemnasa yeyote.

Limetangaza kuwa linanuia kuwakamata na kuwarejesha makwao raia wa mataifa kadha ya eneo la Afrika Mashariki kama vile Tanzania (301), Uganda (393), Somalia (4,090), Sudan Kusini (136), Ethiopia (1,713) and Rwanda (338).

Hii ina maana kwamba shirika hilo lina anwani za wanakoishi watu hao, hivyo litawafuata huko, na bila shaka nao hawatasubiri kunaswa tu, kwa hivyo huenda tayari wamehofu na kwenda mafichoni.

Pia, vimeripotiwa visa kadha vya wahamiaji, hata Wakenya, kuwasaliti wenzao wasio na vibali kwa kuwaitia polisi ili wakamatwe na kutimuliwa kutoka Amerika.

Wakenya wana uwezo wa kufanya jambo kama hilo, lakini ukweli ni kwamba hakuna ushahidi wamelifanya, kwa hivyo inaaminika wanaochapisha habari hizo kwenye mitandao ya kijamii wanatafuta kiki tu ili akaunti zao ziwavutie wasomaji wengi.

Msako wa wahamiaji wasio na vibali ulianzishwa siku ya pili baada ya Trump kuapishwa na unaendeshwa kwa fujo katika miji mikubwa iliyo ndani ya majimbo ambayo kwa muda mrefu yametumika kama hifadhi salama za wahamiaji hao.

Mathalan, mambo yanachemka na wahamiaji wameingia baridi kwenye jiji la Washington, D.C. na majimbo ya California, Colorado, Connecticut, Illinois, Massachusetts, New Jersey, New York, North Dakota, Oregon, Rhode Island, Utah, Vermont na Washington.

Kulikochacha zaidi ni miji mikubwa kama vile Chicago (Illinois), Seattle (Washington), Atlanta (Georgia) na jimbo zima la New York, lakini pia msako huo unafanyika kwa viwango vya chini kwingineko kusikoishi wahamiaji wengi.

Kwa mfano, katika Kaunti ya Fairfax, jimbo la Virginia linalopakana na jiji la Washington, D.C, kumeripotiwa visa vya polisi kuwagongea watu milango kwa fujo mno alfajiri kuu wakitafuta wahamiaji wasio na vibali.

Polisi maalum wa shirika la ICE walikwenda eneo hilo kuwatafuta wahamiaji fulani wa asili ya kusini mwa Amerika, ila wakakosea anwani na kumbishia Mwamerika wa kizungu aliyewashutumu kwa kuwa wakali mno.

“Niliamshwa na kelele kuu, ambazo naweza kusema ni za kichokozi, kutokana na jinsi walivyogonga mlango wangu. Niliwaambia wajitambulishe, wakasema wao ni polisi. Niliwauliza iwapo walikuwa na kibali cha mahakama, wakaniambia ndio, kisha nikafungua mlango nikitarajia kuwaona maofisa wa Kaunti ya Fairfax, ila nikakuta watu tofauti.”

Mtu huyo ambaye, japo alionekana kwenye video, hakutaka jina lake lijulikane ili polisi hao wasilipize kisasi, alisema alipowaeleza kuudhika kwake na tabia yao, maofisa hao walimtishia kwa kumuuliza: “Unataka kutiwa ndani?”

Alisema aliamua kufungua mlango pale alipowauliza maofisa hao walikuwa wakimtafuta nani, wakataja jina la Kihispania la mtu asiyemjua, ila hata baada ya kumkosa waliyekuwa wakimtafuta bado walimtishia.

Ingawa Trump anawaogopesha watu wengi, anakabiliwa na changamoto kadha ndani na nje ya Amerika katika juhudi zake za kuwafukuza wahamiaji asiowataka na pia za kuiunda upya serikali nzima.

Kando na kesi nyingi ambazo zimewasilishwa mahakamani kupinga amri kadha dhalimu alizotoa baada ya kuapishwa – miongoni mwazo inayosema mtoto anayezaliwa Amerika na wazazi wasio na vibali hatapata uraia mara moja kama ilivyo kawaida – anapingwa kimataifa.

Mataifa ya kusini mwa Amerika, Mexico na Colombia, hivi majuzi yalizinyima ndege nne za kijeshi za Amerika uhuru wa kutua kwenye nyanja zao kwani zilikuwa zimewabeba wahamiaji waliofukuzwa Amerika, hali mataifa hayo hayakuwa na mkataba wowote na Amerika.

Hata hivyo, marais Claudia Sheinbaum (Mexico) na Gustavo Petro (Colombia) baadaye walinywea na kughairi nia baada ya Trump kutishia kuongeza kodi za bidhaa za mataifa hayo zinazouzwa Amerika kwa asilimia 25, hatua ambayo ingezua matatizo ya kiuchumi.

Rais Claudia amekiri kuwa tayari Trump amefanikiwa kuwapeleka Mexico wahamiaji karibu 5,000, baadhi yao raia wa mataifa mengine, akabaki na kibarua cha kuwasadikisha raia wake kwamba Trump hatumii Mexico kama sehemu ya kuwabwaga raia wa kigeni.

Inaonekana vitisho vya Trump vinaendelea kumzalia matunda. Kwa mfano, alipokuwa akifanya kampeni mwaka jana, alisema iwapo angechaguliwa, angebadili jina la ‘Guba la Mexico’ kuwa ‘Guba la Amerika’.

Tayari kampuni ya Google, ambayo hubadili ramani ya dunia kuendana na mabadiliko ibuka, inaita eneo hilo ‘Guba la Amerika’.

Kenya – na mataifa mengine ya Afrika kwa jumla – inatarajiwa kuathiriwa vibaya na uamuzi wa Trump kusimamisha baadhi ya misaada ya kifedha inayofadhili miradi mbalimbali nje ya Amerika.

Hii ina maana kwamba wafanyakazi wa mashirika yanayotegemea misaada hiyo ama watafutwa kazi au walazimishwe kwenda likizo ndefu bila malipo kutokana na ukosefu wa fedha.

– Douglas Mutua anaishi jimbo la Virginia, Amerika