Sababu za Wakenya kumuomba Uhuru msamaha
KUONEKANA hadharani baada ya miezi kadhaa kwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta siku mbili kabla ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa Oktoba 26, kulisisimua Wakenya wakaibua kumbukumbu huku wakijuta kwa kupuuza ushauri aliowapatia kabla ya kuondoka mamlakani.
Bw Kenyatta amekuwa kimya tangu Julai alipotoa taarifa kuhimiza utulivu nchini kufuatia maandamano dhidi ya serikali na tangu wakati huo hakuwa ameonekana hadharani hadi Alhamisi ofisi yake ilipochapisha picha akihudhuria hafla ya Mungano wa Afrika jijini Abidjan, Cote Devoire.
Kutojitokeza kwake hadharani wakati wa matukio makubwa ya kisiasa hasa kuondolewa mamlakani kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kulikuwa kumezuka uvumi wa kila aina kuhusu hali yake ya afya.
Picha zake zilizoonyesha akiwasili katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Félix Houphouët-Boigny Abidjan ziliwasisimua Wakenya waliofurahia kumuona akionekana kuwa mwenye afya na kumuomba msamaha kwa kuwa walipuuza ushauri wake.
Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022, ambao uliashiria kuondoka kwake mamlakani baada ya kuhudumu kwa mihula miwili, Bw Kenyatta alimuunga kiongozi wa ODM Raila Odinga aliyegombea urais kwa tiketi ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya dhidi ya Rais William Ruto aliyekuwa naibu rais wakati huo.
Hata hivyo, Wakenya, hasa wakazi wa ngome ya Bw Kenyatta ya Mlima Kenya, walikataa kumuunga Bw Odinga na kumpigia kura kwa wingi Bw Ruto na mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua wakisema sera zake zilikuwa bora kuliko za mgombea urais wa Azimio.
Walidai kuwa Bw Kenyatta alitaka kuendelea kutawala kupitia Bw Odinga waliyemtaja kama kibaraka wake.
Baada ya kuingia mamlakani, viongozi waliochaguliwa kutoka Mlima Kenya, akiwemo Bw Gachagua walimshambulia Bw Kenyatta huku baadhi wakihusishwa na njama za uvamizi katika shamba lake la Northlands, ambako mali iliharibiwa na kondoo kuibwa.
Hata hivyo, baada ya miaka miwili chini ya utawala wa Kenya Kwanza na kuondolewa kwa Bw Gachagua, wakazi wanaonekana kujuta kwa kupuuza ushauri wa Bw Kenyatta huku wakimtaka ajitokeze kuwapa mwelekeo wa kisiasa.
Bw Gachagua hakuachwa nyuma akijuta kwa “kutumiwa kumdhalilisha mfalme wa Mlima Kenya” Uhuru Kenyatta na kumuomba msamaha hadharani.
Kabla ya hoja ya kutimuliwa kwake mamlakani, Bw Gachagua alidai sehemu ya masaibu yake ni kuridhiana na Bw Kenyatta na kuhimiza umoja wa wakazi wa eneo la Mlima Kenya kisiasa.
Japo Bw Kenyatta hajawahi kutaja hadharani msamaha wa Bw Gachagua na iwapo alimsamehe anavyodai naibu rais huyo anayepigana kujiokoa kisiasa, maoni ya Wakenya baada ya Uhuru kuonekana hadharani yanaonyesha majuto na matumaini makubwa kwamba anaweza kutoa mwelekeo wa kuhusu hali ya siasa nchini.
“Ambia Uhunye tulimkosea kweli, tunajua alikasirika lakini tumeomba msamaha, huyu jamaa huku anatumaliza, arudi tu hata apige mahojiano/mkutano mmoja, itatupatia matumaini, mwambie mzazi hatupi watoto wake, anawaadhibu wanarekebisha,” Bonface [email protected] aliandika kwenye X.
Mkenya mwingine aliandika: “Kama kuna kitu anaweza kufanya atusaidie, tunaomba afanye na atakuwa ametusaidia sana.”
Wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa japo huenda hatashiriki siasa za makabiliano hadharani kutokana na wadhifa wake akiwa rais mstaafu, mwelekeo wa kisiasa wa Bw Kenyatta hasa kwa wakazi wa Mlima Kenya utapokelewa vyema.
“Sio Mlima Kenya pekee, Wakenya wamekuwa wakilinganisha utawala wake na wa sasa na kumsifu. Hii inaonyesha sauti yake inaweza kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini japo sidhani atafanya hivyo hadharani,” akasema mchambuzi wa siasa, Dkt Isaac Gichuki.