TAHARIRI: Malipo ya juu mahakamani yataua demokrasia
Na MHARIRI
Kwa Muhtasari:
- Mahakama inazidi kuwataka wanaopoteza kesi kuwalipa washtakiwa pamoja na IEBC mamilioni ya pesa
- Bi Wavinya Ndeti aliamriwa amlipe gavana Alfred Mutua na IEBC Sh10 milioni baada ya kupoteza kesi
- Majaji wanapaswa kuangalia upya kiwango cha malipo wanachowatoza wanaoshindwa
- Kuna uwezekano kwamba siku za usoni watu wataendeleza wizi waziwazi, wakijua hakuna atakayethubutu kuwashtaki
MALIPO ya juu ambayo wanaoshindwa kwenye kesi za uchaguzi wanatakiwa kulipa yanahatarisha demokrasia nchini.
Idara ya mahakama imeendelea kuwataka wanaopoteza kesi kuwalipa washtakiwa pamoja na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) mamilioni ya pesa.
Tukio la punde zaidi ni lile la amri ya Mahakama ya Busia kwamba mpiga kura Peter Odima alipe Sh12 milioni kwa kupoteza kesi ambapo alikuwa amepinga matokeo ya kuchaguliwa Gavana Sospeter Ojaamong. Bw Odima atalazimika kulipa pesa hizo kwa gavana huyo na pia IEBC.
Mnamo Ijumaa, aliyekuwa mbunge wa Kathiani, Bi Wavinya Ndeti aliamriwa amlipe gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua pamoja na IEBC, baada ya kesi yake ya kupinga matokeo kutupwa.
Jaji Aggrey Muchelule alimwamuru Bi Ndeti, aliyewania ugavana wa Machakos kwa tikiti ya chama cha Wiper, alipe Sh10 milioni, baada ya kukosa ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai ya kuzuiwa kwa maajenti wake wakati wa uchaguzi.
Kiwango kipunguzwe
Sheria kama ilivyo inahitaji kuwa anayepoteza kesi agharamike, lakini majaji wanapaswa kuangalia upya kiwango cha malipo wanachowatoza wanaoshindwa.
Lengo la kuwepo kwa idara ya mahakama ni kuwezesha kuwepo kwa utangamano, na kila mwananchi aishi akihisi kuwa ana uhuru wa kwenda kortini kulalama haki zake zinapokiukwa.
Si jukumu letu kumshauri Jaji Mkuu David Maraga kuhusu jambo hili, lakini kuna wasiwasi kuwa kuwatoza wanasiasa wanaopoteza kesi mamilioni ya pesa, kunaweza kukwamisha kukua kwa demokrasia nchini.
Inawezekana kuwa wapo baadhi ya wanasiasa wasiokubali kushindwa, na hutafuta kila mbinu kuhakikisha uchaguzi unarudiwa, ili wabahatishe tena.
Wizi waziwazi
Lakini Kenya wanasiasa hutumia kila mbinu kushinda uchaguzi. Kwa hivyo mtu anapohisi kuwa ameshindwa kwa njia isiyo halali, ni haki yake kwenda kortini.
Iwapo itaonekana kama kufanya hivyo kunastahili adhabu ya kulipa milioni kumi au zaidi, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba siku za usoni watu wataendeleza wizi waziwazi, wakijua hakuna atakayethubutu kupeleka kesi ya uchaguzi.
Tukifikia hatua hiyo, basi Kenya itakuwa nchi ya watu kuingia uongozini bila ridhaa ya wananchi.