Makala

ULIMBWENDE NA AFYA: Siri ya kuwa na ngozi yenye afya nzuri

April 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

VYAKULA vya asili vina virutubisho muhimu vinavyosaidia mwili kupambana na magonjwa na pia kuimarisha afya ya ngozi.

Miongoni mwa vyakula hivyo ni pamoja na vile vyenye asili ya kijani ambavyo huwa na uwezo mkubwa zaidi katika kuponya magonjwa na kusaidia kujenga mwili.

Sehemu kubwa ya miili yetu ni ngozi na ni sehemu muhimu ya mwili ambayo ina jukumu kubwa la kuukinga na kuufunika mwili na viungo mbalimbali. Hivyo afya yake pia ni vizuri ikazingatiwa.

Vyakula tunavyokula vinaweza kuchangia katika muonekano wa ngozi zetu na kusaidia kupambana na matatizo ya ngozi, ikiwa ni pamoja na kupunguza mikunjano ya uso na suala zima la afya na muonekano wa ngozi.

Ni wazi kwamba wengi hupenda kuonekana vizuri, lakini kutokana na kutokuwa na ufahamu sahihi juu ya namna ya kudumisha afya za ngozi zetu kutofahamu njia sahihi za kudumisha afya za ngozi zetu huchangia baadhi yetu kushindwa kufikia lengo na mara nyingine hujikuta tukijisababishia madhara makubwa yasiyotibika hapo baadaye.

Ni muhimu kujua kwamba kila tunachokula huwa ni moja ya sehemu ya miili yetu ikiwa ni pamoja na sehemu ya nje, hii ina maana kuwa kila tunavyokula vyakula bora ndivyo ngozi zinavyoonekana vizuri zaidi.

Vyakula hivi vinaweza kusaidia kuimarisha afya ya ngozi:

Asali

Asali ambayo hutengenezwa na nyuki kwa viambato au malighafi asilia ni chakula muhimu kwa ajili ya kuimarisha afya ya ngozi na pia afya ya binadamu. Hii ni kwa sababu kila kilicho kizuri katika afya yako ni kizuri pia kwa ngozi.

Kwa kawaida ngozi nzuri huhifadhi unyevu ili kuzuia kukauka na kupasuka na ndiyo maana huwa tunatumia mafuta ili kuifanya ngozi iwe na unyevu. Hivyo asali husaidia kutunza na kuhifadhi unyevu kwenye ngozi na ina kiwango kikubwa cha sukari na ‘acids’ ambazo huzuia vijidudu wanaozaliana kwenye ngozi.

Tumia asali kwa kupaka wakati wa kuoga, kisha acha kwa muda kabla ya kuiondoa. Kufanya hivyo husaidia kuinawirisha ngozi.

Mayai

Kiini cha yai huwa na vitamini A na B huku sehemu yenye ute ikiwa na protini nyingi ambayo ni muhimu pia kwa ngozi. Ute wa yai ni muhimu katika kuifanya ngozi kuwa nyororo na yenye kung’aa na pia husaidia ngozi kujilinda vizuri dhidi ya mionzi ya jua.

Chungwa na limau

Bidhaa hizi ni muhimu pia katika kuimarisha afya ya ngozi kwa sababu husaida kutengeneza collagen ambayo ni aina ya protini inayotengeneza ngozi. Vitamini C husaidia sana kuondoa uvimbe na mikunjo ya ngozi na hivyo kuilinda ngozi isizeeke mapema.

Mboga za majani

Ni muhimu kwa afya ya ngozi kama tujuavyo zimesheheni vitamini na virutubisho vya aina mbalimbali vyenye faida kubwa kwa ngozi na mwili kwa ujumla. Kama unataka uwe na ngozi nyororo usisahau kula mboga hizi za majani kwani husaidia ngozi kuzalisha seli mpya na kuondoa zile zilizokufa. Hivyo kupunguza ukavu na kutunza ngozi na kuifanya ing’are na kuvutia.

Vyakula vya baharini

Kwa ujumla vyakula hivi ni vizuri kwa afya ya ngozi. Vyakula vingi vya baharini vina kiwango kikubwa cha Zinc na Omega 3 ambayo ni muhimu kwa siha ya ngozi. Faida za Omega 3 ni pamoja na kuondoa kukakamaa au ukavu wa ngozi, kupunguza kuvimba na kukunjamana kwa ngozi na husaidia mzunguko mzuri wa damu mwilini hivyo kuboresha ngozi.

Jenga au fanya kuwa mazoea ulaji wa vyakula vyenye lishe bora kwa kuwa na ngozi bora zaidi. Pia kunywa maji kwa wingi.