Maoni

Maoni: Trump ataangushwa na wanawake

Na DOUGLAS MUTUA August 26th, 2024 4 min read

UMEWAHI kutazama runinga, ukamuona mtu wa kwenu kijijini, ukatamani kumuuliza ‘ulipotelea wapi? Mbona hututembelei nyumbani’?

Juzi nilitamani kumuuliza maswali hayo rais wa 44 wa Amerika, Barrack Obama, alipotoa hotuba ya kusisimua ajabu kwenye Kongamano la Kitaifa la chama cha Democrat (DNC).

Nakuapia nitamuuliza maswali hayo nikikutana naye kwenye mitaa ya jiji la Washington, D.C. anakoishi baada ya kustaafu mnamo mwaka 2017.

Nitamkumbusha kauli yetu sisi Waafrika – na yeye ni mmoja wetu – inayosema kwamba ahadi ni deni, nayo dawa ya deni ni kulipa.

Ana deni letu kwa kuwa alituahidi kwamba akistaafu angetutembelea nchini Kenya mara kwa mara, sasa hana majukumu mengi kama zamani, lakini bado hajatimiza ahadi hiyo.

Tunamsubiri.

Japo sasa ni mstaafu, nadhani Obama anathamini amani na heshima zake zaidi.

Mambo yanayoendelea nchini Kenya yanaweza kukufanya kichaa, ukaokota takataka na kula kwenye mapipa ya taka pamoja na nguruwe, ukajifedhehesha.

Hata ingekuwa wewe, ungejisumbua kuzuru nchi ambako mambo yanakwenda visivyo, kuna wafanyakazi hewa wa serikali wanaolipwa mishahara, shule hewa za umma zinazopata migao ya fedha kila mwaka? Unaweza?

Hata ingekuwa wewe, ungezuru nchi ambako mibabe iliyoambatwa na taasubi ya kiume inamtimua ofisini, tena kwa kurudia, gavana wa kike kwa sababu haiamini inapaswa kuongozwa na mtu anayevaa rinda?

Mwanguko wa Kawira Mwangaza wa Meru ni ithibati ya kiza kinachotutawala.

Mwangaza akipata kiza mahakamani, Meru itakumbukwa milele kwa kulima mirungi ya kulewesha, kuuzia nchi nzima mbolea yenye mchanga na kuwadhalilisha wanawake.

Amini usiamini, watu wenye heshima zao kama Obama mwana wa K’ogelo wana akili razini zisizowaruhusu kujipaka matoke wakitagusana na watu wachafu, wasio na tatizo wakipigana miereka na nguruwe.

Kenya ni nchi inayojulikana sana ughaibuni kwa mambo makuu inayofanya duniani, lakini baadhi ya yanayofanyika ndani ya nchi ni ya kuudhi, na wengi hawangetaka kunasibishwa nayo.

Tufagieni nyumba yetu ili tuwafukuze viroboto, kupe, funza, vipepeo, viwavi na wadudu wote waharibifu ili tuepuke maradhi na fedheha, tuwavutie watu wa heshima kutoka kote duniani, watalii, wawekezaji na hata wasomi wazito.

Rais Obama, aliye na asili ya Kenya kwani marehemu babake alikuwa Mkenya, amerejea kwenye ulingo wa siasa kwa fujo, si kuwania urais tena, bali kumpigia debe mwandani na mwanafunzi wake wa kisiasa: Bi Kamala Harris.

Pamoja na mkewe, Michelle Obama, wameleta mwamko mpya katika chama cha Democrat na siasa za Amerika kwa jumla, wakatukumbusha miaka ambapo waliishi Ikulu ya White House na heshima za watu walioleleka na kuelimika vizuri.

Kelele za kuwashangilia zingekutoboa masikio, sikwambii na jumbe zao zilizo kama manukato, za kuwapa Waamerika matumaini.

Waliwakumbusha Waamerika unoko wa Donald Trump, miaka minne aliyoishi Ikulu na machafuko aliyoleta, migawanyiko aliyoibua, mbegu ya chuki aliyopanda, wakawahimiza wamzuie kuendelea na sinema hiyo kwani, kwa kawaida onyesho la pili huwa baya zaidi.

Kamala, ambaye ndiye Makamu wa Rais wa Amerika, anawania urais dhidi ya mrithi wa Obama, Trump, dume tatanishi kupitiliza ambalo huwatukana matusi ya nguoni wanawake, huchukia watu Weusi, huigiza walemavu na kusema heri wafe, hudharau maskini.

Hakika, Obama angehusishwa, hata kwa mbali sana, na moja kati ya mambo hayo ya kuudhi alipokuwa madarakani, angetafutiwa njia za kumtimua na kumsawiri kama mtu aliye na hulka ya mnyama.

Michelle alizungumzia jinsi Trump alivyojikakamua kuwachochea Waamerika kuwaogopa na kuwachukia yeye na mumewe, mbinu ambazo Trump amekuwa akitumia kumdhalilisha Kamala, aliyezaliwa na mama Mhindi na baba mweusi kutoka Jamaica.

Raha iliyoje kuwaona makada wa ngazi za juu wa chama cha Democrat wakiwakumbusha Waamerika kwamba siasa za chuki na matusi hazifai, kuwaasa wafanye siasa za uungwana na wala si za chuki anaoeneza Trump.

Kwenye kongamano hilo, Kamala aliidhinishwa rasmi kubeba mwenge wa chama cha Democrat, thibitisho kwa Trump kwamba hakika atakutana naye kwenye midahalo miwili inayotarajiwa kutoa cheche kali mwezi ujao, na ndani ya debe mnamo Novemba 5.

Haikosi thibitisho hilo linamkosesha usingizi Trump; chama cha Democrat kilimgeuzia kibao hivi majuzi kilipomshawishi Rais wa sasa, Joe Biden, asiwanie dhidi yake kwa sababu ya uzee, kikamuunga mkono Kamala.

Amini usiamini, kugeuziwa kibao ghafla kulimpa Trump kichaa, akaanza kuropokwa, akashindwa kufanya mikutano ya hadhara ya kampeni, watu wake wakaungama kibao kimekula kwake, akasubiri Democrat wamalize kongamano lao ili ajue ataanzia wapi tena!

Daah! Msisimko ninaoshuhudia huku hauna mfano wake. Watu wanaweka nembo za kumdhihaki Trump na kumsifia Kamala kwenye magari yao bila kificho, wakitazamana wanacheka kana kwamba kuambiana ‘tusubiri siku ya kura ifike tumtie adabu fidhuli!’

Kambi ya Trump imedhihaki utasa wa wanawake wasio na watoto kwa kufuga paka badala ya kuzaa na kulea watoto, nao wamejibu kwa kuweka picha za paka kwenye madirisha ya magari yao na kutangaza: “Mimi ndimi mwanamke mfugaji paka!”

Mapema leo nilikutana na bi-vizee waliokuwa na nembo hizo waakiendelea na shughuli zao madukani. Nao wasichana wasiozidi umri wa miaka 20 wakiketi chini kwenye maegesho na kuichekea kwa furaha nembo hiyo.
Vimwana hao waliovalia kaptura kutangaza haki zao na uhuru wanaofurahia kwa kuwa wanawake nchini Amerika waliapa kumzuia Trump kuwa chochote nchini mwao.

Suala tata la marufuku ya uavyaji mimba ambalo Trump amekuwa akilitumia kusawiri Democrat kama chama cha wauaji limemgeuka vibaya kwa kuwa limefafanuliwa kwa mapana na marefu.

Ajabu akidi ni kwamba limetokea kuwaunganisha wanawake wa vyama vyote viwili dhidi ya Trump kwa sababu marufuku hiyo pia inawanyima misaada wa kisayansi walio na changamoto ya kutunga mimba kwa kujamiiana kikawaida.

Mbinu ya wanasayansi kuunganishia kwenye maabara yai la mwanamke na mbegu ya mwanamume na kisha kuyapanda kwenye kizazi cha mwanamke ni marufuku kwenye majimbo mengi.

Trump na wenzake kwenye chama cha Republican wamenukuliwa wakishangilia hali ya taharuki iliyosababishwa na maruguku hiyo, jambo ambalo limemfanya adui nambari moja wa wanawake.

Wameapa kujitokeza kwa fujo kumpinga kwa kumchagua Kamala.

Suala la haki za wanawake limetokea kuugubika msimamo wa kuudhi wa chama cha Democrat kuunga mkono ushoga, mashoga nao wanaonekana kujifunza kutotanua vifua, kutotembea kwa mwendo wa aste-aste na kutoonyesha bendera yao ya upinde wa mvua hadharani.

Kwa ufupi, hata mambo ya kuudhi ambayo kwa kawaida huhusishwa na Democrat yanafumbiwa macho kwa sababu hayana uzito kama maudhi ya Trump, mhalifu aliyekutwa na hatia mara 34, ila aliyediriki kuwania wadhifa wa kuilinda na kuitetea Katiba ya Amerika.

Muujiza usipomtendekea Trump kati ya sasa na siku ya Uchaguzi Mkuu, ataingia kwenye kumbukumbu kama mwanasiasa aliyekomeshwa na wanawake alipothubutu kutumia unoko kushinda uchaguzi.

Kwa sasa, yeye na wao ni pamba na moto!

[email protected]