MAONI: Kenya isiingilie mizozo ya majirani
AMA Kenya ina watunga-sera hafifu wa mashauri ya kigeni, wataalamu wa mawasiliano wasiotosha mboga, au viongozi wa ngazi ya juu zaidi ambao kamwe hawafuati ushauri wa wataalamu wa diplomasia.
Nimeishia kushuku hivyo baada ya kuona jinsi, katika muda mfupi tu, taifa letu linavyoendelea kujikwaa linaposhughulikia masuala ya kimataifa, hasa Barani Afrika.
Unaposoma makala hii, Kenya inalaumiwa kwa kuingilia masuala ya ndani kwa ndani ya mataifa kadha Barani Afrika: Sudan Kusini, Sudan, Ethiopia, Morocco, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Hapa pana jambo na ni sharti tulishughulikie kwa wepesi unaostahili, si kuendelea kulikanusha, kisa na maana uzalendo au utaifa usio na tija.
Mataifa hayo yote hayawezi kuwa yanaichukia au kuisingizia Kenya, iwe kwamba nchi yetu ndiyo pekee inayoendesha mambo kisawasawa.
Haikosi kiherehere chetu kimewasababisha majirani kuguna kwamba mtagusano wetu nao unawaumiza.
Siku chache zilizopita, Sudan Kusini na Sudan (Khartoum) zilijitoa kimasomaso na kukosoa mambo tofauti ambayo yalitamkwa na viongozi wetu.
Sudan Kusini ililalamika kwamba Bw Raila Odinga – mjumbe maalum aliyetumwa na Serikali ya Kenya kujaribu kumpatanisha Rais Salva Kiir na Makamu wake, Dkt Riek Machar – alisema mambo yasiyo ya kweli wakati wa ziara yake jijini Juba.
Rais Kiir alisema madai ya Bw Odinga kwamba Dkt Machar na mkewe, Bi Angelina Teny, ambaye pia ni Waziri wa Ndani, wamefungwa kifungo cha nyumbani, si ya kweli.
Serikali hiyo ilifafanua kwamba aliyezuiliwa ni Dkt Machar, Bi Teny yuko huru huria, na ikaendelea kumtambua kama waziri wa serikali, kauli ambayo ni kinyume na matamshi yaliyotolewa na Bw Odinga aliporejea nchini.
Sudan Kusini pia ilikosoa madai ya Bw Odinga kwamba alipoomba kukutana na Dkt Machar, Rais Kiir alikataa na badala yake akamwambia ashauriane na Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Sudan Kusini ilisema mkutano kati ya Bw Odinga na Rais Museveni ulipangwa mapema kabla ya Bw Odinga kuelekea Juba.
Ukisikia majibizano hayo mwanzo unakanganyikiwa na kujiuliza msema kweli ni nani, halafu unakumbuka Kenya imejipata katika hali hiyo kwingineko tangu mwaka 2022.
Kabla ya Sudan Kusini kulalamika kuhusu matamshi ya Bw Odinga, Sudan (Khartoum) nayo ilitoa taarifa kukanusha madai yaliyotolewa na Rais William Ruto kwamba, hata baada ya Sudan kuzuia bidhaa za Kenya kuuzwa ndani ya mipaka yake, tungali tunauza majani-chai huko.
Serikali ya kijeshi ya Sudan ilikuja juu na kusema kuwa tangu ilipotoa amri ya bidhaa za Kenya kutouzwa nchini humo mapema mwezi jana, haijabatilisha amri hiyo na wala hakuna bidhaa zetu zozote zinazoingizwa huko.
Kumbuka serikali ya Sudan, inayoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, 2024 ilimkataa Dkt Ruto kuwa mpatanishi wake na kiongozi wa vikosi maalum vya Sudan, Jenerali Mohamed ‘Hemedti’ Hamdan Dagalo.
Wakati huo Dkt Ruto alilaumiwa kwa kile kilichoitwa kumpendelea Jenerali Hemedti, madai aliyokanusha.
Hata hivyo, Dkt Ruto aliliruhusu kundi la Jenerali Hemedti kukutana jijini Nairobi na kuunda serikali mbadala ya kuipinga ile ya Jenerali Burhan.
Ni hatua hiyo ya Nairobi kukubali kutumika kama jukwaa la kuundia na kuzindulia serikali mbadala ambayo ilisababisha Jenerali Burhan kuiwekea Kenya vikwazo vya kiuchumi.
Malalamiko kwamba Kenya inaingilia masuala ya ndani kwa ndani yalitolewa na serikali ya DRC pale kundi tanzu la waasi wa M-23 lilipozinduliwa jijini Nairobi mwaka jana.
Ethiopia na Morrocco zinatulaumu kwa masuala kama hayo pia.
Panapofuka moshi hapakosi moto; madai hayo yote hayawezi kuwa ya uongo. Miaka iliyopita Kenya haikujulikana kwa kuvuruga mambo, ilisifika kwa kuwapatanisha wagombanao.
Hebu na turejeeni huko kwa kuwa wapatanishi, kwa kurekebisha sera ya diplomasia na kitengo kizima cha mawasiliano katika wizara ya mambo ya nje, nao viongozi wetu wafuate ushauri wa wataalamu, si kujikwaa ndimi kiholela. Hayo ni mazoea.