Maoni

MAONI: Sakaja asitumie Gachagua kama sababu ya kufeli kama gavana wa Nairobi

Na BENSON MATHEKA October 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

ANAPOJIANDAA kufika katika Bunge la Kitaifa kuunga mashtaka ya kuondolewa ofisini kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja Arthur ana maswali kadhaa anayopaswa kujibu wakazi wa kaunti yake.

Japo anamhusisha Bw Gachagua na madai ya kupinga mpango wake wa kuhamisha wafanyabiashara kutoka katikati ya jiji hadi barabara ya Kangundo na kuondoa msongamano wa magari jijini, Bw Sakaja anasahau kuwa akiwa Gavana, hakuna anayepaswa kumuelekeza kuhusu jinsi ya kufanya kazi yake.

Hivyo basi, asijaribu kutumia hoja ya kumtimua Bw Gachagua kama kisingizio cha kushindwa  wa serikali yake ya kaunti kuhudumia wakazi. Sidhani ni Gachagua anayefanya mashimo kujaa katika barabara za jiji ambalo Bw Sakaja aliahidi kurekebisha.

Sidhani ni Bw Gachagua anayefanya taka kukosa kuzolewa hadi Rais William Ruto akakiri jiji linanuka. Mashimo yaliyo katika barabara za Nairobi yalionekana mara ya mwisho miaka 23 iliyopita chini ya utawala wa Kanu.

Ni aibu jiji kurudi katika hali lililokuwa miongo miwili iliyopita  wakati mapato yake yameimarika. Japo kuna changamoto ambazo hazikuwepo miaka iliyopita, Bw Sakaja hana sababu ya kutetea kushindwa kwake kuachilia barabara za Jiji kuharibika hadi kufikia hali ya sasa.

Watangulizi wake Evans Kidero na Mike Sonko wanaonekana kufanya kazi bora katika urekebishaji na uboreshaji wa jiji kuliko Bw Sakaja ambaye tofauti na wao, ana uhusiano mwema na Serikali ya Kitaifa.

Licha ya kupigwa vita ikiwemo wafanyabiashara kuchochewa kuandamana kupinga utawala wake, Dkt Kidero hakuachilia barabara za jiji kuharibika na taka kujaa kote.

Kabla ya Bw Sonko kusukumiwa Shirika la Kusimamia Nairobi (NMS) alikuwa ameanzisha kampeni ya kukarabati barabara na kuboresha jiji kwa kupanga miti na maua.

Miaka miwili ya utawala wa Sakaja, hali ya Jiji inazidi kuwa mbaya na hafai kubebesha lawama mtu mwingine.