Michezo

Arsenal waingiwa na kiwewe ukame utazidi baada ya Liverpool kuendelea kutisha

Na GEOFFREY ANENE February 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MASHABIKI wa Arsenal wameanza kuhofu kwamba msimu huu wa 2024-2025 watatoka mikono mitupu baada ya Liverpool kuonyesha nia ya kufagia makombe yote manne inayoshiriki, kufuatia ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye kipute cha Carabao Cup mnamo Alhamisi usiku.

Liverpool wanaongoza Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 56 baada ya kujibwaga uwanjani mara 23. Vijana wa kocha Arne Slot wako alama sita mbele ya Arsenal ya kocha Mikel Arteta ambayo pia imesakata mechi moja zaidi.

Liverpool walizima Spurs 4-0 kupitia mabao ya Cody Gakpo, Mohamed Salah (penalti), Dominik Szoboszlai na Virgil van Dijk kwenye mkondo wa pili wa Carabao Cup ugani Anfield kutinga fainali kwa jumla ya mabao 4-1. Reds walikuwa wamepoteza 1-0 mkondo wa kwanza katika uwanja wa Tottenham Hotspur Stadium.

Virgil van Dijk (kati) wa Liverpool asherehekea kufunga bao na Mohamed Salah (kulia) dhidi ya Tottenham kwenye Carabao Cup, Alhamisi. PICHA | REUTERS

Mabingwa watetezi Liverpool watavaana na Newcastle katika fainali ugani Wembley hapo Machi 16. Newcastle walikanyaga Arsenal 2-0 uwanjani Emirates hapo Januari 7 na 2-0 ugani St James’ Park mechi ya marudio Jumatano usiku.

Vijana wa Slot pia wako katika raundi ya nne ya Kombe la FA ambapo watakutana na wanyonge Plymouth Argyle kesho Jumapili.

Isitoshe, Liverpool wako raundi ya 16-bora kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kwa upande wao, Arsenal wameaga Carabao na FA baada ya kupoteza mikononi mwa Newcastle na mabingwa watetezi Manchester United mtawalia.

Vijana wa Arteta wana uwezo wa kuwania taji la UEFA lakini watalazimika kufanya kazi ya ziada. Watakutana na AC Milan, PSV Eindhoven, Feyenoord ama Juventus katika raundi ya 16-bora.

Kambini mwa Arsenal, Arteta ameshinda Kombe la FA msimu 2019-2020 na Ngao ya Community Shield 2020-2021 na 2023-2024.

Matamanio makubwa ya mashabiki ni kuona Arsenal wameshinda EPL ambayo wana ukame wa miaka 20 sasa. Vile vile, Arsenal haijawahi kushinda UEFA.