Hakuna alama zenu hapa, Ambani aambia Gor kuelekea Debi ya Mashemeji Jumapili
KOCHA wa AFC Leopards Fred Ambani amesema hajali iwapo Gor Mahia inasaka taji la Ligi Kuu (KPL) au la na wao wanalenga kupigana kwa jino na ukucha kushinda Debi ya Mashemeji uga wa MISC Kasarani mnamo Jumapili.
Mchuano huo mkubwa wa Ligi Kuu (KPL) utagaragazwa wakati ambapo K’Ogalo wanawinda taji lao la 22. Leopards nao wanaonekana kuwa na uwezo finyu wa kushinda taji hilo.
Hii itakuwa mechi ya 97 ya Mashemeji ambayo itakuwa inakutanisha Gor na Leopards nao mkondo wa kwanza uliogaragazwa mnamo Machi 30 ukiishia sare tasa ugani Nyayo.
Katika mechi ya mkondo wa kwanza timu hizo mbili zilishutumiwa kwa kuonyesha mchezo duni na kukosa kuyafuma magoli langoni.
Kufuatia kifo cha Katibu Mkuu wa AFC Leopards Gilbert Andugu, timu zitakuwa na muda wa dakika moja kumkumbuka na kumuenzi kabla ya mechi yoyote ya KPL kuanza.
Mashabiki ambao wapo eneo la wageni mashuhuri zaidi Kasarani (VVIP) watalipa Sh5,000 huku wale kwenye eneo la wageni mashuhuri na mashabiki wa kawaida wakilipa Sh1000 na Sh300 mtawalia kutazama debi ya Mashemeji.
Gor inawinda taji la KPL zikiwa zimesalia mechi tano msimu huu utamatike kwa kuwa wapo nafasi ya pili kwa alama 53. K’Ogalo wapo alama mbili nyuma ya Kenya Police na moja mbele ya Tusker.
Iwapo hali itasalia hivi na timu zote zishinde mechi zao zinazofuata, basi mshindi wa KPL ataamuliwa kwenye mtanange wa mwisho mnamo Juni 22.
Siku hiyo, Kenya Police itavaana na Gor Mahia huku Tusker ikicheza dhidi ya Kakamega Homeboyz.
Ambani alikiri kuwa Gor itakuwa ikipambana vikali kwenye debi hiyo kupata alama zote tatu lakini naye hataki kupoteza rekodi ya kutoshindwa na Gor kama mchezaji na kocha.
“Mechi ya wikendi itakuwa ngumu kwa sababu Gor inapigania ubingwa wa KPL nayo sisi hatuko tayari kupoteza tukilenga kumaliza kwenye nafasi bora. Nimewaambia wachezaji wangu wasiniangushe,” akasema Ambani, ambaye alishinda KPL na Ingwe mnamo 1998.
“Hata kama hatuko kwenye kinyángányiro cha KPL, siko tayari na nipo tayari kuhakikisha tunapigana na kushinda,” akaongeza.
Gor ikipigwa na Leopards, itakuwa pigo kwao hasa Police wakishinda Bandari kule Mombasa nao Tusker wakipige FC Talanta Nairobi.
Ambani pia alitoa wito kwa mashabiki wa Leopards wajitokeze kwa wingi ili Gor nao wapate pesa. Kwenye mkondo wa kwanza Ingwe ilipata Sh7.3 milioni kwenye debi ya Mashemeji.
Leopards ilishinda Gor mara ya mwisho mnamo Mei 14, 2023 ikitwaa ushindi wa 2-1 uwanja wa Nyayo. Gor nayo ilipiga Ingwe kwenye mechi ya mkondo wa pili msimu uliopita ambapo waliwahi ushindi wa 1-0 mnamo Aprili 24.