Dimba

Liverpool hawashikiki, Arsenal waponea nao Forest waangukia pua

Na GEOFFREY ANENE, MASHIRIKA January 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ARSENAL wamepata nafasi ya kupumua katika nafasi ya pili baada ya kupunguza presha kutoka kwa Nottingham Forest walipoponyoka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Wolves, huku viongozi Liverpool wakidumisha pengo la alama sita kwa kupiga Ipswich Town 4-1, Jumamosi.

Vijana wa kocha Mikel Arteta wanasalia nambari mbili kwenye ligi hiyo ya klabu 20 baada ya ushindi huo mwembamba kuimarisha alama zao hadi 47.

Ushindi wenyewe haukupatikana kwa urahisi kwani Arsenal walipata pigo dakika ya 43 wakati Myles Lewis-Skelly alilishwa kadi nyekundu ya utata kwa kuchezea Matt Doherty visivyo.

Hata hivyo, wanabunduki hao waliendelea kujituma na kupata mpenyo dakika ya 74 baada ya beki Riccardo Calafiori kukamilisha krosi ya Gabriel Martinelli.

Dakika nne tu kabla ya bao hilo, Wolves pia walisalia wachezaji 10 uwanjani kufuatia kadi nyekundu kwa mchezaji Joao Gomes. Calafiori aliingia nafasi ya kiungo chipukizi Ethan Nwaneri mapema katika kipindi cha pili.

Beki Riccardo Calafiori (kushoto) wa Arsenal asherehekea na difenda William Saliba baada ya kufunga bao dhidi ya Wolves ugani Molineux, Jumamosi. PICHA | REUTERS

Nambari tatu Forest waliokuwa sako kwa bako na Arsenal kwa pointi 44, waliaibishwa 5-0 na wenyeji Bournemouth kupitia mabao ya Dango Ouattara (matatu), Justin Kluivert na Antoine Semenyo. Tricky Trees hawana ushindi dhidi ya Bournemouth katika mechi 10 sasa.

Vijana wa kocha Nuno Espirito Santo hawakuwa wamepoteza michuano tisa iliyopita kabla ya kichapo kikali kutoka kwa Bournemouth wanaoimarisha rekodi yao ya kutoshindwa katika mashindano yote hadi mechi 12.

Newcastle United wako katika nafasi ya nne kwa alama 41 baada ya kubwaga wenyeji Southampton wanaovuta mkia 3-1. Newcastle waliona lango kupitia kwa Alexander Isak (magoli mawili) na Sandro Tonali.

Saints walitangulia kutetemesha nyavu za Newcastle kupitia kwa Jan Bednarek, lakini wakapoteza mwelekeo baada ya Isak kusawazisha 1-1 kwa njia ya penalti.

Ushindi huo ni wa kihistoria kwa Newcastle kwani wameshinda mara nne mfululizo ligini kwa mara ya kwanza tangu Oktoba 1996. Isak naye sasa ni mchezaji wa kwanza kabisa wa Newcastle kufungia klabu hiyo katika michuano mitano mfululizo ya ligi ugenini. Amempiku Peter Beardsley aliyefungia Newcastle mara nne mfululizo mwezi Desemba 1993.

Dango Ouattara (kulia) wa Bournemouth asherehekea kufunga bao huku wachezaji wa Nottingham Forest wakivunjika moyo uwanjani Vitality, Jumamosi. PICHA | REUTERS

Chini ya kocha wao mpya David Moyes, Everton wanaendelea kufufuka baada ya kulemea wenyeji Brighton 1-0 kupitia penalti safi kutoka kwa Iliman Ndiaye iliyopatikana kabla ya mapumziko. Brighton sasa hawana mara tano mfululizo kwenye ligi nyumbani.

Liverpool ya kocha Arne Slot ilibomoa washiriki wapya Ipswich Town 4-1 ugani Anfield kupitia mabao ya Cody Gakpo (mawili), Dominik Szoboszlai na Mohamed Salah anayeongoza ufungaji wa mabao ligini humo msimu huu. Jacob Greaves alifungia Ipswich bao la kujifariji katika dakika za majeruhi.

Liverpool wana alama 53 na pia mechi moja ya akiba dhidi ya Everton. Wamekung’uta timu zilizopandishwa daraja kushiriki Ligi Kuu mara 11 mfululizo ugani Anfield.