Michezo

Mihic: Lazima tupige Leopards debi ya Mashemeji Jumapili

Na CECIL ODONGO March 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA wa Gor Mahia Sinisa Mihic amewataka mashabiki wa timu hiyo wajazane katika uga wa kitaifa wa Nyayo huku akiahidi kuwa wanatarajia kupata ushindi mkubwa kwenye Debi ya Mashemeji wikendi hii dhidi ya AFC  Leopards.

Mchuano huo wa Ligi Kuu (KPL) unaohusudiwa na wengi, utachezwa katika uga wa Nyayo wenye uwezo wa kuwasitiri mashabiki 20,000. Mtanange wenyewe utaanza saa tisa mchana na timu zote zimekuwa zikishiriki mazoezi makali kuelekea mchuano huo.

Hii itakuwa debi ya kwanza kwa Mihic raia wa Croatia ambaye aliteuliwa kama kocha wa Gor mnamo Februari 3. Amewahakikishia  mashabiki wa K’Ogalo kuwa debi hiyo ni mchuano wa kawaida na atazoa alama zote kwa sababu vijana wake wamejiandaa vyema.

“Kila kitu kinaendelea vyema kimaandalizi kwa mechi yetu dhidi ya  AFC Leopards. Tunaweka mikakati ya kuwaadhibu vizuri,” Mihic akaambia Taifa Leo.

“Tuna nafasi ya kuzoa alama zote tatu na tutaelekea mechi hiyo kitaaluma na kwa umakinifu. Huu ni mchuano ambao lazima tuushinde,” akaongeza.

K’Ogalo imekuwa ikiendelea na mazoezi kabambe uwanjani Mpesa Academy na hivi leo itafanya mazoezi uga wa Nyayo kwa maandalizi ya debi.

Msimu huu Gor haijakuwa wembe jinsi ambavyo imekuwa katika misimu ya nyuma.

Kwenye mechi tano ambazo amesimamia, Mihic ameshinda tatu huku mechi mbili zikiishia sare.  Baadhi ya mashabiki wa Gor wamekuwa wakimshinikiza Mihic ajitume na kikosi chake ili waadhibu Leopards,  wakimwaambia ni mwiko kushindwa na Ingwe.

Kiungo wa Gor Enock Morrison alisema kuwa hawana jingine ila kuwapa mashabiki wao burudani kwa kuengua Leopards.

“Kila mtu anataka kuanza debi, tuna nguvu na kila mchezaji anajituma mazoezini. Tumekuwa tukisubiri mchuano huu kwa kipindi na lazima tupate ushindi,” akasema Morrison.

Kauli yake imeungwa na nahodha Philemon Otieno ambaye amesema mchuano huo ni spesheli na wanalenga kusalia na ubabe wao wa kulemea Leopards.

“Tutajituma sana tukilenga ushindi kwa sababu Leopards ni mpinzani mgumu na maandalizi yetu ni muhimu. Kila mtu yupo tayari kwa mchuano huo,” akasema Otieno.

Msimu uliopita, Gor ilishinda mechi ya mkondo wa kwanza 2-0 na pia wakatwaa alama zote mkondo wa kwanza wakishinda 1-0. Mara ya mwisho Ingwe kushinda Gor ni mkondo wa pili wa 2022/23 wakipata ushindi wa 2-1 mnamo Mei 14, 2023.