Pipeline na Prisons wazuiwa kufanyia mazoezi Kasarani
Na GEOFFREY ANENE
KLABU za Pipeline na Prisons, ambazo zitapeperusha bendera ya Kenya katika mashindano ya voliboli ya Bara Afrika mnamo Machi 6-15, 2018, zimefungiwa nje ya ukumbi wa kimataifa wa Kasarani.
Mabingwa mara saba wa Afrika, Pipeline, na Prisons, ambao wana mataji matano ya Afrika, wamekuwa wakitumia uwanja huo wa pekee wa kimataifa nchini Kenya kwa maandalizi yao kwa karibu mwezi mmoja.
Taarifa kutoka Shirikisho la Voliboli la Kenya (KVF) zinasema ukumbi huo sasa unatumika kwa mashindano ya kimataifa ya tenisi ya meza.
“Pipeline sasa imelazimika kufanyia mazoezi ya viungo katika jimu yake mtaani Pipeline nayo Prisons imehamisha mazoezi yake hadi katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha KCA mtaani Ruaraka,” taarifa hiyo imesema Alhamisi.
Klabu hizi zinatarajiwa kutaja vikosi vyao vya mashindano wakati wowote kutoka Ijumaa na baadaye kuelekea Misri wikendi. Pipeline inanolewa na kocha Japheth Munala nayo Prisons iko chini ya David Lung’aho.