Michezo

Rais wa Burkina Faso alia timu yake ya taifa kufungiwa nje na Nigeria kuwania tiketi ya Kombe la Dunia 2026

Na MASHIRIKA October 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS wa Burkina Faso na shabiki mkubwa wa soka, Ibrahim Traore, anataka majibu kutoka kwa Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) kuhusu jinsi nchi yake ilivyobanduliwa kushiriki mechi za mchujo za kuingia Kombe la Dunia 2026 licha ya kumaliza na alama sawa na Nigeria.

Ushindi wa Super Eagles wa 4–0 dhidi ya Benin, uliwapa Nigeria nafasi kwa tofauti ndogo ya magoli (+7 dhidi ya +6) na kuwa moja ya timu nne-bora baada ya mechi za makundi za kufuzu hapo Oktoba 14.

Mambo yalibadilika baada ya CAF kuamua kwamba matokeo dhidi ya timu zilizomaliza mkiani kwenye makundi hayangehesabiwa katika kuamua washindi bora wa pili.

Uamuzi huo ulifuatia kujiondoa kwa Eritrea kutoka Kundi E kabla ya kuanza kwa mashindano, hali iliyolisababisha kundi hilo kubaki na timu tano pekee. Ili kudumisha usawa, CAF iliamua kufuta matokeo dhidi ya timu za mwisho kwenye kila kundi.

Uamuzi huo uliigharimu Burkina Faso, ambayo ushindi wao mkubwa wa 6–0 na 4–1 dhidi ya Djibouti ulifutwa.

Alama zao zikapungua kutoka 21 hadi 15 na tofauti ya magoli kutoka +15 hadi +6. Nigeria, kwa upande mwingine, iliendelea kutumia matokeo yao ya sare mbili za 1–1 dhidi ya Zimbabwe, na kumaliza na pointi 15, lakini tofauti bora ya magoli.

Matokeo hayo yamezua hasira jijini Ouagadougou. Duru kutoka Burkina Faso zinasema kuwa Rais Traore ameomba maelezo ya kina kutoka CAF.

Beki mkongwe wa Burkina Faso, Steve Yago naye alionyesha mshangao, akisema, “Ni jambo la ajabu sana. Unashinda michezo dhidi ya timu dhaifu kwenye kundi lako, halafu Nigeria wanamaliza juu yetu ilhali hawakuweza kupiga Zimbabwe. Inaonekana kushinda timu ya mwisho si jambo la maana tena.”

Kwa matokeo hayo, Nigeria waliungana na Gabon, Cameroon, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika michuano ya mchujo mwezi Novemba nchini Morocco kuamua ni timu ipi ya Afrika itakayocheza mchujo wa mabara kwa nafasi ya kingia Kombe la Dunia 2026. Burkina Faso waliowahi kufika fainali za Kombe la Afrika (AFCON), wamemaliza nafasi ya tano, wakikosa kwa bao moja pekee.

Imetafsiriwa na Geoffrey Anene