Michezo

Soka ya Italia kurejea kwa nusu-fainali ya Coppa Italia

June 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

JUVENTUS na AC Milan zitakuwa klabu za kwanza kurejelea soka ya Italia zitakapovaana Ijumaa ya Juni 12 katika mkondo wa pili wa nusu-fainali ya Coppa Italia.

Shughuli zote za soka nchini Italia zilisitishwa mnamo Machi 9, 2020 kutokana na virusi vya ugonjwa wa corona uliofanya Italia kuwa miongoni mwa mataifa yaliyoathiriwa zaidi duniani.

Mchuano wa mkondo wa kwanza wa nusu-fainali hiyo uliosakatwa mnamo Februari 13, 2020 ulikamilika kwa sare ya 1-1, bao la Juventus ambao ni mabingwa watetezi likifumwa wavuni kupitia penalti ya Cristiano Ronaldo.

Milan watakosa huduma za mvamizi mkongwe, Zlatan Ibrahimovic, 38, ambaye anauguza jeraha baya la mguu.

Fainali ya Coppa Italia imepangiwa kutandazwa Juni 17, siku tatu kabla ya kuanza upya kwa mechi za msimu huu katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Katika nusu-fainali nyingine ya Coppa Italia, Napoli watapania kuendeleza ubabe wao dhidi ya Inter Milan baada ya kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya vijana hao wa kocha Antonio Conte katika mkondo wa kwanza.

Mechi zote zitachezewa ndani ya viwanja vitupu japo Rais wa Shirikisho la Soka la Italia (FIGC), Gabriele Gravina amesema upo uwezekano wa mashabiki kuanza kurejea uwanjani kwa utaratibu fulani utakaotekelezwa kufikia mwisho wa msimu huu.

Wiki hii, iliamuliwa kwamba muda wa ziada katika mechi za kuwania mataji yote katika soka ya Italia isipokuwa Serie A, umefutiliwa mbali. Badala yake, timu husika zitaelekea moja kwa moja kupiga mikwaju ya penalti iwapo zitatoshana nguvu kufikia mwisho wa dakika 90 za mchuano wa mkondo wa pili.

Hadi kusitishwa kwa soka ya Italia mnamo Machi 9, 2020, zilikuwa zimesalia mechi 12 katika Serie A kwa msimu huu kukamilika rasmi huku Juventus wakiselelea kileleni mwa jedwali na mgongo wao kusomwa na Lazio.

Nusu-fainali ya mkondo wa pili wa Coppa Italia kati ya Juventus na Milan ilikuwa imeratibiwa kusakatwa Machi 4, 2020 kabla ya kuahirishwa na vinara wa jiji la Turin, Italia.

Mnamo Mei 20, 2020, FIGC ilifichua kwamba Agosti 2 ndiyo itakayokuwa tarehe ya mwisho kwa mechi zote za Serie A katika msimu huu wa 2019-20 kusakatwa.