HabariSiasa

MIGUNA MIGUNA: Ajipiga kifua kisha kukunja mkia na kusalia Canada

May 16th, 2018 2 min read

Na WYCLIFFE MUIA

MWANASIASA na wakili mbishi aliyefurushwa nchini, Dkt Miguna Miguna alikunja mkia kuhusu kurejea Kenya Jumatano licha ya kusisitiza awali kuwa angerejea nchini, ije mvua au jua.

Bw Miguna, ambaye amejitangaza kiongozi wa vuguvugu la National Resistance Movement (NRM) hakutoa sababu maalum ya kukatiza safari licha ya msimamo wake awali kuwa alikuwa amepanga safari yake kikamilifu na angewasili uwanja wa JKIA mwendo wa saa kumi alasiri Jumatano.

Kwenye ujumbe alioweka kwenye mitandao akitangaza kuahirisha safari yake, Bw Miguna alisema muungano wa NASA umekufa na ODM sio chama cha upinzani tena kwani kimejiunga na Jubilee, na kuwa sasa NRM ndicho chama kipya cha upinzani.

Pia aliwahimiza wafuasi wake kuendeleza uwazi hadi atakaporuhusiwa kurudi nchini.

Alisema Idara ya Uhamiaji imekataa kutii agizo la mahakama la kumpa uraia wa Kenya na kuwa mawakili wake walimshauri asubiri.

Mnamo Machi, wakili huyo ambaye pia ana uraia wa Canada alizua vionja uwanjani JKIA aliporudi Kenya lakini akakatazwa kuondoka uwanjani humo.

 

Sindano ya kumlemaza

Alizima juhudi za kumwondoa kwa kuzua sarakasi za kila aina lakini hatimaye alirudishwa Dubai kabla ya kuelekea Canada. Alidai alidungwa sindano ya kumlemaza aliporudishwa Canada.

Hiyo ilikuwa mara ya pili kwake kufukuzwa nchini mwaka huu, mara ya kwanza ikiwa ni alipofurushwa muda mfupi baada ya kumwapisha Raila Odiniga kama “rais wa wananchi” mnamo Februari 28.

Kwa hatua yake ya jana, Bw Miguna aliwavunja moyo baadhi ya wafuasi wake ambao walikuwa wamesisimka kumpokea tena nchini.

Kabla ya kutangaza kusitisha kurejea kwake jana, alikuwa ameapa kurudi nchini liwe liwalo, na kudai hatua ya Kenya kumnyima pasipoti ili atumie ya Canada ni mtego.

Mapema mwezi huu, wakili huyo aliapa kurejea nchini: “Narudi Kenya Mei 16. Mimi ni Mkenya kwa kuzaliwa. Sharti serikali itekeleze maagizo ya mahakama ya kunipatia pasipoti yangu bila masharti.”

 

Aombe uraia upya

Hata hivyo, Idara ya Uhamiaji imesisitiza sharti wakili huyo ajaze fomu za kuomba uraia wa Kenya kabla ya kuomba pasipoti.

Mawakili wake pamoja na Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNCHR), wamekuwa wakishinikiza serikali impe pasipoti ili arejee nchini.

“Kwa sababu Idara ya Uhamiaji imekataa kunipa pasipoti na kunirejesha nchini bila masharti kama ilivyoagizwa na korti, nimeagiza mawakili wangu waripoti kwa mahakama kuwa serikali imekaidi maamuzi yake,” alisema katika ujumbe wake Jumatano akiwa Canada.

Naibu mwenyekiti wa KNCHR George Morara alisema korti inasubiriwa kutoa mwelekeo kufikia Ijumaa hii.

Wiki iliyopita, Katibu wa Idara ya Uhamiaji, Gordon Kihalangwa alisema bado Bw Miguna si Mkenya hadi atume maombi ya uraia.

“Idara haitampa pasipoti Miguna kwa sababu hajatuma maombi. Lazima kwanza apate uraia wa Kenya kabla ya kupata pasipoti,” alisema Kihalangwa.

Masaibu ya Dkt Miguna yalianza baada ya kuongoza kuapishwa kwa kinara wa upinzani Raila Odinga kama ‘rais wa wananchi’ mnamo Januari 30.
Siku chache baada ya kiapo hicho, Miguna alikamatwa na kupelekwa Canada.

 

Sarakasi JKIA

Mnamo Aprili 29, wakili huyo alifurushwa hadi Dubai baada ya siku tatu za sarakasi katika uwanja wa ndege wa JKIA, Nairobi.

Baadaye alisafiri kutoka Dubai hadi Canada ambapo amekuwa akiishi.

Dkt Miguna amekuwa akimshtumu Bw Odinga kwa kumtelekeza baada ya kumuapisha.

“Muafaka wao wa kisiasa unapasha kurejesha uongozi wa kisheria na wala si kelele za refaranda,”alisema Miguna

Wakili huyo alikana madai kuwa anapanga kutumia ‘vichochoro’ kuingia nchini adai ni njia ya kutaka kumuua.

“Wale wanapendekeza nipitie katika mipaka ya Tanzania au Ugandan kisiri wametumwa na Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. Wanataka kutumia maafisa wa usalama wa Uganda, Tanzania na Kenyan kuniteka nyara, waniue na wanizike katika makaburi fiche au wanitupe Ziwa Victoria.”