Habari MsetoMashairi

SHAIRI: Ukihitaji habari, tafuta Taifa Leo

April 18th, 2018 1 min read

Na KULEI SEREM

Gazeti la  Kiswahili, halina mapendeleo,
Nazungumzia lili, hili la  TAIFA LEO,
Gazeti lenye ukweli, wa habari ufunguo,
Ukihitaji gazeti, tafuta TAIFA LEO.

Kwa habari za nyakati, tena kwa lugha fasaha,
Maneno kwenye gazeti, si yale ya kimzaha,
Lina maandishi mufti, kweli linaleta raha,
Ukihitaji gazeti, tafuta TAIFA LEO.

Matukio yalojiri, hatupati kwa fununu,
Lina waandishi mahiri, shupavu na wenye mbinu,
Hakika zake habari, nazienzi kama tunu,
Ukihitaji gazeti, tafuta TAIFA LEO.

Taarifa sadikifu, zisizotiliwa chumvi,
Kwa Kiswahili sanifu, lugha iso na ugomvi,
Kwa habari timilifu, hadi kulikunja jamvi,
Ukihitaji gazeti, tafuta TAIFA LEO.

Tayari nimenunua, ninayo yangu nakala,
Kurasa nazipekua, najisomea makala,
Unaweza kununua, ufuatilie maswala,
Ukihitaji gazeti, tafuta TAIFA LEO.