Habari MsetoLugha, Fasihi na ElimuMashairi

BURIANI WALIBORA: Washairi watumia ubunifu wao kumwomboleza 'Shakespeare' wa Kiswahili

April 16th, 2020 32 min read

BURIANI PROFESA

Weye kweli ni shujaa, ninasema duniani

Kifo chako meduwaa, kusikia redioni

Mafunzoyo yatang’aa, daima ulimwenguni

Buriani Kiongozi, Profesa Ken Walibora.

 

Mukoya ninahuzuni, Mwandishi mempoteza

Mfanowe hapanani, wapekeye aliweza

Kiswahili ushindini, mchangowe ulikuza

Buriani Kiongozi, Profesa Ken Walibora.

 

Lijinyima waziwazi, kuboresha Kiswahili

Twakumbuka mtetezi, majukuani kamili

Walimu na wanafunzi, liwajenga nakubali

Buriani Kiongozi, Profesa Ken Walibora.

 

Miaka imeshasonga, vitabuvye mevisoma

Hakika alivitunga, kwa busara na hekima

Wallahi pia malenga, mshairi wa heshima

Buriani Kiongozi, Profesa Ken Walibora.

 

Wizara ino Elimu, gwiji alitambuliwa

Kalamuye lifahamu, shuleni litahiniwa

Guru Wallah Mwalimu, limtuza hilo juwa

Buriani Kiongozi, Profesa Ken Walibora.

 

‘Kidagaa’ meigiza, ndani Miale ya Njiwa

Kikundi chetu mecheza, shule tele natambuwa

Matukio yakuliza, mengine kufurahiwa

Buriani Kiongozi, Profesa Ken Walibora.

 

Alisawazisha vote, viumbe vake Jalali

Kupenda lipenda wote, wanadamu kihalali

Miito litika kote, likitunza Kiswahili

Buriani Kiongozi, Profesa Ken Walibora.

 

Inasikitisha Sana, mauti yamemteka

Hatunaye sisi tena, japo alichoandika

Waswahili kuungana, kauliye lisikika

Buriani Kiongozi, Profesa Ken Walibora.

 

Tamati yarahmani, mlaze pema pa wema

Mfungulie peponi, makosaye futa jama

Kwako Allah tarudini, tujalie mwisho mwema

Buriani Kiongozi, Profesa Ken Walibora.

Mukoya .H. Aywah,

Malenga Mpelelezi,

Lang’ata, Nairobi.

 

BURIANI WALIBORA

Gwiji Ken Walibora,alipendeza kikweli,

Kwetu alikuwa bora,litufaa Kila hali,

Leo kwetu ni hasara,mwenzenu sili silali,

Waridi limedondoka,buriani Waliaula.

 

Waridi limedondoka,tumebakia ukiwa,

Waja twasononeka,profesa kwondokewa,

Misingi aliyoweka,daima ataenziwa,

Johari tumepoteza,dunia inaomboleza.

 

Johari tumepoteza,kifo kimemchaguwa,

Laiti ungatweleza,mbeleni tungalijuwa,

Kiswahili kimefiwa,ela ndiyo majaliwa,

Jagina ametuacha,hapa kwetu ni kilio.

 

Jagina ametuacha,kidagaa kutwozea,

Kila usiku twakesha,machungu yamekolea,

Kifo ngetujulisha,chochote tungekupea,

Kito kimetuambaa,lala salama Walibora.

 

Kito kimetuambaa,ela aliyotwachia

Dawamu yatatufaa,nyayo zake kifwatia,

Lugha yetu itang’aa,fani zake kistawia,

Galacha ametuacha,makiwa wanalugha.

 

Galacha ametuacha,ahera ameiwahi,

Twanzie alipofikisha,kwa lugha na fasihi,

Lugha yetu kwimarisha,yalokombo kusahihi,

Mwalimu wetu wa dhati,tutaonana baadaye

 

Mwalimu wetu wa dhati,lugha lishughulikia,

Tuliipata bahati,vitabu kitwandikia,

Kumbe kuna Afiriti,nyumaye akunyatia

Profesa wetu ameaga,Afrika yaomboleza

 

Profesa ameaga,pasi kutupa kwaheri,

Nami hapa nafunga,kuhitimisha shairi,

Ela zako kunga,taweka hata dahari

Ua letu limedondoka,ni pigo kwa dunia.

Mtunzi:Wasuwa Maxwell

“Mpasuwa Allama”

Kahawa, Nairobi.

 

PEMA PEPONI WALIBORA

Yamejaa maozini, majonzi na huzuni

Mesononeka moyoni, maraha hapatikani

Sijui nifanye nini, ni mpango wa Manani

Ulazwe pema peponi, wetu Ken Walibora

 

Ni dua zetu mwandani, uliko uweni vyema

Akujalie Manani, kujazilie rehema

Kwa heshima na imani, ulale pema salama

Ulazwe pema peponi, wetu Ken Walibora

 

Likuwa mwenye imani, asiye hata kiburi

Aso inda asilani, siku zote mwenye heri

Ulitenda kwa makini, kwa mtima ninakiri

Ulazwe pema peponi, wetu Ken Walibora

 

Mengi sina kuyasema, tamati hapa mwishoni

Umetenda mengi mema, hapa kwetu mtaani

Najitoma kwa huruma, kwazo zangu shughulini

Ulazwe pema peponi, wetu Ken Walibora

Edward Ombui Almaarufu Malenga Mdogo

 

Wingu jeusi metanda,sononeko meingia

Sijui ta pakuenda, dunia yote yalia

Kovidi licha kutanda, muhibu menikimbia

Mola kusafie njia, Walibora taonana

 

Siku njema litupea, ila leo sio njema

Habari zinapepea, kigogo umetuhama

Majonzi yatulemea, baba na akina mama

Mola kusafie njia, Walibora taonana

 

Kiti hiki cha moyoni, sasa chanisonesha

Fasihi ino mbioni, daima uliboresha

Sasa nimo kilioni, moyoni menitonesha

Mola kusafie njia Walibora taonana

 

Kweli mti meanguka, kinda sasa tumeyumba

Japo si tuna hakika, tumebaki tukiomba,

Kifika kwa malaika, wakupokee mjomba

Mola kusafie njia Walibora taonana

Utunziwe mzazi Maina?

Malenga mwangamiza korona

 

LALA PEMA WALIBORA

Ni Kenya yote makiwa, yametufika tunayo

Nimeshachanganyikiwa, waniuma sana moyo

Fanya wepesi Moliwa, mazuriye yawe ndiyo

Lala pema WALIBORA, dua nyingi twakwombea

 

Ilikuwa ndoto yangu, kukutana nawe gwiji

Nahisi sana uchungu, sina wa kunifariji

Umesharudi kwa Mungu, umeacha pweke mji

Lala pema WALIBORA, dua nyingi twakwombea

 

Kazizo zilivyo safi, nyingine tutazimisi

Zilizojaa ucheshi, nayo lugha kwa ukwasi

Kunuka si kwa marashi, hunukia na ndo basi

Lala pema WALIBORA, dua nyingi twakwombea

 

Rambirambi nazituma, kwayo yake familia

Kifo chake chatuuma, ni kama tamthilia

Pigo kwa taifa zima, japo ndio yetu njia

Lala pema WALIBORA, dua nyingi twakwombea

 

Tusihuzunike sana, tusije tukakufuru

Amjalie Rabana, kaburi lipate nuru

Aweze kuepukana, adhabu isimdhuru

Lala pema WALIBORA, dua nyingi twakwombea

Malenga wa KONGOWEA

Kongowea Mombasa

Juma Zedi

 

*WALIBORA BURIANI..

Namuuliza Jalali, mbona mengine jamani

Ni matungu kweli kweli, Walibora chukuani

Kifo weye si halali, tunda mbichi wavunani

Hayafi uloandika, Walibora Buriani

 

Kote kote ni makiwa, ubunifu maarifu

Ni simanzi tumejawa, japo tungo tunasifu

Changamoto ulitowa, kiswahili sufusufu

Hayafi uloandika, Walibora buriani

 

Tumusifu Walibora, Kwa tungo zote jamani

uandishi na kuchora, na ulumbi tusemeni

Tuchoreni barabara, tukighani salamani

Hayafi uloandika, Walibora buriani

 

Nalilia usalama, barabara kisafiri

Kwa majonzi ninahema, ajali jitu hatari

Liandika Siku njema, Riwaya kifo bashiri

Hayafi uloandika, Walibora buriani

 

Kila mja alosoma, kazi zako ashangaa

Kifo mekosa huruma, Walibora tunalia

Hadi siku ya kiama, tutaonana Jalia

Hayafi uloandika, Walibora Buriani

 

Tamati ya Ziraili, japo mengi ulizani

Tumuombeni Jalali, unapoenda peponi

Akubariki kwa hali, atunusuru jangani

Hayafi uloandika, Walibora buriani.

Emmanuel Nyongesa

 

BURIANI KEN WALIBORA

1.Johari nakosa vina,hata mizani jamani

Urari pia hakuna,nabaki kutunga duni

Syamini hayupo tena,zimebaki buriani

Lala pema Walibora,ShakeSpear wa kwetu

 

2. Ulianza ja uvumi,jana na juzi jioni

Watu kawa hawasemi,fununu mitandaoni

Ya kuwa tarehe kumi,ulipotea nyumbani

Buriani Walibora,Mfalme wa fasihi

 

3.Nakumbuka kama jana, tukiongea simuni

Wazo kabadilishana, juu ya fasihi fani

Ukamba tutaonana,Corona ikiishani

Buriani Walibora, Mfalme wa fasihi

 

4.Tungo uliniahidi,nitumie kwa diwani

Shairi mbili zaidi,ukasema tanipani

Leo hauyupo badi,umetoka duniani

Buriani Walibora, Mfalme wa fasihi

 

5.Siku Njema meandika, kikatumika shuleni

Kidagaa kadhalika,ni nani asojuani

Na ndoto ya Amerika, na kipenda si utani

Buriani Walibora,Mfalme wa fasihi

 

6.Maskini Babu Yangu, Damu Nyeusi diwani

Na tamthilia chungu, zimejaa madukani

Na leo la kifo wingu,mekufunika mwandani

Buriani Walibora,Mfalme wa fasihi

 

7.Saba beti za Johari,za kusema Buriani

Naitimisha shairi, nifute chozi machoni

Metukumba kweli shari,soote ulimwenguni

Buriani Walibora,mfalme wa fasihi

Kipngeno Bett

 

MESHATUACHA GALACHA

Yanisuta yangu nafsi,nimebaki wakilio,

Faraja kwipa nafasi,wangu moyo situlio,

Mi Mwavitu binafsi,laniliza li tukio,

Meshatuacha galacha,buriani Walibora.

 

Lizipata zo habari,asubui na mapema,

Moyo haukua shwari,wangu mwili katetema,

Siku katiwa dosari,nikabaki kukakama,

Meshatuacha galacha, buriani Walibora.

 

Tulikua etieti,habari hatuamini,

Walibora si maiti,ugonjwa niwalini?,

Hadi kapazwa sauti,Walibora mocharini,

Meshatuacha galacha, buriani Walibora.

 

Gani nitaje liache?,aliyotenda mwalimu,

Vitabuvye sivichache,tenavilivyo muhimu,

Mioyo ikelekeche, tutakuenzi dawamu,

Meshatuacha galacha,buriani Walibora.

 

Swahili lipagania,kawa lugha ya taifa,

Chipukizi twavunia,jemedari yako sifa,

Japo hupo kwa dunia,twazindika taarifa,

Meshatuacha galacha,buriani Walibora.

 

Twakuomba ya Manani,Mrehemu wetu ken

Muhifadhi ko mbinguni,walio wema peponi

Alofanya duniani,muezeshe aherani,

Meshatuacha galacha,buriani Walibora.

John Mwavitu

Malenga wa Mwache

 

Buriani Mtoto wa Mwalimu

Sio tena siku njema, kidagaa kimeoza

Siyo sauti ya mama, taanzia yatuliza

Mauko yametufuma, Walibora kun’poteza

Kuvunjika kwa mdomo, mate yanatawanyika

 

Mtoto wa mualimu, metutoka Walibora

Mbiu kaja kama bomu, kwamba kifo metupora

Kusadiki ni vigumu, kuitikia kudura

Tumebaki tuna pengo, kisa kung’olewa jino

 

Kifo na mingi milango, kwa ajali metupoka

Meathirika vitengo, fasihi na kadhalika

Uli uti wa mgongo, ghafula umeondoka

Haina kinga ajali, apendalo makuduri

 

Kamanda wa Kiswahili, wa kikweli mzalendo

Kiswahili kukidhili, ulipinga kwa vitendo

Kandika kazi aali, zenye na mwingi uhondo

Amri yake Rahimu, kattu haina rufani

 

Titi mame kukomboa, liliona la kikati

Kauli mbiu za doa, za kigeni ndizo ati

Ajinabi kuvutia, kakataza si shuruti

Kwani kila msafiri, huusifu mzigowe

 

Itakuwa siku njema, kilazwa pema peponi

Uupokee uzima, kwa rehema za Dayani

Sauti tazidi vuma, kwa kazizo duniani

Innalillahi! Najua, sote hapa twaondoka

Kelvin Kombo Motuka

Malenga wa Vilimani

Nyamataro.

 

LAZWA PEMA WALIBORA 

Wema wako twaujua, ucheshi pia ujuzi

Lako jina twatambua, kwenye lugha we kurunzi

Kifo nacho kimebagua, cha chukua wenye ulinzi

We kawa mwandishi bora, lazwa pema Walibora

 

Siku chache zimepita, sura yako tulikosa

Hofu nayo tukapata, usingizi tulikosa

Ndani ndani tukajuta, moyoni tukatutusa

We kawa kiongo bora, lazwa pema Walibora

 

Asubuhi kaamka, hewani kuna huzuni

Waswahili tukamaka, ni lipi latokeani?

Ndani yetu kawa shaka, na ikazidi moyoni

Wewe kawa taa bora, lazwa pema Walibora

 

Habari katufikia, kuwa kifo mekunasa

Chozi katiririkia, hili jambo katutesa

Huzunini mebakia, kikumbuka hiki kisa

We kawa mwalimu bora, lazwa pema Walibora

 

Vitabu twavikumbuka, ‘Siku Njema’ kawa bora

‘Mbaya Wetu’ uliandika, ‘Waja Leo’ ukachora

‘Sina Zaidi ‘ kashika,’ Kidagaa ‘ pia ni bora

Kiswahili metikiswa, Fasihi metingika

 

Kwa heri tunasema, kwa uchungu tunanena

Na usafiri kwa neema, twaombea Maulana

Akulaze pale pema, mahali penye wanana

Walibora umehama, mioyoni ni mahame

MALENGA MWENYE MALENGO

S. M KIAMA

 

Tunawaza kuwazua,  majibu kitendawili

Donda hili tunalia,   uchungu watukabili

Ameenda kwa Jalia,  Walibora wetu nguli

Walibora metuacha,  siku njema kawa mbaya

 

Ilianza kiuvumi,  kumbe kweli uliaga

Metawala kwenye ndimi,  mambo hayaendi shega

Kifo chako si uvumi,   metulazimu kukoga

Walibora metuacha,  siku Njema kawa mbaya

 

Kwetu sisi mashabiki,  wa Lugha ya kiswahili

Kimeshaoza ni dhiki,   Hali Tena sio Hali

Kifo hiki mamuluki,   kutunyang’anya jabali

Walibora metuacha,  siku njema kawa mbaya

 

Masikini babu yangu, kalale pema peponi

Kifo kakuweka pingu,  yatubidi kuamini

Kote katanda ukungu,  hatuoni Ni huzuni

Walibora metuacha,  siku njema kawa mbaya

 

Ndoto zile Marekani,  tazikumbuka hakika

Lipokuwa duniani,  tungo zako litushika

Katuchochea ndotoni,  wengi wetu twaandika

Walibora metuacha,  siku njema kawa mbaya

 

Kazi zako za fasihi,  hata Sasa zinadumu

Vizazi vitaziwahi,   kuyapata ya muhimu

Kayatunga kisahihi, nguvu yako kwa kalamu

Walibora metuacha,  siku njema kawa mbaya

 

Ukingoni samahani,  Mola wetu Baba Mungu

Pokea Bora jamani,   atawale nawe mbingu

Muondoe matatani,   huyo Ni swahiba wangu

Walibora metuacha,  siku njema kawa mbaya

Isaac Nyaribari

 

Duru zilofika kwetu, zimetutwiza huzuni

Fundo kama mrututu, metusakama moyoni

Sisahau kamwe katu,  zako safi hamkani

Kweli mebabatuliwa, Bae bae Walibora

 

Lisilo budi hubidi,  kwayo chonda takuaga

Kifo nguvu mekuzidi, kwa mafutu mekubwaga

Ila kwetu ni khalidi,  nasahako tutaiga

Kweli mebabatuliwa, Bae bae Walibora

 

Siku njema mewa baya, sio tulivyozoea

Mekatika zetu nyaya,  akili metulegea

Waswahili tumegwaya,  dagaa metuozea

Kweli mebabatuliwa, Bae bae Walibora

 

Siamini  walaula,  eti Kweli metutoka

Ngewa ndoto falaula,  ka ndoto ya Amérika

Nitatuma zangu sala,   peponi kukubalika

Kweli mebabatuliwa, Bae bae Walibora

 

Laiti  tungejuapo,  wafikia yako ncha

Tupate la mwisho kopo, kabla siku yako kucha

Tule pamoja kiapo,  kiswahili kutoacha

Kweli mebabatuliwa, Bae bae Walibora

 

Kazi zako za sanaa,  litunga kwa uchapasi

Kaamini kila saa,   fasihi hutaanisi

Damuni hutochakaa, ingawapo ni nyeusi

Kweli mebabatuliwa, Bae bae Walibora

 

Ujinga katuondowa,  tuzidi kukakawana

Kiswahili kitakuwa,  kwetu kufa kuzikana

Tu jambo wa kibarawa, lakini tutang’ang’ana

Kweli mebabatuliwa, Bae bae Walibora

 

Mafunzo ulotutia,  kwetu ni hazina bora

Mshawasha litutia,  gwiji wetu walibora

Nasi tutakuchangia, Uvishwe taji akhera

Kweli mebabatuliwa, Bae bae Walibora

 

Sina mengi kunenani,  nakomesha unenaji

Kheri tele safarini,  ufikie huo mji

Mahali pema peponi, roho pate ‘tuliaji

Kweli mebabatuliwa, Bae bae Walibora

Malenga: Shenvah .D. Mutugi

Chuo Kikuu chá Chuka

 

LALA SALAMA GURU

Wangu moyo meatuka,habari za kushitusha

Michirizi sokauka, uso wangu melowesha,

Walibora meitika, kifo kamnyamazisha,

Buriani Walibora, lala ulale salama.

 

Michango humu nchini,kisanaa tena sana,

Sautiyo redioni, lizindua wengi Sana,

Stadi uandishini, kifo hapa umechuna,

Buriani Walibora, lala ulale salama.

 

Shupavu na runingani,aling’aa kwa haiba,

Uhariri gazetini, hata katika katiba,

Tulijua mioyoni,tungekijaza kibaba,

Buriani Walibora, lala ulale salama.

 

Konde kifo metufuma,kifasihi megusika,

Riwaya zote livuma,hisia zetu lishika,

Buheri mwenye uzima, na ajali kakufika,

Buriani Walibora,lala ulale salama.

 

Kwa vyote nilivyosoma,ulikuwa la waridi,

Maadili yalivuma, riwayazo karadidi,

Melala bila huruma, kifo hakibishi hodi,

Buriani Walibora,lala ulale salama.

 

Profesa tunalia,ila merudia mola,

Usingizi wa udhia,na milele umelala,

Duniani twapitia,akuonee fadhila,

Buriani Walibora,lala ulale salama.

 

Mungu uso dosari,guru wetu mpokie,

Muonee na fahari,palo pema mlazie,

Keni wetu ni kwaheri,maovu akuepushie,

Buriani Walibora,lala ulale salama.

Mwalimu Jack Ogonda

Mjukuu wa Seremala’

Bungoma

 

*BURIANI  MTOTO WA MWALIMU*

Tumeshikwa na kimako,

Wa pwani hata wa bara,

Kwa habari za mauko,

Yake *ken Walibora*

Pigo kubwa lililoko,

Kweli kubwa hasara.

Mtoto wake mwalimu, jamani tutakukosa.

Jamani tutakukosa,

Sanaani kwa hakika,

Uandishi lijitosa,

Lugha ikaimarika,

Kurasa kwa ukurasa,

busara uliandika,

Mtoto wake mwalimu, hayafi uloandika.

Hayafi uloandika,

Kila mja atasoma,

Kwa kweli umesifika,

Kuandika *siku njema*

Mioyo umetuteka,

Kwayo *sauti ya mama*

Mtoto wake mwalimu, hakika takukumbuka.

Hakika takukumbuka,

Runingani kwa yakini

Taarifa  lisisika,

Ukisoma kwa makini,

Kila mja ulimteka,

Kwa sautiyo laini,

Mtoto wake mwalimu, pengo lako ni dhahiri

Pengo lako ni dhahiri,

Kwa sekita ya elimu,

Hasa kwa ushairi,

Kweli ulitia hamu,

Utunzi ulo mahiri,

Kaendesha gurudumu.

Mtoto wake mwalimu, buriani buriani .

Buriani buriani,

Karima  takuongoza.

Kwaheri duniani,

Japo ni ngumu kumeza

Twasononeka moyoni,

*kidagaa kimeoza*

Mtoto wake mwalimu,  siamini  metutoka.

Siamini metutoka,

Machoni bila kwaheri

Ila mtimani fika,

Utabaki kuwa heri,

Paradiso ukifika

Ufurahi Pasi Shari

Mtoto wake mwalimu, kifo hakina huruma.

IRENE OILEPO

Shule ya DEB

Loitokitok

 

HAJAFA WALIBORA

Habari kaamkia,butwa ni wengi kapiga

Siku njema kakwamia,maneno kazidi kunoga

Ni habari za tanzia,mwenzetu katuaga

Buriani Walibora ,rohoni mwetu naishi.

 

Kidagaa kimeoza,kwa haya yaliozuka

Ni hili naloliwaza,fasihi livyoumbuka

Limebaki kunikwaza,wingu lilotufunika

Buriani Walibora,rohoni mwetu naishi

 

Riwaya lizoandika,tamthilia na kadhalika

Kotekote mesifika,hata kule Amerika

Gwiji uliyesikika,tutaishi kukumbuka

Buriani Walibora,rohoni mwetu naishi

 

Waswahili tulobaki ,sife moyo asilani

Tuchapeni kazi kiki,hata kwetu machumbani

Nimebaki kusadiki,kwamba sote tu njiani

Buriani Walibora,rohoni mwetu naishi.

 

Jamani halikubisha,sawia na la korona

Majanga haya yafisha,kucha yabadilishana

Serikali mechapisha,na usafi twamenyana

Buriani Walibora,rohoni mwetu naishi.

 

Yapo mengi ya kusema,muda kisogo menipa

Naomba kuweka koma,langu deni nimelipa

Na anavyosema mama,maisha Mungu metupa

Buriani Walibora,rohoni mwetu naishi.

Utunzi wa Oganda Mose Kevin

Malenga wa Nyikani

Mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

 

BURIANI KEN WALIBORA

Huzuni imetufika, kusikia umeaga

Ulimwengu ‘ nasifika, kwa mazuri ya kuiga

‘Meendeleza Afrika, kwa fasihi ya kuiga

Buriani Walibora, lala pema peponi

 

Kifo hakina huruma, kwa kutupokonya Keni

Kweli maisha mshuma, usokesha asilani

Tumebaki mayatima, kwa baba kutuacheni

Buriani Walibora, lala pema peponi

 

Ulikuza Kiswahili, Afrika na hata Ulaya

Tutumie Kiswahili, kwetu ulituambiya

Daima tukakubali, ‘tazidi kukitumiya

Buriani Walibora, lala pema peponi

 

Pengo kubwa limeachwa, ni nani ataliziba?

Makali akuna kichwa, ajua ni ‘ye ataziba

Hakuna cha kufichwa, ana ‘wezo wa kuziba

Buriani Walibora, lala pema peponi

 

Vitabu uliandika, tusome tuelimike

Riwaya za kusifika, vile ndoto ya Amerike

Siku njema ikifika, nasi peponi tufike

Buriani Walibora, lala pema peponi

Shaabash!! …. Biketi Emmanuel

 

MTI MKUU UMEGWA

Mengi machozi usoni, katu hatuachi kulia

Nyingi huzuni moyoni, tanzia metufikia

Metuacha duniani, pweke tunajisikia

Mti mkuu umegwa, safiri salama Keni.

 

Mauti yalipofika, nilidhani kama ndoto

NDOTO yako AMERIKA, Lienea kama moto

Nyikani kavu ukawaka, ukavuka hata mito

Mti mkuu umegwa, safiri salama Keni.

 

Ziliganda mishipani, zetu DAMU NYEUSI

Kaenda mbio mwilini, motemote kwa matiti

Takupeza namba wani, waziwazi weye mti

Mti mkuu umegwa, safiri  salama Keni.

 

SAUTI YANGU MAMA, Linitia wasiwasi

‘’Duniani amehama, si NDOTO YA ALIMASI’’

Nitakuenzi daima, kusahau si rahisi

Mti mkuu umegwa, safiri salama Keni.

 

Wengi wakwita jagina, miye nakuita nguli

Namshukuru Rabana, kwa yako nzuri amali

Fasihi yako kwa inna, ilinifaa kwa hali

Mti mkuu umegwa, safiri salama Keni.

 

Lala pema Walibora , na akutunze Karima

Sana ulitia fora, kote barani ulivuma

Ulipika ‘ wali bora’ , hususani SIKU NJEMA

Mti mkuu umegwa, safiri salama Keni.

 

Mauti metupokonya, kigogo alotufaa

Kwa nini hukutuonya, ngetuacha Ijumaa?

Tumebaki tukisonya, metufika nyingi dhaa

Mti mkuu umegwa, safiri salama Keni.

 

KIDAGAA NIOZEA, ila namwomba Manani

Dua nikikuombea, ulale pema peponi

Tamati nitakomea, japo mawazo akilini

Mti mkuu umegwa, safiri salama Keni.

Kim  Mkonokono

Nakuru

 

Kutwa hivi mekeshea, buriani ino nikupokeze,

Mtima kiwa mzito, machozi njia mbili,

Kikuwaza ewe galacha,winoni na mabukuni,

Lala pema ulojiendea,akupokee na Rabana.

 

Kwa  manenoye nakusifia, ulotunga ungali hai,

“Kinywa chako mwenyewe, kisikusifu Fulani,

Ni kheri sifa upawe,na wengine duniani,

Sifa nyingi upaliwe,  zijae hadi pomoni,

 

Lala pema ulojiendea, akupokee peponi Rabana.

Nakutakia siku njema, Walibora kisafiria mauti

Meishi nasi vema,kiswahili kakivika suti,

Chanda kino chema,mbona watupokoya mauti,

 

Lala pema ulojiendea, akupokee peponi Rabana.

Kwa  tungo tutakusifia, ewe mwandishi mlezi,

Metuacha na tanzia, Kiswahili chalilia mlezi

Sifa zako hazitafifia,daima sisi tutakuenzi,

 

Lala pema ulojiendea, akupokee peponi Rabana.

Mti  mkuu umekigwa,wa  nyuni tunayumba,

Ila haliwezi pingwa,liamualwo maulana,

Lala pema ulojiendea, akupokee peponi Rabana

 

Kingoni ndipo kaditama,shairi  ino  sanda

Ya kusitiri mweledi, Ken Waliula Walibora

Mpokee ewe Mteheremezi, hadi tena  tapoonana

Lala pema ulojiendea, akupokee peponi Rabana.

Erick Kitheka (Malenga mbichi)

 

SALAMA WALIAULA

Umetoweka mhimili, wa’ndishi twataabika

Twasononeka kwa hili, baba yetu kaondoka

Ameng’atwa na ajali, maisha yakakatika

Kuno kustahimili, jamani ninaponzeka

 

Lala salama mwalimu, kwa dhati tunakupenda

Umetujaza fahamu, makini yametuganda

Fasihi twaiheshimu, tutazidi kuiponda

Nenda salama mwalimu, mbegu umeshaipanda

 HUSSEIN M KASSIM

BURIANI MTAJIKA KEN

 

Habari kishapokea, haupo tena profesa

Huzuni ‘metuletea, ni bayana takukosa

Kiswahili ‘metetea, hadhiye kupanda hasa

Kwa mema takukumbuka, ulale pema peponi

 

Hadithi ‘metutungia, mashairi yapo pia

Nyimbo ukatughania, mafumbo ‘katutungia

Wasomi wakusifia, dunia yakulilia

Kwa mema takukumbuka, ulale pema peponi

 

Twakumbuka siku njema, tungo uliyoisuka

Damu nyeusi tazama, peupe mengi kaweka

Japo taa imezima, mwanga wako unawaka

Kwa mema takukumbuka, ulale pema peponi

 

Kidagaa vile vile, kumbe kingetuozea!

Kilisomwa kwenye shule, ubunifu kachochea

Ulipika mengi tule, ghafla umetwondokea

Kwa mema takukumbuka, ulale pema peponi

 

Kabuni ya Almasi, na ya Amerika pia

Ndoto za mja mweusi, upeo kuufikia

Ukakanya yalo hasi, ila chanya kusifia

Kwa mema takukumbuka, ulale pema peponi

 

Naisikia sauti, ya mama niienziyo

Kajitolea kwa dhati, kutweleza maishayo

Umegwa mkuu mti, ‘lia budi hatunayo

Kwa mema takukumbuka, ulale pema peponi

 

Wingu kuu limetanda, machozi yatudondoka

Galacha tulikupenda, molani akakutaka

Hatunalo la kutenda, huna budi kuondoka

Kwa mema takukumbuka, ulale pema peponi

 

Kalamu chini natia, maneno ‘meniishiya

Shairi ‘mekutungia, wa nane namaliziya

Sifa nakumiminia, kwayo ulotufanyiya

Kwa mema takukumbuka, ulale pema peponi

Emmanuel Kenga 

 

BURIANI WALIBORA

Wingu jeusi latanda,mwangaza wetu  lakata

Hofu tele yatupanda,’sanifu roho kakata

Tapatapi wakulinda,lugha safi ya kuvuta

Utu bora ulilinda,Walibora we kwaheri

 

Siku Njema twaingoja,loahidi siku moja

Imani nayo si hoja,amani twala kimoja

Damu nyeusi  vioja,tawatupa wewe ngoja

Walibora watugura,msanifu wayo kombo

 

Mgomba changaraweni,haupandwi ukaota

Je mwilio kaburini, misemo utasokota?

Ndoto zetu marekani,ni vipi zitajikita?

Kaumbuka Kongowea,makinda sisi twayumba

 

Kimeingia mchanga,kitumbua chenye ladha

Riwayaze kazipanga,zinashinda hata fedha

Tamthilia kazitunga,zang’aa pasi bugudha

Tawasifu kaitunga,kwaheri nyota Walibora

 

Aushini cha kudumu, mabadiliko kamaka

Kifoni hautadumu,maisha mapya utapaka

Kiswahili lugha tamu, twakusifia ‘we Kaka

Waliaula we bakora,tumeporwa Walibora

Denis Waswa Barasa

 

MOLA AMLAZE PEMA

Imelia parapanda,ya kiama imetimu

Mbinguni amepanda,ametuaga mwalimu

Zahuzunisha kaida,nyoyoni zatuhujumu

Mola amlaze pema,Profesa Waliaula.

 

Nazileta rambirambi, kwa ndugu na marafiki

Naleta piya maombi, rahimu awabariki

Poleni kwayo mawimbi,wanalugha na ashiki

Mola amlaze pema,Profesa Waliaula.

 

Mwalimu mchapakazi, Purofesa msifika

‘Staarabu mkufunzi,kila kona lotukuka

Mcha mungu waziwazi, mwadilifu naandika

Mola amlaze pema,Profesa Waliaula.

 

Galacha wetu mzazi, heri tunamtakia

Apawe mema makazi, na mola wetu jalia

Kusahau hatuwezi, mema al’otufanyia

Mola amlaze pema, Profesa Waliaula.

 

Wasomi amewafaa,makali aliwatia

Al’ofunza wanang’aa,hekima liwaghawia

Ametuacha shujaa, waswahili tunalia

Mola amlaze pema, Profesa Waliaula.

Felix Gatumo

 Malenga Mtamu

Igandene, Meru

 

*BURIANI WALIBORA*

Habari mtandaoni,zatamba ulimwenguni,

Na bado hatuamini,yani tuko mataani,

Ajali barabarani,mekutoa duniani,

Buriani Walibora,ulale mahali pema.

 

Umesifika shuleni,na hata pia vyuoni,

Siyo tuu humu nchini,hata kule Marekani,

Vitabu umeandikani,vyasomwa ‘te duniani,

Buriani Walibora,ulale mahali pema.

 

Ulizama riwayani,hadithi ukatupani,

Hi ndoto ya Marekani,Siku Njema mlangoni,

Nayo Tuzo hadithini,Mbaya Wetu mchezoni,

Buriani Walibora,ulale mahali pema.

 

Utabaki mawazoni,na hata mwetu moyoni,

Ulowaacha nyumbani,tawaweka maombini,

Nasi tuko safarini,tutakutana peponi,

Buriani Walibora,ulale mahali pema.

     Mtunzi: Samuel Jomo.

    Mwalimu: Kisoko Girls, Nambale.

   Kutoka: Lugari,Kaunti ya Kakamega.

 

SIKU NJEMA IMEENDA

Mwanzo nashika kalamu, kalamu hino ya babu,

Kisha niwape salamu, salamu zenye ajabu,

Hizi hazina utamu, utamu huku dhurubu,

Jamani siku si njema, imeenda na mwenyewe,

 

Amekuwa marehemu, marehemu tena bubu,

Alokuwa na fahamu, fahamu bila taabu,

Kwa yake nyingi elimu, elimu iso aibu,

Jamani siku si njema, imeenda na mwenyewe,

 

Siku njema nafahamu, nafahamu ni sababu,

Yake yeye kuwa bomu, bomu ingawa tabibu,

Alibuni bila simu, simu ilikuwa tabu,

Jamani siku si njema, imeenda na mwenyewe,

 

Kweli chema hakidumu, hakidumu ni dhahabu,

Chaweza tiliwa sumu, sumu usoweza tibu,

Kisha kikawa ni pumu, pumu ndwele ya kusibu,

Jamani siku si njema, imeenda na mwenyewe,

 

Mwisho nashika kalamu, kalamu  yenye ajabu,

Niiombe ihukumu, ihukumu wa majibu,

Wajuao kutuhumu, kutuhumu kwa aibu,

Jamani siku si njema, imeenda na mwenyewe.

©IDDI NICK…

Mwendawazimu Timamu

 

UNGALIJUA MAPEMA

Mwandani umeondoka, kwa mababu umeenda,

Sifa zako za hakika, pia nazo zimeenda,

Na jina lako tajika, kulitaja nimependa,

Ungalijua mapema, ungeghairi ziraili,

 

Tumehaha kwa hakika, mili yetu imekonda,

Chepesi hata kushika, mikono imeshaganda,

Kuimba pia twachoka, sauti zimeshaenda,

Ungalijua mapema, ungeghairi ziraili,

 

Ona tunavyoteseka, hatuna mlo makinda,

Bongo zimeweweseka, kama njia zimepinda,

Jamani tuna mashaka, na baraste ni migunda,

Ungalijua mapema, ungeghairi ziraili,

 

Nauliza sitachoka, mbona babu ukaenda?

Au ulishaudhika, na shida za hii kanda?

Ama kweli ulifika, upeo wa kutupenda?

Ungalijua mapema, ungeghairi ziraili,

 

Ningeweza kukutamka, na mauti yakatenda,

Ningesuta bila shaka, nyendo zake za kuwinda,

Nayo ingelalamika, na mwishowe kukulinda,

Ungejua mapema, ungeghairi ziraili,

 

Washairi wachomeka, kimeanguka kibanda,

Angalia wazunguka, kama nzi kwa kidonda,

Hawana la kupachika, kuta wingu limetanda,

Ungejua mapema, ungeghairi ziraili,

 

Tamati nasononeka, Mwendazimu wa kuranda,

Nalo tone natoneka, nikiilamu sanda,

Haidhuru ‘mefanyika, na Mwenyezi ametenda,

Ungejua mapema, ungeghairi ziraili

©IDDI NICK…

Mwendawazimu Timamu

 

KINA CHA FIKIRA

Ndugu Ken Walibora, ametuachia pango

Tena pango la hasara, lisofidiwa mpango

Kile Kina Cha Fikira, nani ataziba pengo?

Walahi Taifa Leo, hicho Kina Cha Fikira!

 

Nnahisi ufukara, akili yajaa dongo

Kuondoka Walibora, lugha yanuka usungo

Haing’ari ingang’ara, ikaujenga mjengo

Walahi Taifa Leo, hicho Kina Cha Fikira!

 

Kijarida kilong’ara, Cha lugha yenye mgongo

Na ilimu ilo bora, ilonakishiwa mwango

Sasa inajipa kura, iwe heri au fyongo

Walahi Taifa Leo, hicho Kina Cha Fikira!

 

Ni uzee wa busara, ndio wanipa ukongo

Kwani Ken Walibora, alikuwa kwangu gongo

Hachezesha kimpira, lugha isingie chongo

Walahi Taifa Leo, hicho Kina Cha Fikira!

LUDOVICK MBOGHOLI

AL – USTADH – LUQMAN

NGARIBA MLUMBI (WAKITA TTC 006)

 

BURIANI WALIBORA

Mniacheni nilie, nimeshindwa stahimili

Ni wapi nikimbilie, hili kwangu pigo kali

Hebu mnisimulie, mmemfanyani Wali?

Buriani buriani, Buriani Walibora

 

Wamemgonga kwa gari, kisha wakalikimbiza

Mja asiye hatari, wema aloutangaza

Naumia sio siri, maumivu nauguza

Buriani buriani, Buriani Walibora

 

Nambieni nambieni, achaneni kunyamaza

Kulikoni kulikoni, Walii mkammeza

Mbona iwe ye jamani, aso kisasi lipiza

Buriani buriani, Buriani Walibora

 

Nimeumia moyoni, pengo kubwa pengo hili

limekwenda tumaini, nguzo yake Kiswahili

Si ntumbani duniani, kifo hiki ni katili

Buriani buriani, Buriani Walibora

                  Gilbert Kinara

                   “Tabibu Mshairi”

                   Keumbu, Kisii, Kenya

 

SAFIRI SALAMA WALIBORA!

Kifo mbona huna sura,tukujue kwa mapema,

Wavizia kila mara, Kuiba bila huruma,

Kibeba walo imara, sisaze hata karama,

Gwiji safiri salama,tuko nyuma WALIBORA.

 

Kwa majonzi twaparara, tukaikosa salama,

Tukavikuna vipara, Quliza mbona mapema,

Dunia umeigura, tena kitendwa dhuluma,

Gwiji safiri salama,tuko nyuma WALIBORA.

 

Toka kwako WALIBORA, utatudumu daima,

Utunzi wenye busara,na mafunzo ya gharama,

Yalokufanya kung’ara, miongoni mwetu umma,

Gwiji safiri salama,tuko nyuma WALIBORA.

 

We ndiwe mfano bora, wa vitabu kuvisoma,

Profesa uso kera, bukuni ulo jituma,

Na kweneza njema sera,waja’si tuje kuchuma,

Gwiji safiri salama,tuko nyuma WALIBORA.

 

Ushujaa WALIBORA,kwangu mimi naungama,

Uloniasa kuchora, Kiswahili lugha njema,

Na mashairi Kapera, tatunga hadi kiama,

Gwiji safiri salama,tuko nyuma WALIBORA.

 

Lala pasipo wakora, peponi lipo Karima,

Utu wako uwe kura, itokutunuku wema,

Usiwe wa kuzurura, jahimu kuso rehema,

Gwiji safiri salama,tuko nyuma WALIBORA.

 

Tamati napopapura,tuko nyuma WALIBORA,

Kuishi ni kwa kudura, na yake Mola neema,

Kwake hakuna hasara, vuno lake akichuma,

Gwiji safiri salama,tuko nyuma WALIBORA.

Malenga Kilimani,

“Sauti Za Makiwa”

 

BURIANI WALIBORA

Buriani naitoa, Kwa simanzi teletele,

Kwa ujumbe ulozoa, hisia za kwangu tele,

Ama meliacha doa, katika Lugha teule,

Buriani Walibora, peponi ulale pema.

 

Ujumbe niliupata, Kwa Kalamu ya Galana,

Nikakataa kata, kua hili si bayana,

Ukweli nimeupata, meamini muungwana ,

Buriani Walibora, peponi ulale pema

 

Kiswahili mekikuzi, Afrika na kwingine,

Mebishana na wapuzi, wenye midomo minene,

Lugha sasa ni pendezi, apingae nimuone,

Buriani Walibora, peponi ulale pema.

 

Hadithi uliziunda, zilobora zikavuma,

Siku njema iliwanda, sitachoka kuisema,

Kiswahili ulipenda, Kwa  juhudi na heshima,

Buriani Walibora, peponi ulale pema

 

Nimeshindwa wamalanga , utunzi kuendeleza,

Linaniliza Janga, nikijaribu kuwaza,

Ila Mola lie panga, ana lengo  liso kwaza,

Buriani Walibora, peponi ulale pema.

MTUNZI

MALENGA WA MALANGA

 

Msamehe Walibora

Imefika fazaiko, katika taifa zima

Moyoni Ni masumboko, na furaha imezima,

Kiswahili ghadhabiko, HAKUNA wakuungama

Yaillah ya manani, msamehe Walibora,

 

Kiswahili amejenga, fasihi nazo sarufi,

Riwaya za kutujenga, nyingi Tena si hafufi,

Chipukizi tutatanga, light kwetu Ni ya futi,

Yaillah ya manani, msamehe walibora,

 

Riwaya zilizobora, siku njema kidagaa

Ken wetu Walibora, metuachia balaa,

Maneno ya kusorora, ndio yametapakaa,

Yaillah ya manani, Msamehe walibora

 

Metuachia simanzi, sisi wanafunzi wake,

Tutapeza zake enzi, Ni tamu na lugha yake,

Mwili umekufa ganzi, kusikia kifo chake,

Yaillah ya manani, msamehe walibora,

 

Walibora nampenza, utunzi na wahusika,

Selemani wa mapunda, ubunifu wa hakika,

Lugha take isopinda, hakika nasikitika,

Yaillah ya manani, msamehe walibora,

 

Huzuni imeshatanda, kila aliyemtunzi

Walibora hakuganda, kutupa na utatuzi,

Tutazitazama Kanda, kumkumbuka muenzi

Yaillah ya manani, msamehe walibora

 

Watunzi tujikazeni, dua njema tuombeni

Huzuni iko nchini, kiswahili dumisheni,

Alikipenda ye Ken, mfano si tuigeni

Yaillah ya manani, msamehe walibora

 

Hata tukalia Sana, Walibora hatorudi,

Tuombe si Maulana, majonzi hiki kipindi,

Tubaki tukikazana, tupate nao ushindi,

Yaillah ya manani, msamehe walibora

 

Tamati weka kikomo,  tanzia nyingi Sana,

Tuombe mumo kwa mumo, hakika yatamfana,

Ametupa msukumo, Ni ukweli si hiyana

Yaillah ya manani, msamehe walibora

Mtunzi:Sadi Swaleh S2

Lakabu:MWAMBA IMARA

Mombasa Likoni

 

WALIBORA WALIAULA!

Dunia ya Kiswahili, leo imepigwa nyundo,

Nyundo yake ziraili, kinasikika kishindo,

Kwamba ilivyo katili, kutia kwenye mkondo,

Umeenda Walibora, salimia Marijan!

 

Walibora ni wa ngapi, mwanalugha kuondoka,

Kwenye kipindi kifupi, pasipo kupumzika,

Unawapeleka wapi, kifo usiyetosheka,

Umeenda Walibora, salimia Nabhany!

 

Waandishi wa vitabu, wa kupigigwa mifano,

Mauti yamewasibu, leo twashika viuno,

Vya wanafunzi vilabu, kusoma vyauma meno,

Umeenda Walibora, salimu Malimu Mbega!

 

Hii ni damu nyeusi, kumaliza siku njema,

Na tena kwa wasiwasi, funga kazi kwa kuhema,

Kidagaa ni masisi, kimeoza kwa huruma,

Umeenda Walibora, salimu Ali Shamnte!

 

Lala mwana wa Mwalimu, wa ndoto ya Amerika,

Funzo lako litadumu, ni mwiko ulovunjika,

Kupasuka gudurumu, injini hikudhurika,

Umeenda Walibora, salimia Mazirui!

 

Kwamba yamefikwa taji, ni njia ya kuendea,

Enenda mtangazaji, jiunge na mashujaa,

Mapya kwa watazamaji, yakuhusu twaduwaa,

Umeenda Walibora, peponi kutangulia.

 

Ken mla wali bora, wali bora hatoula,

Si wa pwani si wa bara, alipo si wa chakula,

Mashairi yake bora, yameenda na makala,

Umeenda Walibora, salama lala shujaa.

 

Nane kufuli natia, makiwani familia,

Harudi tungamlia, kurasa ameachia,

Ngapi zetu kasalia, siri ya Mola Jalia,

Umeenda Walibora, laleni mpiganaji!

“Malenga wa migombani”

Nyagemi Nyamwaro Mabuka.

Migomba ya Ziwa Kuu.

 

BURIANI WALIBORA

Profesa umeenda, *W* alibora metuacha,

*B* uka imeshatutanda, *A* mana imeshachacha,

*U* meenda kwa kupinda, *L* iamba yako mekucha,

*R* abana mweke Rahani, *I* mpate pumziko.

*I* natuuma mioyo, *B* urudani imetuwa,

*A* lekuwa msi choyo, *O* neni sasa katwawa,

*N* a twabaki amba ndiyo, *R* aufu kamchukuwa,

*I* tunzwe na roho yake, *A* ngali huko peponi.

 *MWANGA MSARIFU* 

 

BINGWA

Nakumbuka zama zile,’liponiamsha mama,

Mapema za siku zile,kwenda ng’ombe kumkama,

Sikupata kero vile,radio niligandama,

Kusikiliza habari, kutoka kwa Walibora.

 

Tangazo lake hakika,lilivuta wengi waja,

Hakupatwa na wahaka,’lipotangazia waja,

Sautiyo siyo shaka,’liyojaza nyingi hoja,

Walibora Mja bora,si bora mtangazaji.

 

Tulipenda kumuiga,mimi na kakangu Mwala,

Lipolonga tuliiga,”Mimi ni Waliaula.”

Hatukuwa na uoga,tulisema kwa ufala,

Kimetuozea hakika,kidagaa kimeoza!

 

Sekondari nipofika,hasa kidato cha tatu,

Kiswahili ‘lisifika,hata katika matatu,

Tulihisi tumefika,kusoma tulithubutu,

Fasihi lipata mwanga,kupata mwandishi bora.

 

Bingwa aliyeandika,riwaya ya SIKU NJEMA,

Kuwapanga wahusika,wabaya na wale wema,

Riwaya ilisifika,kwa mafundisho ya wema,

Kongowea mhusika, hakika alipendeka.

 

Hatutasahau pia,kitabu chake murua,

Riwaya ya KIDAGAA,wengi kiliwaozea,

Hasa wale wa balaa;Mtemi na Kambonaa,

Utunzi wenye ujuzi,hakika tutaupeza.

 

Kwa sasa nina mawazo,moyoni nina huzuni,

Sina hata na uwezo, wa kupata tumaini,

Tutapataje tulizo,na shujaa yu kifoni?

Hakika tumeozewa!kidagaa kesha oza!

 

Ni bingwa aliyependa,lugha yetu Kiswahili,

Lilonifanya kupenda,pia nami Kiswahili,

Kuwa ticha nikapenda,kufundisha Kiswahili,

Mfanowe wa kuigwa,na wa kizazi cha kesho.

 

Namaliza nikisema, asante kwa kuandika,

Nilimaliza kusoma,na piya kumakinika,

Hata kama inauma,bado tutakukumbuka,

Safiri salama bingwa,kwa Pahala palo wema!!

Malenga:Mwalimu Nancy Chebet Mibei,

 Shule ya upili ya Our Lady Of Glory Kaptagat Girls. 

 

TUONANE SIKU NJEMA!

Zahuzunisha habari, za simanzi alfajiri,

Amekwenda kwa Kahari, mwandishi mashuhuri,

Nikivuta tafakuri, naingiwa na ghururi,

Kalale mahali pema, tuonane siku njema!

 

Kenda zake kwa hakimu, kweli chema hakidumu,

Yaomboleza kaumu,  wote tulomfahamu,

Wa Lamu hadi Kisumu, wanafunzi kwa walimu,

Kalale mahali pema, tuonane siku njema!

 

Hadithi zako murua, tungo za kusisimua,

Tunakuombea dua, uabiripo mashua,

Leo jua limetua, mekwenda tusikojua,

Kalale mahali pema, tuonane siku njema!

 

Makiwa familia, amekwenda kwa Jalia,,

Marafiki wanalia, tumeshindwa vumilia,

Parapanda tapolia, ndipo roho tatulia,

Kalale mahali pema, tuonane siku njema!

 

Umetoka duniani, umetutoka machoni,

Ila mwetu fikirani, utadumu aushini,

Mekuweka mtimani, Walibora buriani,

Kalale mahali pema, tuonane siku njema!

 

Metuacha na majonzi, ewe wetu mkufunzi,

Kwa wengi tulokuenzi, imezimika kurunzi,

Waandishi na watunzi, walimu na wanafunzi,

Kalale mahali pema, tuonane siku njema!

© Bismark Bin Kimanga

“Malenga Muadilifu”

Rongai Nakuru.

 

BURIANI PROFESA KEN WALIBORA

Laiti tungalijua

Tungalimsihi sikunyakue

Jamani profesa wetu

Wa fasihi na Kiswahili jumla

Profesa Ken Walibora

Ingekuwa Bora usingetuwacha

Nilidhani ilikuwa ndoto

Na SI ndoto ya Amerika

Labda Ni zaidi yake Amerika

Najuta zaidi ya kujuta

Imekuwa SI ndoto Tena

Imekuwa SI siku Njema Tena

Laiti ningalijua

Ningalikuandikia mapema

Sahiba wa kufa kuzikana

Ingawa hatukupatana

Mahuluki na ndwele wanamenyana

Imekuwa Ni kufa na kuzikana

Nilidhani siku Moja takupata

Univukishe mipaka

Mipaka ya uandishi

Malenga Chipukizi ninalia

Kidagaa kimeniozea

Chozi limegeuka damu nyeusi

Waswahili tumejitia ububu

Kusema labda tujaribu

Tufafanulie babu

Tena kwa utaratibu

Dhamirake “Nizikeni Papa hapa”

Umekuwa mgumu mjarabu

SI hadithi fupi

SI riwaya

SI mashairi

SI uanahabari

SI makongamano

SI makala anuwai

Twakuvisha taji shehe, mekikuza Kiswahili

Ufanisi wako shehe, dhahabu unastahili

Vipaji tunavyo shehe, kukikuza Kiswahili

Najiuza mie shehe, wanijie mwanamwali

Nanena, Dua Njema kwa Rabuka

Nanena, akuangazie wa milele mwanga

Nanena, kwa amani pumzika

Nanena, pale pale tutakuzika

Nanena, machozi hayeshi profesa

Nanena, Basi liwe kwetu Chozi la Heri.

Kama Lile la Assumpta Matei.

*KAWIRA ESTHER SUSAN*

*Malenga Chipukizi,*

*CHUO KIKUU CHA CHUKA

 

Kweli mauti huruma, hukuumbiwa hakika,

Kifo we mwenye dhuluma, umemtorosha bingwa,

Walibora kwa karima, twakuombea ufike,

Kidete tutasimama, Kiswahili kutukuza,

 

Ukandika Siku Njema, na Riwaya nyinginezo,

Darasani kasimama, nikaitwa kongoea,

Siku zote kila juma, damu nyeusi tetea,

Kidete tutasimama, kiswahili kutukuza,

 

Fasihi imesimama, kwa juhudi zako gwiji,

Tungo nzuri ukafuma, Riwaya ukaandika,

Kila siku ukazima, Kasumba za kikoloni,

Kidete tutasimama, Kiswahili kutukuza,

 

Wananyuni kutuama, mti kubwa kaanguka,

Kwa wote wanaosoma, majonzi yawatawala,

Kwa mola tutasimama, pazuri ‘kupumzishe,

Kidete tutasimama, Kiswahili kutukuza,

Mtunzi; B.w Mukele D.K 

Mwalimu,

 Shule ya Upili St Johns-Kwa Mulungu.

 

BURIANI KEN WALIBORA

1.Johari nakosa vina,hata mizani jamani

Urari pia hakuna,nabaki kutunga duni

Syamini hayupo tena,zimebaki buriani

Lala pema Walibora,ShakeSpear wa kwetu

 

2. Ulianza ja uvumi,jana na juzi jioni

Watu kawa hawasemi,fununu mitandaoni

Ya kuwa tarehe kumi,ulipotea nyumbani

Buriani Walibora,Mfalme wa fasihi

 

3.Nakumbuka kama jana, tukiongea simuni

Wazo kabadilishana, juu ya fasihi fani

Ukamba tutaonana,Corona ikiishani

Buriani Walibora, Mfalme wa fasihi

 

4.Tungo uliniahidi,nitumie kwa diwani

Shairi mbili zaidi,ukasema tanipani

Leo hauyupo badi,umetoka duniani

Buriani Walibora, Mfalme wa fasihi

 

5.Siku Njema meandika, kikatumika shuleni

Kidagaa kadhalika,ni nani asojuani

Na ndoto ya Amerika, na kipenda si utani

Buriani Walibora,Mfalme wa fasihi

 

6.Maskini Babu Yangu, Damu Nyeusi diwani

Na tamthilia chungu, zimejaa madukani

Na leo la kifo wingu,mekufunika mwandani

Buriani Walibora,Mfalme wa fasihi

 

7.Saba beti za Johari,za kusema Buriani

Naitimisha shairi, nifute chozi machoni

Metukumba kweli shari,soote ulimwenguni

Buriani Walibora,mfalme wa fasihi

Utunzi wa Ustadh Emmanuel

Johari Adimu

Malenga kutoka Akhera

 

BURIANI GURU

Katuacha WALIBORA,

Hali yetu sio bora,

Imebidi nimechora,

Wa Waraka huu bora,

Sio siku njema tena,

Hata raha mie sina,

Mbona wewe hungekana?u

Heri ungepiga kona,

La simanzi limetanda,

Kusubiri ulidinda,

Ukasema unaenda,

Takumbukwa kwenye kanda,

Duniani kawasili,

Dhamira kiwa swahili,

Guru kajaa akili,

Yanitoka kinakili,

Nakupa wa buriani,

Ya kaisha duniani,

Sisahau asilani,

Takuenzi aushini,

#malengaAmaganga

Sauti yako nyororo,

Tabasamu yako ya kunasa,

Ulitugusa wengi wetu,

Buriani ndugu Walibora.

Leo hii si siku njema,

Wengi wetu tulivyokujua,

Lugha pevu tutaikosa,

Buriani ndugu Ken.

Vipindi ulichangia,

Redioni na runingani,

Ukatukuza wengi wetu,

Buriani ndugu Waliaula.

Wanafunzi wa vyuoni,

Mashabiki wa kandanda,

Sote tutakukosa,kwa mvuto wa kipekee

Safiri salama ndugu Ken walibora.

(Ustadh Vincent Obuki)

Mwalimu mwandishi..Thika Rd.Christian School, Nairobi.

 

BURIANI WALIBORA

Mola wetu mkarimu,mwenye wingi wa rehema

Leo hii mrehemu,Walibora kwa neema

Mwandishi mtaalamu,kaileta siku njema

Buriani Walibora,nahodha wa Kiswahili

 

Walibora buriani,waziwazi isikike

Ulishika usukani,Kiswahili kisifike

Kidagaa vitabuni ,watu wote makinike

Buriani Walibora ,nahodha wa Kiswahili

 

Nizikeni papa hapa,baadhi ya kazi zako

Siku njema ukanipa,yote kwa heshima yako

Utu wako ukalipa,kaenea jina lako

Buriani Walibora,nahodha wa Kiswahili

 

Kaditama mwisho wangu,takupeza Walibora

Ninasema kwa uchungu,kwani ulikuwa bora

Unalia moyo wangu,mauti yametupora

Buriani Walibora ,nahodha wa Kiswahili.

(Kelvin Njuguna shule ya Msingi GoodShephered Nakuru)

 

MTI UMEANGUKA

Machozi yanatutoka, hatwachi katu kulia,

Mioyo yasononeka, habari metufikia,

Hakika twasikitika, waswahili tunalia,

Mti umeanguka, lala pema Walibora

 

Mauti yametufika, hivi kama tunaota,

Mlima ukaanguka, simanzi ikatupata,

Nyoyo zetu zateseka, hili sisi kutupata,

Mti umeanguka, lala pema Walibora

 

Sio peke Afrika, kotekote duniani,

Kilio kinasikika, hata kule marekani,

Jemedari metutoka, tufanye yapi yakini,

Mti umeanguka, lala pema Walibora

 

Tasnia meyumbika, na nyororo kulegea,

Weye mkuu kutoka, kileleni ‘kozoea,

Walibora pumzika, ila tulikuzoea,

Mti umeanguka, lala pema Walibora

 

Aliyapenda Rabuka,muumba na Muumbua

Mapema akakutaka, kwake upige hatua,

Hivi kwetu metutoka, ila kwake mekimbia,

Mti umeanguka, lala pema Walibora

 

Ken tutakukumbuka, amali metuachia,

Siku njema hijafika, na dagaa metwozea,

Mbona haraka hakika, mkono kutupungia?

Mti umeanguka, lala pema Walibora

 

Peponi kapumzika,kwa Mola twakuombea,

Kamsifu msifika, wewe aliyekutwaa,

Na hutasahaulika, lugha livyopigania,

Mti umeanguka, lala pema Walibora

 Shukran Malenga,

Mwalimu Salvine Obonyo 

Stahiki mkwezi 

 

Naisikia Sauti, Sauti Ni yake mama,

Farisi wetu hayati, hebu fanya himahima,

Ndoto zetu za dorati, kinywa ‘mebaki achama,

Siku Njema ‘mewadia, pumzika gwiji wetu,

 

Kumbukumbu ‘lizoacha, zitasalia moyoni,

Ndoto zetu Alinacha, Rudi Tena duniani,

Maulana nitamcha, ‘kulaze pema peponi,

Siku Njema ‘mewadia, pumzika gwiji wetu,

 

Masikini babu yangu, ‘likuthamini kwa kweli,

Kazi yako chunguchungu, tulijadili paneli,

Mtimani ‘na uchungu, kusahau muhali,

Siku Njema ‘mewadia, pumzika gwiji wetu,

 

Dagaa ‘metuozea, hangarara tumebaki,

Machoni umepotea, ajmaina mashabiki,

Kazi yako tasalia, tutabaki kusadiki,

Siku Njema ‘mewadia, pumzika gwiji wetu.

Brian Okum.

 

LAZWA  PEMA WALIBORA

Wema wako twaujua, ucheshi pia ujuzi

Lako jina twatambua, kwenye lugha we kurunzi

Kifo nacho kimebagua, cha chukua wenye ulinzi

We kawa mwandishi bora, lazwa pema Walibora

 

Siku chache zimepita, sura yako tulikosa

Hofu nayo tukapata, usingizi tulikosa

Ndani ndani tukajuta, moyoni tukatutusa

We kawa kiongo bora, lazwa pema Walibora

 

Asubuhi kaamka, hewani kuna huzuni

Waswahili tukamaka, ni lipi latokeani?

Ndani yetu kawa shaka, na ikazidi moyoni

Wewe kawa taa bora, lazwa pema Walibora

 

Habari katufikia, kuwa kifo mekunasa

Chozi katiririkia, hili jambo katutesa

Huzunini mebakia, kikumbuka hiki kisa

We kawa mwalimu bora, lazwa pema Walibora

 

Vitabu twavikumbuka, ‘Siku Njema’ kawa bora

‘Mbaya Wetu’ uliandika, ‘Waja Leo’ ukachora

‘Sina Zaidi ‘ kashika,’ Kidagaa ‘ pia ni bora

Kiswahili metikiswa, Fasihi metingika

 

Kwa heri tunasema, kwa uchungu tunanena

Na usafiri kwa neema, twaombea Maulana

Akulaze pale pema, mahali penye wanana

Walibora umehama, mioyoni ni mahame

MALENGA MWENYE MALENGO

S. M KIAMA 

 

BURIANI WALIBORA

Tulipokutana Guru,mwaka juzi Nairobi,

Hata leo nashukuru,miaka hiyo arubi,

Hapo mbeleni Nakuru,nikiwa naye kibibi,

Zawadi uliamuru,nikapewa na ya bibi.

 

Hatukuachia hapo,redio tulipatana,

Na kila nikuonapo,picha zako ni amana,

Nakikumbuka kiapo,gwiji nilipokuona,

Uliapa Kiswahili,kutetea kwa kamili.

 

Ulienda na ulaya,nyumbani ukarejea,

Ungalikuwa mbaya,mbali ungekatalia,

Gwiji hukuona haya,maelfu kuachia,

Kilichokuwa moyoni,kilikuwa Kiswahili.

 

Meza uliitandika,chakula ulipakua,

Picha umeitundika,umeigongomelea,

Kitanda kakitandika,kimebaki kulalia,

Gange umetufanyia,hatuna kijisababu.

 

Sitalia tapongeza,shughuli zako aula,

Maswali sitauliza,kwa nini Waliaula,

Nitabaki nikiwaza,yako nikikosa ila,

Itatuchukua muda,kukubalia mauti.

 

Ustadhi siamini,ni vigumu kukubali,

Umenitoka jamani,umejiendea mbali,

Walibora bin Keni,siungami miye hili,

Umeenda bila hata,siku njema kutegua.

 

Ulichora siku njema,ukapika kidagaa,

Lile pia tumbo zima,ulichotuandikia,

Kidete ulisimama,lugha hino kukokea,

Umeenda bila hata,kidagaa kukipika.

 

Kamau nilikujua,mdogo najikulia,

Riwaya ya kuanzia,ni yako nilisomea,

Motisha ukanitia,lugha nikaichukua,

Umeenda bila hata,tumbo kulitia shibe.

 

Lala pema profesa,Mola akupe amani,

Ingawa litatutesa,tumeikosa imani,

Mola hapewi makosa,akhera na duniani,

Akulaze pema Yeye,tutaonana inshalla.

 

Zimeisha kumi beti,nipige bismillahi,

Imejaa atiati,kujua lipi sahihi,

inaniishia hati,kuandika na kusihi,

Nitamuachia Mola,afanye haki jaala.

@2020

Ustadh Kamau.

Malenga Mfawidhi.

Thika.

 

*BURIANI PROFESA KEN WALIBORA*

Laiti tungalijua

Tungalimsihi sikunyakue

Jamani profesa wetu

Was fasihi na Kiswahili jumla

Profesa Ken Walibora

Ingekuwa Bora usingetuwacha

Nilidhani ilikuwa ndoto

Na SI ndoto ya Amerika

Labda Ni zaidi yake Amerika

Najuta zaidi ya kujuta

Imekuwa SI ndoto Tena

Imekuwa SI siku Njema Tena

Laiti ningalijua

Ningalikuandikia mapema

Sahiba wa kufa kuzikana

Ingawa hatukupatana

Mahuluki na ndwele wanamenyana

Imekuwa Ni kufa na kuzikana

Nilidhani siku Moja takupata

Univukishe mipaka

Mipaka ya uandishi

Malenga Chipukizi ninalia

Kidagaa kimeniozea

Chozi limegeuka damu nyeusi

Waswahili tumejitia ububu

Kusema labda tujaribu

Tufafanulie babu

Tena kwa utaratibu

Dhamirake “Nizikeni Papa hapa”

Umekuwa mgumu mjarabu

SI hadithi fupi

SI riwaya

SI mashairi

SI uanahabari

SI makongamano

SI makala anuwai

Twakuvisha taji shehe, mekikuza Kiswahili

Ufanisi wako shehe, dhahabu unastahili

Vipaji tunavyo shehe, kukikuza Kiswahili

Najiuza mie shehe, wanijie mwanamwali

Nanena, Dua Njema kwa Rabuka

Nanena, akuangazie wa milele mwanga

Nanena, kwa amani pumzika

Nanena, pale pale tutakuzika

Nanena, machozi hayeshi profesa

Nanena, Basi liwe kwetu Chozi la Heri.

Kama Lile la Assumpta Matei.

*KAWIRA ESTHER SUSAN*

*Malenga Chipukizi,*

*CHUO KIKUU CHA CHUKA

 

NENDA SALAMA MWALIMU

Yalaiti umauti, ungasubiri katiti

Unong’oneze wakati, tungafanya mikakati

Ela wetu muhabati, yamemfika mauti

Pole mwana wa mwalimu, utaishi mtimani

 

Pole mwana wa mwalimu, kifo kimekuchaguwa

Na kilivyokidhalimu,mwalimu hakuuguwa

Waja tungekihukumu, bali yote majaliwa

Kiswahili kimefiwa, twasema sote makiwa

 

Kiswahili kimefiwa, hayu nasi jemedari

Mwanga tuliojaliwa, kwa sasa umejibari

Na simanzi ‘mepaliwa, hali zetu sio shwari

Ni ngumu hali ingawa, tamwombea kwa Qahhari

 

Na ngumu hali ingawa, kwa Mola twatakadamu

Khuzuni ingatujawa, faradhi kwa  binadamu

Kudumu muhali kuwa, safari mekulazimu

Mepaa kwa zako mbawa, mekwenda kwenye hukumu

 

Mepaa kwa zako mbawa, mzawa wa Cherengani

Daima utaenziwa, likuwa mwenyi thamani

Ingawa utafukiwa, wakutiye mchangani

Yapaswa wewe kujuwa, utaishi mtimani

Adamu Jibril (Abu Sanaya)

Malenga wa Jangwani

Nairobi Kenya.

 

WALIBORA

Lifikapo jambo hili, huwa ngumu kusadiki,

Na hali huibadili, daima huwacha dhiki,

kakiacha kiswahili,  Walibora kafariki,

Makiwa hayaneneki. kimefiwa kiswahili.

 

Kakiacha kiswahili, kama matoto ya nyuki,

Kimengiwa idhilali, na walizi taharuki,

Imezimika kandili, Walibora kafariki

Makiwa hayaneneki. kimefiwa kiswahili,

 

Imezika kandili, kiza kimetamalaki,

Aloshika muhimili, kafwata njiya ya haki,

Kimeondoka kivuli, Walibora kafariki,

Makiwa hayaneneki, kimefiwa kiswahili.

 

Kimeondoka kivuli, makao hayakaliki,

Tena kime kwenda mbali, kwa pumzi hatufiki,

Ametuondoka nguli, Walibora kafariki,

Makiwa hayaneneki, kimefiwa kiswahili.

 

Ametuondoka nguli,  pengole halizibiki,

Kweli dunia bahili,  ya Robarti naafiki,

Imezimika kauli, Walibora kafariki,

Makiwa hayaneneki, kimefiwa kiswahili.

 

Imezimika kauli, tumombee kwa Maliki,

Amfanyie  sahali,  na pepo ambariki,

Ametutenga kimwili, Walibora kafariki,

Makiwa hayaneneki, kimefiwa kiswahili.

 

Ametuntenga kimwili, rohani hatubanduki,

Hako aliye batali, akaepa kitu hiki,

Lugha imepata feli, Walibora kafariki,

Makiwa hayaneneki, kimefiwa kiswahili.

 

Lugha imepata feli, kadimati rafiki,

Mapenzi yake Jalali, daima hayakwepeki,

Inabidi tukubali, Walibora kafariki,

Makiwa hayaneneki, kimefiwa kiswahili.

MKANYAJI

HAMISI A.S KISSAMVU, DSM

 

BURIANI PROFESA, LALA SALAMA MUFTI:

Jumatano naamka, habari zanifikia,

Walibora metutoka,ninakiri ninalia,

Kifo hiki kimefika,chanifanya kuduwaa,

Buriani Profesa,lala salama Mufti.

 

Liandika Siku Njema,mawazoye kayakweza,

Maarifa tukachuma,yako ngoma twaicheza,

Naingoja siku njema,kiondoke hiki kiza,

Buriani Profesa,lala salama Mufti.

 

Nani asiyekijua,Kidagaa kilichooza,

Akili kilizindua,maudhui kiyakweza,

Maadili kachochea,kalaani yalooza,

Buriani Profesa,lala salama Mufti.

 

Ustadh ninakiri,naipenda ile ndoto,

Amerika kusafiri,imekuwa ili moto,

Yapandisha yangu hari,ninampa chake kito,

Buriani Profesa,lala salama Mufti.

 

Mauti yamemtwaa,memchukua Walibora,

Nimepigwa na butwaa,mauko si kitu bora,

Hivi sasa nanyamaa, heshima bila papara,

Buriani Profesa,lala salama Mufti.

 

Nakuomba moyo wangu,yakubali yalofika,

Japokuwa ni machungu, Maulana atashuka,

Thawabu nzima chungu,atampa kimvika,

Buriani Profesa,lala salama Mufti.

 

Karimu ninakuomba,mlaze pema peponi,

Wewe ndiwe kamuumba,kamleta duniani,

Ninajua tampamba,thawabu paradisoni,

Buriani Profesa,lala salama Mufti.

Simon M. Wachira

‘Ustadh Sinajina’

Shule ya Msingi Mathia :Kirinyaga

 

BURIANI WALIBORA

Midadi Naizagaza,  japo mwingi wa simanzi,

Machozi yanichiriza, moyo wangu una ganzi,

Sitoweza kujikaza, kaenda nilomuenzi,

Tangulia walibora,  Farisi wa Kiswahili.

 

Habari nilizipuza, hakika sikusadiki,

Nilidhani wanacheza,  wandishi wapenda kiki,

Ila ziliniduwaza, baada ya kuhakiki,

Tangulia Walibora, Farisi wa Kiswahili.

 

Dunia imepoteza, Nguli gwiji na galacha,

Ni mengi ulochangiza,  ya lugha na litrecha,

Hakuna wa kulijaza, pengo lako uloacha,

Tangulia Walibora, Farisi wa Kiswahili.

 

Sitoweza endeleza,  beti nne nitakoma,

Pepani naona giza,  mkono unatetema,

Ni kweli hakitaweza,  kudumu kilichochema,

Tangulia Walibora, Farisi wa kiswahili.

Malenga: Gambo Bin Masomo.

Chuo Kikuu cha Pwani.

 

BURIANI WALIBORA

Shairi ninalitunga,machozi yakinitoka,

Kama mtoto mchanga,hakika natatizika,

Nimeshindwa na kulonga,maneno yametoweka,

Buriani Walibora,tulia pema mbinguni.

 

Dunia hii dunia,Ina mengi masaibu,

Waswahili wanalia,huzuni umewasibu,

Meshindwa na kuongea,mewaacha na taabu,

Buriani Walibora,tulia pema mbinguni.

 

Hakuna sampuli yako,hilo naliweka wazi,

Kuboronga kwako mwiko,mlezi wa chipukizi,

Gwiji wa mtiririko,twazipenda zako kazi,

Buriani Walibora,tulia pema mbinguni.

 

Ni Mola amekuita,toka hapa duniani,

Lienda bila kusita,katuacha majonzini,

Mauti yamekugota,Nahodha wa yetu fani,

Buriani Walibora,tulia pema mbinguni.

Everlyne Makhakha,

“Mtumbua majipu”

 

NAKUAGA WALIBORA

Nashika yangu kalamu, machozi yakinitoka,

Moyo unavuja damu, uchungu ulonifika,

Wema kumbe hawadumu, wakati wao kifika,

Nakuaga Walibora, profesa wa fasihi.

 

Mekuwa mtu muhimu, hasa kwangu nakumbuka,

Nikikupigia simu, ya hekima litamka,

Mauti kitu dhalimu, hwacha tozi kidondoka,

Nakuaga Walibora, Profesa wa fasihi.

 

Maneno yako adhimu, nilipenda ukimaka,

Kiswahili lugha tamu, iliweza kutumika,

Ni nani atanikimu, ulivyokuwa hakika?

Nakuaga Walibora, profesa wa fasihi.

 

Kazi yenu mahasimu, linifanya kuzinduka,

Diwani yenye utamu, WAJA LEO lisukika,

Ndiyo ilinipa hamu, nikaanza kuandika,

Nakuaga Walibora, profesa wa fasihi.

 

Ninamuomba Rahimu, peponi kusitirika,

Pengolo kwangu dawamu, haliwezi kuzibika,

Kukuita Marehemu,ulimi wanikatika,

Nakuaga Walibora, Profesa wa fasihi.

 

Mwisho wako umetimu, duniani kuondoka,

Jambo moya ufahamu, huwezi kusahulika,

Wengi tulikuheshimu, njia kitupa mwafaka,

Nakuaga Walibora, profesa wa fasihi.

 

Ken mwana wa mwalimu, kiharusi menishika,

Akilini utadumu, kwa mkono kunishika,

Wape insia salamu, wa peponi ukifika,

Nakuaga Walibora, profesa wa fasihi.

Allan Lumunyasi Chevukwavi.

Mwoshashombo.

Nairobi.

 

Lala Pema Walibora

Kwa nguvu zake Kudura, natanguliza shairi,

Kwa Wapwani na Wabara, ni kilio kimejiri,

Edi ninazo hasira, kumpoteza jabari,

Lala pema Walibora, penye wema na pazuri.

 

Ni pigo tena hasara, kwetu sisi washairi,

Imekuwa ni ibura, kuondoka jemedari,

Kuelekea akhera, pasi kutupa kwaheri,

Lala pema Walibora, penye wema na pazuri.

 

Umeondoka sogora, ulo mwandishi hodari,

Kazi zako zilo bora, kote zimekithiri,

Kwa mtazamo na sura, zimeandikwa vizuri,

Lala pema Walibora, penye wema na pazuri.

 

Imeanguka tiara, tu mashakani tayari,

Twajililia ja jura, na mambo hayako shwari,

Hukuwa nayo papara, kwetu ikawa fahari,

Lala pema Walibora, penye wema na pazuri.

 

Nakoma sitii fora, kifo kimeniathiri,

Macho yangu yamefura, kwa machozi ya tiriri,

Nafunga kwa mkarara, siendelezi shairi,

Lala pema Walibora, penye wema na pazuri.

Edison Wanga,

Son Bin Edi,

Mwana Wa Mambasa,

Mambasa.

 

BURIANI WALIBORA

Machozi yamenitota,mi mwenzenu sijifai

Umebomoka ukuta,walibora hana uhai

Zimwi limekutafuta,na rohoyo kuidai

Buriani walibora,ulazwe mahali pema

 

Ulitufunza subira,kwa riwaya Siku Njema

Limujenga kongowera,mtu asokata tama

Mapunda kawa tambara,kwa kuwinda walo wema

Buriani walibora, ulazwe mahali pema

 

Ubaguzi limulika,marekani darasani

Liona kweli hakika,tabu zake Fikirini

Mweusi hana tambuka,ng’ambo huko libaini

Buriani walibora, ulazwe mahali pema

 

Ukabila donda hili,kwa hadithi lilipinga

Maukoye Maende kweli,yalikuwa kubwa janga

Hawakujali yake hali,hata ile ya kukonga

Buriani walibora, ulazwe mahali pema

 

Kikaja kile kidaga,wengi kikawaozeya

Nasaba bora lipiga,Wa haki waloteteya

Kawafanya kama mboga,Himila akawapeya

Buriani walibora, ulazwe mahali pema

 

Otii naye Wanjiru,yao ndoa lishutumu

Lisema tujikusuru,hali zetu kufahamu

Na wale walioguru,semi zao tuheshimu

Buriani walibora, ulazwe mahali pema

 

Ya koinange usiku,liyaweka paruwanja

Ulitaja tunoshuku,siri zao ukapunja

Wahubiri Wa mabuku,vyapo vyao huvivunja

Buriani walibora, ulazwe mahali pema

 

Beti nane memaliza,chini naweka kalamu

Japo keni atuliza,alosema tufahamu

Tusije damu kulaza, kumufungiya saumu

Buriani walibora, ulazwe mahali pema

©Mwalimu Muhatia

(Msakatonge)

 

Ya kuwaa mishumaa, mbona ghafula huzima,

Wakati ndio twakaa, vizuri kuitizama,

Kutuonya yenye waa, nasi tupate andama,

Ai kifo na kutwaa, zile roho safi njema

 

Hiki kivumvu kuwa, na moyoni kunivama,

Na kwikwi pasi kutuwa, ndani hasonga ruhuma,

Sina wa kunilimuwa, mwalimu amenihama,

Ai kifo na kutowa, zile roho safi njema

 

Ni kilio na kutweta, mitilizi kuandama,

Kwa mayondi kunipata, yenye kukusa kuhema,

Mtangani nikasota, kwa kite kisichokoma,

Ai kifo na kukata, zile roho safi njema

 

Mauti yana adhaba, huacha huzuni nyuma

Hujitiya ukuruba, kwa mmoya yakakwima,

Ndipo hawa ni msiba, wala si yeo ni zama,

Ai kifo na kuiba, zile roho safi njema

Jacob Ngumbau Julius, Nairobi.

 

Leo sio siku njema,Kama hapo walibora

Umahiri umezama,tumelia tukafura

Metoweka mja mwema,kifo hakina subira

Walibora kuondoka,ni pigo kwa waswahili

 

Safari ya amerika,pamoja na siku njema

Ni yeye ameandika, alikuwa na hekima

Hatutaki kuachika,mioyo inainama

Walibora kuondoka,Ni pigo kwa waswahili

 

Mimi naye kukutana,kongamao la chakita

Alikuwa muungwana,Tena hakupenda Vita

Mawaidha liyanena,mema Wala si matata

Walibora kuondoka ni pigo kwa waswahili

 

Waswahili chipukizi,wote tulikutizama

Kazi zako tukaenzi,Sasa tunashika tama

Uliwa chetu kipenzi,mengi hatuwezi sema

Walibora kuondoka, Ni pigo kwa waswahili

 

Gazeti taifa leo,  Kila siku na kauli

Wosia wa kila Leo,ulitukuza kwa kweli

Ulikuwa kimbilio,lipokuwa ngumu Hali

Walibora kuondoka ni pigo kwa waswahili

 

Tutafuata zako nyayo,mbeleni tutahadithi

Sisi hatutafa moyo,tutawa wako warithi

Twahuzunika kwa hayo,lakini tutahadithi

Walibora kuondoka ni pigo kwa waswahili

 

Tunakuomba rabuka,uwalinde waswahili

Na uwaongeze miaka,hekima wainakili

Maisha yao twaweka,kwako ili uwajali

Walibora kuondoka ni pigo kwa waswahili

Wairimu Weru

Mchele wa chenga

Chuo kikuu Cha Moi

 

MHISANI KAFA JINA

Kazi ya Mola Jalali, huwa haina makosa,

Hata ingawa sahali, au gumu kwetu hasa,

Hutujuzu tukubali, ma’na huwa ishapusa,

Ninashindwa kuamini, Walibora katuwacha.

 

Moyoni nina huzuni, na jalada la ukungu,

Machozi mengi machoni, kila kiungo kichungu,

Kuondoka kwa mwandani, ni uchungu walimwengu,

Ninashindwa kuamini, Walibora katuwacha.

 

Habari za kuatua, zilitua Jumatano,

Wengi tukaomba dua, yakichacha malumbano,

Ati kaaga Jambia, mtaa wa Mfangano,

Ninashindwa kuamini, Walibora katuwacha.

 

Kennedy Waliaula, kijana wa Mualimu,

Umetughubisha dhila, himaya ya waalimu,

Tumeshindwa hata kula, umetukosesha hamu,

Ninashindwa kuamini, Walibora katuwacha.

 

Hufa na mswano wake, muwa haki walimwengu,

Hazina ya kichwa chake, ‘tafukiwa dungudungu,

Huku kutupiga teke, twamuwachia Mulungu,

Ninashindwa kuamini, Walibora katuwacha.

 

Moyo wanitoja damu, ninaloa karatasi,

Jina lako litadumu, kwa hizi zetu nafusi,

Majagina wasalimu, Chinua na Euphrase,

Ninashindwa kuamini, Walibora katuwacha.

Ramadhan Abdallah Savonge,

“Malenga Wa Nchi Kavu”, Kivumanzi

 

BURIANI WALIBORA

Kifo hakina huruma,matozi yanidondoka,

Naandika nayasema,huzuni umenivika,

Gwiji wetu amezama,mwandishi ametoweka,

Buriani Walibora,safiri salama Bingwa,

 

Duniyani tunapita,haya kweli ni maisha,

Unatukumba utata,mengine yahuzunisha,

Kifo kinapokuita,jamani chaharakisha,

Buriani Walibora,safiri salama Bingwa,

 

Mwandishi wetu mahiri,kazi yako livutiya,

Uliyekuwa hodari,utunzini libobeya,

Kiswahili kwako shwari,wengi walikusifiya,

Buriani Walibora,safiri salama Bingwa,

 

Liandika Siku njema,kidagaa kumwozea,

Kapewa kwote heshima,tuzo ewe jizolea,

Nchini ukaja vuma,habari kuzipokea,

Buriani Walibora,safiri salama Bingwa,

 

Ulikuwa mshairi,takukumbuka malenga,

Wengi waliyakariri,bila kuwapiga chenga,

Ubunifu ninakiri,walibora ulilenga,

Buriani Walibora,safiri salama Bingwa,

 

Maisha yako jamani,yalitupeya motisha,

Safari toka zamani,wengi sana nufaisha,

Kujituma masomoni,hilo ulihakikisha,

Buriani Walibora,safiri salama Bingwa,

 

Kiswahili ulikuza,Radioni runingani,

Kisabuni kujikaza,kokote mitandaoni,

Lugha tusije poteza,Sheng’i iwe namba wani,

Buriani Walibora,safiri salama Bingwa,

 

Hakika tulikupenda,Mola kupenda zaidi,

Mazuri uloyatenda,nasisi tajitahidi,

Kule wewe unaenda,takutana naahidi,

Buriani Walibora,safiri salama Bingwa,

 

Ni mengi sitamaliza,nomba neze kumaliza,

Kurasa naweza jaza,walibora mwomboleza,

Hakuna kunikataza,labuda kunituliza,

Buriani Walibora,safiri salama Bingwa,

SEME DUNCAN

Sememshairi254

“Malenga wa Kiminini”

 

Ukweli sijaamini,Walibora kuondoka,

Tuna majonzi nchini,maovu yametendeka,

Naumia mtimani,machozi yatiririka,

Jagina ametuacha,buriani Walibora.

 

Watu wengi wakutamani,na kwa sasa wakutaka,

Ulifunza darasani,ukavuka na mipaka,

Ulifika Marekani,na huko ulitajika,

Jagina ametuacha,buriani Walibora.

 

Utabaki akilini,na ukweli hutatoka,

Hivyo basi duniani,twajua ulisifika,

Tuanze na redioni,ambapo ulisikika,

Jagina ametuacha,buriani Walibora.

 

Makala magazetini,ni mengi uliandika,

Na hadithi vitabuni,ulichapisha hakika,

Tutafanyaje jamani,ametuacha haraka,

Jagina ametuacha,buriani Walibora.

 

Ni kifo cha walakini,amekuita Rabuka,

Na waswahili poleni,bado mtamkumbuka,

Hatuna matumaini,waenda kupumzika,

Jagina ametuacha,buriani Walibora.

 

Kalamu naweka chini,moyo wangu wateseka,

Ni machozi mashavuni,ningali nimeshituka,

Tutakutana peponi,siku yangu ikifika,

Jagina ametuacha,buriani Walibora.

Malenga Kitongojini,

Lionel Asena Vidonyi,

Seeds High School,Kitale.

 

KIFO CHAKE WALIBORA

Nimepokea tanzia, kwenye vyombo vya habari,

Ya kwamba amejifia, mwanalugha mashuhuri,

Mwandishi alobobea, kwa riwaya na shairi,

Kifo chake Walibora, kimenitia huzuni.

 

Gwiji Ken Walibora, alitutia hamasa,

Kwayo kazi yake bora, iliyopigwa msasa,

Toka Pwani hadi Bara, alienziwa kabisa,

Kifo chake Walibora, kimenitia huzuni.

 

Kazi zake za sanaa, kama vile Siku njema,

Na novela -Kidagaa, duniani zilivuma,

Wasomi ziliwafaa, wa kisasa na wa zama,

Kifo chake Walibora, kimenitia huzuni.

 

Mutisya ninashangaa, Mrithi wake ni nani?

Kote atakayeng’aa, Kenya hadi Marekani,

Mwandishi alokomaa, Sogora wa hino fani,

Kifo chake Walibora, kimenitia huzuni.

 

Pengo aliloliacha, ni vigumu kuzibika,

Ken alikuwa kocha, kwa wale wanaibuka,

Usiku mchana kucha, alikuwa aandika,

Kifo chake Walibora, kimenitia huzuni.

 

Kweli mshale mzuri, haukai ziakani,

Na kalamu ya Kahari, haikosi asilani,

Alivyokuwa mzuri, ametuondoka Ken,

Kifo chake Walibora, kimenitia huzuni.

CORNELIUS MUTUKU MUTISYA

“Malenga wa Kaviani”

WAKITA-MACHAKOS

 

Mauko yametupoka

Tumepigwa bumbuwazi, akili zimebanana

Zimebaki kumbukizi, za kupoteza mungwana

Tuachie Maulana, atulizaye banguzi

Mauti yametupoka, Walibora mtajika

 

Jagina wa kutajika, metuacha na huzuni

Kazi zake zasifika, kwa weledi na kubuni

Vitabu vya kuandika, makala hata matini

Walobaki tujimudu,  twendeleze kazi yake

Amos Sitati (Baharia wa nchi kavu)

 

Jahazi

Jahazi letu lazama,limepigwa na dhoruba,

Jahazi limekuwama,nyufa hatujaziziba,

Jahazi na limegoma,kifo sitamani toba,

Jahazi kuna zahama,abiria waomba Baba.

Jahazi linaelea,nahodha dira poteza,

Jahazi nyuma tembea,safari hajamaliza,

Jahazi lazembea,nahodha shindwa ongoza,

Jahazi yumba sogea,abiria menyamaza.

Jahazi langanganiwa,wasojua usukani,

Jahazi latamaniwa,wengi wataka mbeleni,

Jahazi linamezewa,wengi mate watamani

Jahazi linaibiwa,maizi wamo chomboni.

Jahazi yenda mrama,majini tutavamiwa,

Jahazi lina zahama,watu mechanganyikiwa,

Jahazi nitalihama,nahodha talaumiwa

Jahazi nimelisoma,nahodha ameshindiwa.

Jahazi laenda joshi,walio ndani walia,

Jahazi kuwa mazishi,kilalama utafia,

Jahazi hatufikishi,uhuru tulobania,

Jahazi kuwa uzushi,tamaa wameridhia.

Josphat Cheruiyot,

Duma Mla Nyasi,

Longisa Bomet.

 

Mauti Ya Walibora!

Sijanyamaza nalia, Jumatano kikumbuka,

Nikapokea tanzia, Walibora katutoka,

Nikadhani ni umbea, sikuamini hakika,

Mauti ya Walibora, Kiswahili kimefiwa.

 

Kikumbuka Ijumaa, Walibora katoweka,

Familia hikujua, libaki kuhangaika,

Ajali ilitokea, na basi likatoroka,

Mauti ya Walibora, wakenya mepungukiwa.

 

Sikudhani ngetokea, tanzia kumwandikia,

Walibora kumwambia, kwa heri ametutoka,

Walibora lichangia, tanzu zote liandika,

Mauti ya Walibora, fasihi metingizika.

 

Riwaya alichangia, Siku Njema kaandika,

Na pia Tamthlia, Mbaya Wetu nakumbuka,

Mashairi katungia, Hadithi Fupi kandika,

Mauti ya Walibora, ni janga kubwa hakika.

 

Matangazo lichangia, idhaa alisifika,

Makala alichangia, Taifa Leo hakika,

Mihadhara akitoa, ukumbi ulifurika,

Mauti ya Walibora, wasomi mepungukiwa.

 

Vyuoni alichangia, Marekani alifika,

Mafunzo akayatoa, ugenini kaenzika,

Sauti ya kuvutia, kutoa pangoni nyoka,

Mauti ya Walibora, ni pengo lisozibika.

 

Walibora tunalia, mayatima megeuka,

Ni muhali kufidia mahiri alotutoka,

Wandishi lirejelea, kazi zake liandika,

Mauti ya Walibora, msiba umetufika.

 

Nimekabwa na hisia, kalamu imedondoka,

Kikombe tele melia, machozi yasokauka,

Kumbukizi tabakia, gwiji wetu pumzika,

Mauti ya Walibora, rambirambi nimetoa.

FRANKLIN MUKEMBU

Mawimbi Ya Nchi Kavu

Kajuki-Nithi

 

WEMA HAWADUMU

Níjile wenu rijali,nami niunge kaumu

Nikuli yenye thakili,isomwe kwenye nudhumu

Moyo umengia feli,nawajuza mufahamu

Hawadumu duniani,waja wenye insafu

 

Najikaza kulihali,msidhani chakaramu

Ijapo yananidhili,na kunizulia pumu

Inabidi kukubali,hatutamwona dawamu

Hawadumu duniani,waja weñye insafu

 

Ni vigumu kukubali,hatuwezi mzuhumu

Ya kwamba ni ajali,iliyomtoa humu

Inabidi kuhimili,japo kweli lahujumu

Hawadumu duniani,waja wenye iñsafu

 

Angalikuwa yu dhuli,mgonjwa kila timu

Iwe mbaya yake hali,ukongo wamdhulumu

Ingekuwa afadhali,kukubali yalotimu

Hawadumu duniani,waña wenye iñsafu

 

Alizofanya amali,ndugu yetu muadhamu

kukikuza Kiswahili,kwayo ghera na nidhamu

Ni wazi tunastahili,kuzidisha yetu hamu

Hawadumu duniani,waja weñye iñsafu

 

Tumuachie Jalali,yale tusoyafahamu

Tusiulize maswali,yanayopuliza sumu

Hukumu yake ni kali,kwa ndugu na mahasimu

Hawadumu duniani,waja weñye insafu

 

Naiombea famili,amani yao idumu

Wafanyiwe tasihili,kwa kila lilo muhimu

Kulihusu jambo hili,dunia sio karimu

Hawadumu duniani,waja wenye insafu

 

Walibora wastahili,kusifiwa kwa nudhumu

ulivyofanya shughuli, lugha iwe na utamu

Nimesema kwa kalili,shairi limehitimu

Hawadumu duniani waja wenye insafu

Moses Chesire

Sumu ya waridi

Kitale,Kenya

SUMU YA WARIDI

 

SAFIRI SALAMA WALIBORA

Waswahili jongeeni,niseme yalo moyoni

Niseme yalo moyoni,ni mazito si utani

Ni mazito si utani,uamumuzi wa Manani

Mola keshamchukua ,safiri salama bingwa

 

Sitini na nne mwaka,kazaliwa kwa hakika

Kazaliwa kwa hakika,Baraki Kijiji chake

Baraki Kijiji chake,Bungoma gatuzi lake

Mola keshamchukua, safiri salama bingwa

 

Elimu hakuchezea,hilo wazi twalijua

Hilo wazi twalijua,kwa yake nyingi hekima

Kwa yake nyingi hekima,vitabuni kaachia

Mola keshamchukua, safiri salama bingwa

 

Habari za kifo chake,hatimae lisikika

Mara kama ni utani,Mara kama ni ukweli

Na kwa kuwa lisemwalo,bila shaka huwa lipo

Mola keshamchukua, safiri salama bingwa

 

Na zilipothibitishwa,habari za kifo chake

Machozi hayakusita,yakawa yanidondoka

Haswa niliposikia,kagongwa nayo matwana

Mola keshamchukua ,safiri salama bingwa

 

Ingawa we umeaga,kazi zako zipo hai

Na daima zitadumu,mauti hazitoonja

Pengo lako atoziba,hatujampata bado

Mola keshamchukua, safiri salama bingwa

 

Kikomo nimefikia,hizi zangu saba beti

Pia ni dua kwa Mola,arehemu roho yake

Na ailaze mahali,pema Tena ni peponi

Mola keshamchukua, safiri salama bingwa

OKELLO ODWOLI JACOB

KAUNTI YA BUSIA

 

Hapa najikongoweza,Kongowea n’naamba,

Pole zangu naweleza,kwa mbolezi ninaimba,

Sauti ‘mi napaaza, sikiliza nawaomba,

Buriani profesa,daima tutakupeza.

 

Tumo sote kihoroni, nyoyo zetu mashakani,

Machungu yamo nyoyoni,kweli hatuna amani,

Walibora masikini,haupo metuagani,

Buriani profesa ,daima tutakupeza.

 

Maashiki tunalia, wapenzi wa Kiswahili,

Pengo umetuwachia,twalihisi pengo hili,

Na moyo ulitutia,kuienzi Kiswahili.

Buriani profesa, daima tutakupeza.

 

Ukawa hivi kwanini, ewe kifo nauliza?

Kwa Guru huna imani,roho ukajipokeza?

Umetutia huzuni,kipenzi mempoteza,

Buriani profesa, daima tutakupeza.

 

Ewe kifo ni hatari,kwa waja huna imani,

Haupo umesafiri,kwenda kwake Mkawini,

Ken mwandishi mahiri,utasalia nyoyoni,

Buriani profesa, daima tutakupeza.

 

Siku Njema kaandika,jamii kaelimisha,

Kidagaa kadhalika, shuleni ikafundisha,

Ken mwandishi tajika,wengi mewaelimisha,

Buriani profesa ,daima tutakupeza.

 

Makiwa kwa familia, jamaa na marafiki,

‘Mi nguvu nawatakia,na Karima ashiriki,

Mbinguni twaaminia,huko ndiko wastahiki,

Buriani profesa, daima tutakupeza.

Malenga Ustadh Kongowea Alex Barasa,

Kitale