Makala

Talaka chungu wabunge wa Mlima wakiendelea kumtema Gachagua

Na WAIKWA MAINA September 13th, 2024 3 min read

JUHUDI za Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kuunganisha Mlima Kenya zinaonekana kugonga mwamba baada ya wabunge 48 kumuasi na kutangaza sapoti ya kwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki.

Haya yanajiri siku chache baada ya wabunge wa kaunti za Mlima Kenya Mashariki za Meru, Embu na Tharaka Nithi kujitenga na Bw Gachagua na kumtangaza Prof Kindiki kuwa msemaji wao.

Bw Gachagua amekuwa akiendeleza jitihada za kuunganisha Mlima Kenya huku njia yake ya kuwa mgombeaji mwenza wa Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027 ikiwa telezi.

Hii ni baada ya wandani wa Kinara wa Upinzani Raila Odinga kuingia serikalini kwa kuteuliwa mawaziri.

Katika kile walichosema kuwa Maamuzi ya Nyahururu, wabunge hao walisema watamtumia Prof Kindiki kama ‘njia’ ya kumfikia Rais serikalini badala ya Bw Gachagua.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022, Profesa Kindiki alionekana kuwa kifua mbele kuwa mgombeaji mwenza wa Rais lakini mambo yakabadilika na Bw Gachagua kupewa nafasi hiyo dakika ya mwisho baada ya vuta nikuvute.

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah na Mwenzake wa Molo Kuria Kimani waliwaongoza wabunge 48 kutoa taarifa ya kumuasi Bw Gachagua na kusema uaminifu wao ni kwa Prof Kindiki.

“Kutokana na matukio ya sasa na yanayotarajiwa baadaye, kunahitajika kuwa na muunganishaji kati yetu na Afisi ya Rais kuhusiana na masuala ya maendeleo,” ikasema taarifa yao ya pamoja.“Kama viongozi waliochaguliwa kutoka Mlima Kenya, kwa niaba yetu na wakazi waliotuchagua, tumeamua kuwa atakayetuunganisha na serikali kuu ni Profesa Kindiki,” ikaongeza taarifa hiyo.

Wabunge hao wanaotoka kaunti za Kiambu, Murangá, Nyeri, Nyandarua, Kirinyaga, Nakuru, Laikipia na Nairobi, walisema Bw Gachagua ameshindwa kuonyesha uongozi bora na kukataa kuungana na Rais kuwaunganisha Wakenya.

“Juhudi zetu za kusaka maendeleo kwa watu wetu zimetatizwa na kukosekana kwa kiongozi ambaye anatuelewa na anayeweza kupeleka maslahi ya watu wetu kwa serikali kuu.

“Badala yake eneo la Mlima Kenya limegeuzwa uwanja wa kueneza siasa kali kwa manufaa ya mtu mmoja mwenye malengo yake ya kisiasa. Hii imetuzibia njia ya kupeleka maslahi yetu na ya watu wetu kwa Rais,” wakasema.

Bw Ichung’wah ni Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa huku Bw Kimani akiwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha katika Bunge lilo hilo.

Kadhalika, wamemrejelea Naibu Rais kama kiongozi dikteta ambaye amekuwa akiwatishia wakosoaji wake katika jitihada zake za kuunganisha Mlima Kenya.

“Nia yetu ya kuyapa maendeleo umuhimu imezimwa na mtu ambaye anatuona kama washindani wake hivyo basi kututishia. Lengo lake ni kutulazimisha kuunga maslahi yake serikalini ilhali bado ndiyo tumefika chini ya miaka mitatu tangu tutoke uchaguzini,” akaongeza Bw Kimani.

Mwakilishi wa Kike wa Nyandarua Faith Gitau alisema wameafikia uamuzi huo kuzima uhasama wa kisiasa ambao umekuwepo na kuhakikisha wakazi wanatimiziwa ahadi.

“Waliotuchagua wanatutarajia utumie nafasi zetu kuwaletea maendeleo ndiposa tumechukua hatua hii. Lazima tuimarishe sekta za kilimo cha kahawa, chai, viazi, makademia na ufugaji,” akasema.

Bw Kimani alisema kuwa wameamua pia kupigania mfumo ambao utahakikisha uwepo wa ugavi wa mapato unaonufaisha eneo hilo.

Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri alisema uamuzi wa wabunge hao sasa unazima siasa za ubabe ambazo Bw Gachagua alikuwa akitumia kujiweka kama kigogo wa siasa za Mlima Kenya.

Bw Gachagua hajawa akionana ana kwa ana na Bw Kiunjuri na Bw Ichung’wah ambao wamemkashifu kuwa amekuwa akimhangaisha Rais kwa ajili ya maslahi yake ya kibinafsi.

Bw Kiunjuri ambaye alichaguliwa kwa tikiti ya TSP amelaumu Naibu wa Rais kwa kuchangia wandani wa Bw Odinga kuteuliwa serikalini, kutokana na masharti yake makali kwa Ikulu.

Mbunge huyo wa Laikipia alidai hata Naibu Rais alihusika katika kufadhili maandamano ya Gen-Z nchini mnamo Juni na Julai ili kuporomosha uongozi wa Kenya Kwanza.

Bw Gachagua alimjibu akimrejelea kama ‘mwanasiasa wa tumbo’ anayelipwa ili kumtusi na kumtaka atoe ushahidi kuhusu madai yake.

Hata hivyo, baadhi ya wandani wa Bw Gachagua akiwemo wabunge James Gakuya (Embakasi ya Kaskazini), Benjamin Gathiri maarufu kama Meja Donk (Embakasi ya Kati), Seneta wa Murang’a Joe Nyutu miongoni mwa viongozi wengine wameamua ‘kusimama’ na Naibu Rais.