Michezo

‘The Three Lions’ wadumisha ubashiri kwa kutua fainali Euro 2024 kwa kishindo

Na MASHIRIKA July 11th, 2024 1 min read

BERLIN, Ujerumani

Three Lions ya Uingereza ilidumisha ubashiri wa kuwa mmoja wa wagombea halisi wa taji la Kombe la Ulaya (Euro) 2024 baada ya kunyoa Uholanzi 2-1 katika nusu-fainali ya pili Jumatano.

Vijana wa kocha Gareth Southgate waliongoza ubashiri wa kompyuta maalum ya Opta kabla ya mashindano hayo ya mataifa 24 kuanza mnamo Juni 14 na sasa wananusia taji lao la kwanza tangu Kombe la Dunia mwaka 1966. Watavaana na Uhispania katika fainali ugani Olympiastadion hapo Julai 14.

Waingereza wana rekodi nzuri dhidi ya Uhispania katika dimba la Euro. Walipepeta Wahispania 1-0 jijini London na 2-1 jijini Madrid katika robo-fainali mwaka 1968. Waingereza walitamba tena 2-1 mwaka 1980 katika mechi za makundi na kuwalima katika robo-fainali kwa njia ya penalti 4-2 mwaka 1996. Watakuwa wakikutana katika Euro kwa mara ya tano.

Kabla ya makala haya ya 17, Opta ilipatia Uingereza asilimia 19.9 ya kutwaa ubingwa ikifuatiwa na Ufaransa (19.1), Ujerumani (12.4), Uhispania (9.6), Ureno (9.2), Uholanzi (5.1) na mabingwa wa makala yaliyopita Italia (5.0).

Uhispania ya kocha Luis de la Fuente imeshinda mechi zake zote kutoka makundini na sasa inapigiwa upatu mkubwa wa kuponyoka na taji. Waingereza walipiga sare mbili katika kundi lao dhidi ya Slovenia na Denmark.

Kama tu jinsi Uhispania almaarufu La Roja ilivyotoka nyuma na kubandua Ufaransa 2-1 katika nusu-fainali ya kwanza Jumanne, Uingereza walilazimika kujituma zaidi ya kawaida kutupa nje Uholanzi.

Xavi Simons aliweka Uholanzi ya kocha Ronald Koeman kifua mbele dakika ya saba kabla ya Harry Kane kusawazisha kupitia penalti ya utata dakika ya 18 baada ya beki Denzel Dumfries kumchezea visivyo ndani ya kisanduku. Ollie Watkins alifungia Uingereza bao la ushindi dakika ya 90.

Uingereza sasa wamefika katika fainali mbili katika mashindano manne makubwa chini ya Southgate. Walipoteza kwa njia ya penalti 3-2 dhidi ya Italia katika makala yaliyopita jijini London.