Kimataifa

Trump abadili mbinu za kampeni, sasa anauza sera badala ya matusi

Na MASHIRIKA August 16th, 2024 2 min read

WASHINGTON, AMERIKA

ALIYEKUWA Rais wa Amerika Donald Trump ameonekana akianza kubadili mbinu za kampeni kutoka kwa jinsi alivyokuwa amezoeleka akitoa makeke makali dhidi ya wapinzani wake kwa kuyalenga maisha yao ya kibinafsi.

Trump alikuwa akimshambulia vikali Rais Joe Biden kutokana na ukongwe wake kabla ya kiongozi huyo kujiondoa kwenye kiny’ang’anyiro cha Urais mwezi uliopita sababu zilizohusishwa na kukonga kwake na wakati mwingine kulemewa kifikra.

Aliendeleza wimbi hilo hilo la kuelekeza matamshi yake makali kwa kumvamia kwa maneno makali Makamu wa Rais Kamala Harris ambaye sasa ndiye mwaniaji wa Democrats.

Wakati wakati wa hotuba yenye kurasa 45 katika hoteli anayomiliki ya Bedminster, New Jersey, Trump alionekana kubadili mbinu na kutomvamia Harris jinsi ambavyo wengi walitarajia.

Badala yake aligusia masuala yanayohusu Amerika na kuuza ajenda yake kwa raia.

Wengi wanahusisha hili kutokana na takwimu za kura za utafiti kuonyesha kuwa umaarufu wake unashuka huku ule wa Harris nao ukipanda.

Pia kubadilisha mikakati yake ya kampeni kumetokana kwamba baadhi ya madai ambayo amekuwa akitoa kuhusu uongozi wa Amerika na Bi Harris ni ya uongo.

“Hii ni mbinu yetu mpya ya kupata kura. Kiongozi wetu amepunguza semi kuhusu maisha ya kibinafsi ya mpinzani wetu kwa sababu hilo limefasiriwa kama matusi,” alisema Kellyanne Conway, mshauri wa Trump.

Akaongeza: “Kwa sasa mikakati ya ushindi wa Rais Trump upo wazi na kila raia wa Marekani anaiona, ipo kwenye sera.”

Katika hotuba yake Alhamisi, rais huyo wa zamani aliangazia sana sera huku akitaja bidhaa ambazo bei zao zimepanda wakati wa utawala wa Democrats.

Pia alizua maswali iwapo Harris anaipenda Amerika na iwapo anastahili kuongoza nchi hiyo akidai anaegemea mrengo Ukomunisti.

Trump amekashifiwa kuwa kando na kulenga maisha ya binafsi ya Harris, amekuwa akitoa madai ya uongo ambayo ameshindwa kuthibitisha.

Kwa mfano, amedai kuna mataifa mengine yameleta wafungwa wao wenye wazimu waishi Amerika kama wahamiaji.

Hata hivyo, hakuna takwimu kama hizo kutoka kwa Idara ya Uhamiaji ya Amerika ambayo inaonyesha wafungwa wahamiaji haramu wakiletwa nchini humo na hali yao ya kiakili.

Pia alidai bei ya unga na mayai imekuwa ikipanda Marekani lakini hilo likaishia kuwa uongo baada ya kubainika bei hizo zimekuwa zikishuka wakati wa utawala wa Joe Biden.

Pia bila shahidi amedai kuwa asilimia 100 ya nafasi za ajira zinazoundwa Amerika zinaendea wahamiaji haramu hasa watu weusi.

Pia amekuwa akisisitiza kuwa ndiye alishinda uchaguzi wa urais wa 2020 nchini humo ilhali ni wazi alibwagwa.

Japo sasa anaonekana amebadilisha mikakati, wengi wanasubiri kuona iwapo Trump atakuwa na nidhamu na kumakinia kampeni za sera au atarejelea mtindo wake wa kumvamia Harris kwa maneno makali kuelekea uchaguzi huo wa mnamo Novemba mwaka huu.

Pia wengi wanasubiri iwapo Trump atatawala mahojiano mawili ya urais anayotarajiwa kuwa nayo na Harris kabla ya uchaguzi huo.

Kwenye mahojiano na Rais Biden mnamo Juni 27 Trump aliwika na kuonekana kama mshindi kwa sababu Biden hakuweza kumudu baadhi ya majibu na alisahausahau kutokana na ukongwe wake.