Habari za Kitaifa

Furaha mezani, kilio shambani bei ya mahindi ikishuka

Na BARNABAS BII September 2nd, 2024 2 min read

WAKENYA watapata nafuu mifukoni, bei ya unga wa mahindi ikitarajiwa kushuka zaidi msimu huu wa mavuno na pia kuingizwa nchini kwa mahindi ya bei rahisi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Katika ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa, bei ya gunia la kilo 90 ya mahindi inatarajiwa kushuka kutoka kwa Sh4,600 hadi Sh2,200. Wakulima ambao wamekuwa wakiyahodhi mahindi yao nao wameanza kuyauza wakihofia hasara zaidi kutokana na kujaa kwa mazao hayo sokoni.

Tayari bei ya unga wa kilo mbili ya ugali imepungua kutoka Sh180 hadi Sh120 na bei hiyo inatarajiwa itashuka zaidi mahindi yakiwa mengi sokoni.

“Tulitarajia kuwa bei ingepanda ili tupate faida lakini jinsi hali ilivyo kwenye masoko, bei imeshuka hadi Sh2,000 na kutusababishia hasara kubwa,” akasema David Kosgei Mkulima kutoka Ziwa, Kaunti ya Uasin Gishu.

Wamiliki wa kampuni za kusaga mahindi ambao walihojiwa na Taifa Leo nao walisema kuingizwa kwa mahindi kutoka Tanzania na Uganda kumechangia zaidi kushuka kwa bei ya mazao hayo.

Tanzania ndilo taifa ambalo huuzia Kenya na nchi nyingine za ukanda wa EAC mahindi na mchele kwa kiasi kikubwa zaidi. Ina soko kubwa pia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Sudan Kusini.

“Bei ya mahindi inatarajiwa itashuka zaidi kutokana na pia msimu wa kuvunwa  kwa viazi, maharagwe na mazao mengine ambayo hutumika badala ya mahindi,” akasema Joshua Kosgei, anayemiliki kampuni ya kusaga mahindi Eldoret.

Haya yanajiri wakati ambapo Waziri wa Kilimo Dkt Andrew Karanja naye amefichua kuwa Kenya itayavuna magunia 70 ya mahindi kutoka magunia 46 msimu jana.

“Wakenya watapata nafuu kwa sababu tutayavuna magunia milioni 70 kutoka milioni 40-60. Hii itahakikisha taifa linajitosheleza kwa chakula,” akasema Dkt Karanja wiki jana akiwa mjini Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia.

Waziri huyo alisema mavuno yameongezeka kutokana na mpango wa serikali wa kutoa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima na pia mvua ambayo ilinyesha kwa wakati.

Na si ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa pekee, bei ya mahindi pia imepungua kwenye miji ya Kisumu na Nakuru. Gunia la kilo 90 sasa ni Sh3,400 kutoka Sh5,200 Kisumu huku ikiuzwa kwa Sh3,200 Nakuru.

“Ukanda wa Magharibi mwa Nchi wakulima watakuwa wakivuna mahindi huku serikali pia ikileta mengine kutoka mataifa ya EAC. Hii itachangia bei kupungua zaidi,” akasema Joshua Too, mkulima kutoka Moiben Kaunti ya Uasin Gishu.

Utawala wa Kenya Kwanza umeahidi kuwa utaweka mikakati ya kuhakikisha Kenya inajitosheleza na haitaagiza mahindi kutoka nje ya nchi kufikia mnamo 2025.