Uncategorized

Utalipishwa faini ya Sh1 milioni ukipanda ‘ndengu’ bila kibali

Na COLLINS OMULO August 15th, 2024 2 min read

WAKULIMA wa pojo au maarufu kama ndengu, sasa watahitajika kuwa na leseni kushiriki kilimo cha zao hilo la sivyo watozwe faini ya Sh1 milioni au kifungo cha miaka miwili gerezani.

Mswada wa Pojo 2022 ambao upo mbele ya Bunge la Seneti unapendekeza adhabu hiyo kali wakati wabunge nao wanalenga kudhibiti sekta ya kilimo cha pojo nchini.

Aidha, mswada huo umeweka masharti makali katika utoaji leseni kwa wauzaji, watayarishaji na wakulima wakubwa wa maharagwe.

Mswada huo unaeleza kuwa, hakuna anayeruhusiwa kuuza, kutayarisha au kushiriki kilimo cha pojo au bidhaa zinazotokana na mazao hayo hadi wapate leseni kutoka kwa serikali ya kaunti husika.

“Mtu yeyote ambaye atakiuka masharti haya atatozwa faini ya Sh1 Milioni au afungwe kwa muda ambao haupungui miaka miwili,” inasema sehemu ya mswada huo.

Ili utekelezaji wake uimarishwe, mawaziri wa kaunti wataanzisha kamati ya kutoa leseni kwa wakulima.

Kamati hiyo baada ya kutathmini ombi, itamjibu mkulima baada ya siku 21 iwapo itampa leseni au la.

Mswada huo pia unasema serikali ya kaunti inaweza kuweka sheria inayotoa mwongozo wa kufuatwa kabla ya kutolewa kwa leseni.

Pia ni kaunti itakuwa inatoa habari au maelezo kuhusu kile kinachohitajika kuwasilishwa na anayetaka leseni.

Leseni ambayo imetolewa kwa kilimo cha pojo kwa mujibu wa mswada huo, itakuwa ikilipiwa kila mwaka.

“Kamati ya kaunti inaweza kufuta leseni hiyo iwapo mshikilizi wake amekiuka sheria au mwongozo wa kuipata au sheria yoyote ambayo kaunti inaona ni bora,” ukasema mswada huo.

Seneta wa Kitui, Enoch Wambua ndiye anadhamini mswada huo ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza kwenye seneti mnamo Februari 15, 2022.

Kisha ulielekezwa kwa michakato ya kisheria inayohitajika kabla ya kupitishwa Februari 2024. Mswada huo ulipitishwa pamoja na mabadiko yaliyopendekezwa na kufikishwa kwa Bunge la Kitaifa ambalo litakubaliana na seneti au kupendekeza marekebisho zaidi.

Aidha, waziri wa kilimo wa kaunti atahitajika kuweka rejista ya wakulima ambao wamepewa leseni kisha kuarifu Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA).

Pia waziri atakuwa na jukumu la kueleza AFA wale ambao leseni zao zimefutwa au muda wao wa matumizi kurefushwa kila tarehe tano ya kila mwezi.

AFA itaweka sajili ya wakulima wote, wanunuzi na asasi nyingine ambazo zimesajili au kutosajiliwa. Mswada huo pia unampa mamlaka waziri wa Kilimo kuibuka na mwongozo wa kudhibiti kutayarishwa kwa pojo, uagizaji wake nje ya nchi na kuuzwa mazao hayo nje ya nchi.

Usajili wa mkulima utakuwa na maelezo yote kumhusu, mahali anakoendeleza kilimo chake, ukubwa wa ardhi anakolima na aina ya pojo inayolimwa. Kaunti itaamua ada au matozo kwa wakulima ambao wamesajiliwa.

Bw Wambua amesema mswada huo utasaidia kuwatokomeza mabroka ambao wanawafilisi wakulima wa pojo. Hasa, alisema wakulima ambao wanashiriki kilimo cha pojo kutoka Kaunti ya Kitui watanufaikia jasho lao.

Kwa sasa, Bw Wambua anasema wakulima wananyanyaswa kwa sababu kila kilo inauzwa kwa Sh50 kisha mabroka nao wanaiuza kwa bei ya juu huku mkulima akibaki akihangaika na bei ya chini.