Makala

Wanaopigia debe pombe mitandaoni kukabiliwa na faini ya Sh500,000 na kutupwa jela  

Na LABAAN SHABAAN September 25th, 2024 2 min read

WATUMIAJI wa mitandao ya kijamii ambao watapigia debe matumizi ya pombe na dawa zingine za kulevya wanakabiliwa na faini ya Sh0.5 milioni na hatari ya kufungwa jela.

Wanaoandaa vipindi kwa ajili ya majukwaa ya kidijitali watakaopatikana na hatia ya kushawishi utumizi mbaya wa dawa za kulevya wanaweza kusukumwa jela miaka mitatu.

Kulingana na Sheria ya Kudhibiti Pombe ya 2010, wavumishaji watakaokiuka kanuni huenda wakakumbwa na pigo maradufu ya kutozwa faini na kutumikia kifungo gerezani kwa kipindi cha hadi miaka mitatu.

Sehemu ya 43(1) ya sheria hiyo inasema; “Hakuna mtu atakayevumisha matumizi ya pombe na vileo vingine isipokuwa kwa mujibu wa masharti ya Sheria hii.”

Ukiukaji wa matakwa haya ya sheria unaweza kusababisha athari mbaya, kama ilivyoorodheshwa katika Sehemu ya 43(2):

“Mtu atakayekiuka kifungu kidogo cha (1) anatenda kosa na atawajibika kulipa faini isiyozidi shilingi laki tano, au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja.”

Mnamo Jumanne Septemba 24, Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (Nacada) ilitoa onyo kali ikitilia uzito adhabu kwa wanaotumia mitandao ya kijamii kutukuza utumizi wa dawa za kulevya.

“Kukuza dawa za kulevya na matumizi ya dawa za kulevya kupitia mitandao ya kijamii sio tu kutowajibika bali pia ni ukiukaji wa sheria,” mamlaka hiyo ilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Hatua hizi za kutoa adhabu zinatokana na sheria kuu mbili: Sheria ya Kudhibiti Pombe ya 2010 na Sheria ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Dawa za Kisaikolojia ya 1994.

Sheria zote zinapinga waziwazi ukuzaji, utangazaji, au uhimizaji wa matumizi ya dawa za kulevya huku Nacada ikianza kupanua agizo hili kuangazia yaliyomo kwenye mitandao ya kijamii.

Tishio la faini kubwa na kuwafunga wahalifu ni kumbusho la jinsi serikali inajitolea kukabili kuvuma kwa vipindi vya kidijitali vinavyoandaliwa vikihusisha dawa za kulevya.

Msako wa Nacada unatoa onyo kali; hali ya kutukuza utumizi wa dawa za kulevya haitachukuliwa hivi hivi tu, haijalishi umaarufu wa wa mtu ama anawafikia watu wangapi.

Kulingana na Nacada, haya yanajiri kujibu kile mamlaka hii inataja kuwa “mwenendo unaoongezeka ambapo washawishi na waandaaji wa yaliyomo katika mitandao ya kijamii, wanachapisha maudhui ambayo yanahimiza matumizi ya dawa za kulevya.”

Nacada ina wasiwasi kuhusu athari za maudhui kama haya kwa hadhira changa; inaziona kama tishio kubwa kwa juhudi za kitaifa za kukabili  matumizi mabaya ya pombe na dawa za kulevya.