Habari za Kitaifa

Msiguse Gachagua, wakazi walilia Seneti wakitaka Naibu Rais asibanduliwe

Na GEORGE MUNENE October 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wa Kaunti ya Kirinyaga Jumatano waliandamana katika mji wa Kagio wakitaka Seneti kukataa uamuzi wa Bunge la Kitaifa wa kumtimua mamlakani Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Wakazi hao waliandamana barabarani kwa saa kadhaa asubuhi wakimpigia debe Naibu Rais huku Seneti ikikusanyika kujadili hoja ya kumng’atua mamlakani.

Walifunga barabara ya Kutus-Sagana wakiandamana na kusababisha msongamano wa magari kwenye barabara hiyo yenye shughuli nyingi.

Haya yalijiri baada ya kundi la wanawake kutoka Kirinyaga Jumanne kumuomba Rais William Ruto kumteua Gavana Anne Waiguru kuwa naibu wake endapo Naibu wake Gachagua atatimuliwa.

Kundi hilo lililojumuisha wanawake kutoka wadi zote 20 za Kirinyaga lilisema Bi Waiguru ndiye kiongozi anayefaa zaidi kuwa naibu wa Ruto.

Walitaja vituo vya Huduma Center na mfumo wa kidijitali, Ifimis, kama baadhi ya miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Waiguru alipokuwa waziri wa ugatuzi, wakisema anaweza kuaminiwa majukumu makuu.

Taharuki ilitanda, hata hivyo, Jumatano huku waandamanaji wanapinga Bw Gachagua kuondolewa wakizuia magari kupita.

Polisi waliovalia kiraia walitazama kwa mbali lakini hawakutatiza waandamanaji walioapa hakuna vitisho vitakavyowazuia kusimama na Gachagua.

Biashara zilifungwa kwa muda huku wauzaji wakifunga upesi maduka nao waandamanaji wakiimba kumshutumu rais kwa kula njama ya kumtimua naibu wake.

Walisisitiza kimya cha rais kinaashiria wazi kwamba anaafikiana na uamuzi wa kumtimua Gachagua.

“Naibu Rais wetu anapigwa vita kisiasa kwa kuwatetea raia wanaofurushwa kutoka makazi yao na masoko na kupinga ufisadi,” alisema mkazi, Judy Wanjiku.

Walimtaja Bw Gachagua kama mwanasiasa mwenye hadhi ya juu zaidi katika eneo la Mlima Kenya na kigogo wao anayestahili kuheshimiwa na kupatiwa fursa ya kukamilisha hatamu yake ya miaka mitano bila kuhangaishwa.

“Tunategemea maseneta. Wanapaswa kumwokoa Gachagua,” alisema mkazi mwingine.

Wakazi hao hasa walimrai Seneta wao Kamau Murango kutounga mkono maafikiano ya utimuaji katika Seneti.

“Tunamsihi Bw Murango apige kura kupinga, anapaswa kuwa jasiri na kumtetea Gachagua bungeni na kuhakikisha hatobanduliwa kutoka kiti chake,” alisema mkazi, Joseph Njenga