Habari za Kaunti

Mauti madaktari wakidinda kumhudumia mama mjamzito sababu ya mgomo

Na PIUS MAUNDU October 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MWANAMKE mmoja aliyekuwa mjamzito amepoteza mtoto wake baada ya wahudumu wa afya katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Machakos kukataa kumhudumia kufuatia mgomo unaoendelea katika kaunti hiyo.

Mary Mueni alilazimika kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Makueni ili kuokoa maisha yake na yale ya mwanawe.

‘Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Machakos walikataa kumhudumia wakitaja mgomo unaoendelea wa wahudumu wa afya katika kaunti hiyo. Tulipanda matatu hadi Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Makueni. Kwa bahati mbaya, jamaa na abiria ambao walichukua hatua na kutoa huduma za ukunga hawakuweza kumwokoa mtoto,” akasema Jane Kyalo, jamaa aliyeandamana na Bi Mueni hospitalini.

Tukio la Jumatano linaangazia mgomo wa madaktari unaoendelea katika Kaunti ya Machakos.

Chama cha Kitaifa cha Madaktari Kenya (KMPDU) kiliitisha mgomo huo wiki mbili zilizopita ili kushinikiza serikali ya kaunti hiyo kuboresha masilahi ya wanachama wake baada ya juhudi za kuzungumza na utawala wa Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti kugonga mwamba.

Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamesambaratika.

Yaliyomkuta mama huyo sasa yanaonyesha kuwa kuna haja ya mgomo huo kusitishwa.

Seneta wa Machakos Agnes Kavindu ni miongoni mwa viongozi ambao wamemtaka gavana huyo kuchukua hatua za haraka ili kuzima mgomo huo kama njia ya kumaliza mateso miongoni mwa wagonjwa.

Hata hivyo, gavana huyo ametishia kuwafuta kazi madaktari wanaogoma.

Aliwashutumu kwa kutojali masaibu ya wagonjwa huku Katibu wa Kaunti ya Machakos, Muya Ndambuki akifutilia mbali madai ya madaktari hao ikiwemo kupandishwa vyeo.

‘Serikali ya Kaunti ya Machakos inaajiri zaidi ya wafanyikazi 7300. Upandishaji vyeo wa wafanyakazi umedumaa kwa muda huku wafanyikazi wengine wakikabiliwa na hadi miaka 15 bila maendeleo. Kumekuwa na kupandishwa vyeo kwa wataalamu wa afya mnamo 2021, 2022 na 2023 na hakuna idara zingine zote zilizonufaika ila hii ya afya,’ Dkt Ndambuki aliambia wanahabari mgomo ukiendelea.

Imetafsiriwa na Winnie Onyando