Uhuru, Gachagua wasuka ushirika kuhakikisha mlima unakuwa moto kuelekea 2027
KUONDOLEWA kwa aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua kumezua ukuruba usiotarajiwa kati yake na mrengo wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, nia hasa ikiwa ni kuondoa chama cha UDA, kinachoongozwa na Rais William Ruto, kutoka eneo la Mlima Kenya.
Haya yanajiri huku Dkt Ruto akimteua Naibu Rais Kithure Kindiki kuwa naibu kiongozi wa UDA katika juhudi za kudumisha uungwaji mkono eneo hilo kabla ya uchaguzi ujao.
Urafiki huu usio wa kawaida kati ya kambi za Bw Kenyatta na Bw Gachagua unaripotiwa kulenga kurejesha ushawishi wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya.
Tayari wanajitayarisha kufanya kampeni kali ya kudhoofisha chama cha UDA katika eneo hilo. Ushirikiano wao mpya unaweza kusababisha mabadiliko makubwa katika siasa za Mlima Kenya huku kambi zote mbili zikijitahidi kuwashawishi wapigakura kabla ya uchaguzi ujao kuzima ushawishi wa Dkt Ruto katika eneo hilo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee cha Bw Kenyatta, Jeremiah Kioni anasema kwamba baada ya wakazi wa Mlima Kenya kukasirishwa na UDA, Jubilee kikiwa chama cha pili kwa ukubwa katika eneo hilo, ndicho chama mbadala cha Mlima Kenya.
“Ukweli mmoja ambao tumebaini tulipoanzisha harakati za kusajili wapigakura kama Jubilee ni kwamba watu hawakuhama chama chetu. Walipigia kura UDA lakini hawakujiuzulu katika Jubilee. Watu wengi ambao unadhani wako katika UDA wako Jubilee. Kwa hivyo watu wengi Mlima Kenya wako Jubilee,” Bw Kioni aliambia Taifa Leo.
Bw Kioni amekuwa akimpigia debe kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuchuana na Rais Ruto katika uchaguzi ujao wa 2027, na hivi majuzi kumekuwa na mazungumzo na Bw Gachagua ili kuimarisha mrengo wao.
Bw Gachagua katika siku za hivi majuzi amekuwa akitangaza kuwa amerekebisha uhusiano kati yake na Bw Kenyatta katika hali anayoitaja kuwa harakati za kuunganisha eneo la Mlima Kenya.
“Tulisema watu wote; waliokuwa UDA, Jubilee, Azimio, tusameheane na kuungana. Hata Uhuru Kenyatta ni mtoto wetu, aje tutembee pamoja,” Bw Gachagua amekuwa akinukuliwa akisema.
Tayari washirika wa Bw Gachagua wanasaka chama kipya cha kisiasa, wakiwa na matumaini kwamba wataungana na kambi za Kenyatta-Kalonzo kuangamiza UDA katika Mlima Kenya kabla ya kuanza kampeni za kitaifa.
Lakini Dkt Ruto pia anasemekana kuwa chonjo kwa vita vya kila namna ili kudumisha uungwaji mkono katika eneo ambalo lilimpigia kura kwa wingi katika uchaguzi wa 2022.
Jumatatu, Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la UDA liliidhinisha Prof Kindiki kuwa naibu kiongozi mpya wa chama hicho, akichukua nafasi ya Bw Gachagua kuhakikisha chama hicho kinarejesha ushawishi wake Mlimani.
Lakini wadadisi wanasema Prof Kindiki anakabiliwa na kibarua kigumu kurudisha eneo hilo kwa Ruto. Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Dismas Mokua anaamini Rais Ruto hajapoteza umaarufu katika eneo la Mlima Kenya.
“Rais Ruto angepata kura ya Mlima Kenya akiwa na mwanasiasa mwingine yeyote kutoka Mlima Kenya.”
Rigathi Gachagua alianza kujijenga kisiasa baada ya kuteuliwa mgombea mwenza,” Bw Mokua asema.
Anaongeza kuwa Prof Kindiki hahitaji kuunganisha Mlima Kenya nyuma ya Rais Ruto kabla ya 2027 kwa kuwa rais ana uwezo wa kufanya hivyo peke yake.
Prof Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multi-Media Kenya hata hivyo, anashikilia kuwa serikali ya Kenya Kwanza inaweza kurejesha imani Mlima Kenya kwa kutegemea itakavyobadilisha sekta ya afya, elimu, na kutatua migomo inayoongezeka ya vyama vingi vya wafanyakazi.
“Wasiporekebisha haya, basi watu hawatamuangalia (Kindiki) kuwa mtoto wao bali sehemu ya mfumo ambao umeshindwa,” Prof Naituli anasema.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA