Wafalme wa kona Arsenal wahemeshwa na Everton, Liverpool pia ikipigwa breki
ARSENAL wamepigwa breki tena katika juhudi zao za kumaliza ukame wa miaka 20 bila ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kuumiza nyasi bure katika sare ya 0-0 na Everton ugani Emirates, Jumamosi.
Wanabunduki wa Arsenal waliokuwa wakisaka ushindi wa nne mfululizo dhidi ya Toffees, na walifanya kila kitu sawa ikiwemo kumiliki mpira asilimia 77, kufumua makombora 13 na kona 8-2.
Hata hivyo, masogora hao wa kocha Mikel Arteta – ambao majuzi walipata sifa kama wafalme wa kufunga mabao kupitia ikabu, hususan kona – walishindwa kupenya ngome tisti ya Everton.
Martin Odegaard na Bukaya Saka walikuwa na nafasi nzuri za kupata bao, lakini kipa Jordan Pickford akawazima.
Naye Abdoulaye Doucouré alipata nafasi nzuri kwa upande wa Everton, lakini beki Gabriel Magalhaes akazuia vyema.
Ugani St James’ Park, wenyeji Newcastle walirarua Leicester ya kocha Ruud van Nistelrooy 4-0 kupitia mabao ya Jacob Murphy (mawili), Bruno Guimaraes na Alexander Isak.
Wolves walikunja mkia wakpoteza 2-1 mikononi mwa Ipswich Town ugani Molineux. Baada ya Matt Doherty kujifunga dakika ya 15, Matheus Cuhna alidhani ameokoa hali kwa kusawazisha 1-1 dakika ya 72.
Hata hivyo, Ipswich walikuwa na mipango mingine ya kuhakikisha wananyakua alama zote tatu baada ya Jack Taylor kuwafungia bao la ushindi katika dakika za majeruhi.
Viongozi Liverpool wakagawana alama katika sare ya 2-2 dhidi ya Fulham ugani Anfield. Andreas Pereira aliweka Fulham kifua mbele dakika ya 11 kabla ya Cody Gakpo kusawazisha dakika mbili baada ya kipindi cha pili kuanza kutokana na asisti ya mvamizi matata Mohamed Salah.
Reds ya kocha Arne Slot ilimaliza kipindi cha kwanza wachezaji 10 baada ya beki Andrew Robertson kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 17.
Rodrigo Muniz alirejesha Fulham juu 2-1 dakika ya 76, lakini Liverpool ikajinasua tena baada ya Diogo Jota kufungia timu hiyo yake goli la pili dakika 10 baadaye.
MATOKEO YA EPL (JUMAMOSI):
Arsenal 0-0 Everton
Wolves 1-2 Ipswich Town
Newcastle 4-0 Leicester
Liverpool 2-2 Fulham