Makala

Vijana watumia taka kuunda hela Makueni

Na LABAAN SHABAAN December 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA eneo la Kilungu, Kaunti ya Makueni, vijana wanatumia nguo kuukuu na taka nyingine kutengeneza vyombo vya kukita bustani za maua na mimea mbalimbali. 

Kilichoanza kama mradi wa majaribio mwaka wa 2022, kimekua na kuzaa biashara inayoendelea na kuchumia vijana riziki.

Mradi wao umetambuliwa kuwa mbinu muhimu ya kupunguza taka na kubuni fursa za ajira.

Wazo la kutengeneza vifaa hivi lilichochewa na shauku ya mwanzilishi wa mradi huu, Watson Mwendwa, ya kukabili kero ya uchafuzi wa mazingira.

“Nilimotishwa na lengo langu la kupunguza uchafuzi wa mazingira na kubuni suluhu endelevu kwa matatizo haya. Tukiokota ama kukusanya nguo mbovu kuunda bidhaa, tunaokoa mazingira,” anasema Mwendwa.

Vijana hawa hutumia vifaa vingine kama vile nyaya, simiti, chupa za plastiki na vioo kuunda vishikio vya mimea.

Vesi zilizotengenezwa kwa nguo mbovu, chupa, saruji na rangi. Picha|Labaan Shabaan

Taka ni malighafi

Asilimia kubwa ya malighafi yanayotumiwa ni vitu vilivyotupwa kama taka.

“Tulianza kwa kuchangiana mawazo, kutafuta nguo zilizotumika, na kufanya majaribio na mbinu mbalimbali za kutengeneza vesi. Tulikoseakosea katika hatua za awali lakini baadaye tukafaulu,” anakiri Mwendwa.

“Timu yetu ina wanachama wenye ujuzi katika mbinu bunifu, uhifadhi wa mazingira, kutengeneza saruji, na utafutaji wa masoko,” anaongeza akieleza wanapokuwa na changamoto huwabidi kuhudhuria warsha za mafunzo kupata maarifa zaidi.

Vijana hawa wamepanua wigo wa soko lao kwa kuongeza idadi ya bidhaa wanazotengeneza.

“Tumekuwa tukiongeza aina za bidhaa tunazouza na kujenga ushirikiano na mashirika ya mazingira. Tuna wateja waaminifu na tumeeneza programu za usimamizi wa taka sehemu kubwa ya Kaunti ya Makueni,” Mwendwa anafichua akiwa na fahari.

Patrick Muthini, mwanachama wa Rolling Youth Group, akitengeneza vesi kutumia matambara mabovu katika Karakana yao Kaunti ya Makueni. Picha|Labaan Shabaan.

Soko lipo

Wateja wakuu wa mradi huu ni wakazi wa maeneo ya karibu, shule, biashara, na taasisi za serikali.

Vile vile, kampuni za kurembesha mandhari pia ni moja ya masoko yao.

Mwendwa na vijana wengine 21 wa kundi la Rolling Youth Group huwafikia wateja wao kupitia mitandao ya kijamii, maonyesho ya kibiashara na mapendekezo ya wateja waliofurahia huduma.

“Pia tunashirikiana na biashara nyingine kama mawakala wa kutangaza bidhaa zetu,” anaeleza Mwendwa.

Vesi ya kukuza mimea ambayo imetengenezwa kwa nguo kuukuu, chupa na vifaa vingine. Imetengenezwa na vijana wa Rolling Youth Group, Kaunti ya Makueni.  Picha|Labaan Shabaan

Changamoto

Kama ilivyo kwa mradi wowote mpya, kumekuwepo na changamoto katika safari ya vijana hawa kusaka tonge.

“Imekuwa vigumu kuwashawishi wanajamii kuhusu umuhimu wa bidhaa ambazo zimetengenezwa kutokana na taka,” anasema. “Tumeandaa na kushiriki warsha za kuhamasisha watu kuhusu shughuli zetu.”

Ni shughuli ya kibiashara ambayo imewapa vijana ujuzi wa kiufundi, maarifa ya biashara, na usimamizi endelevu wa taka, huku pia ukiwaongezea mapato.

“Binafsi, mradi huu umenipa nafasi ya kujitambua kwa kuchangia katika uhifadhi wa mazingira,” anasema Mwendwa. Kiuchumi, biashara hii inanipa mkate wa kila siku ikizingatiwa sina kazi nyingine isipokuwa hii.”

Vijana hawa wanalenga kupanua mradi kuvuka nje ya kaunti yao.

Malengo ya muhula mrefu ni pamoja na kufungua duka kubwa la kuonyesha bidhaa, kuzindua duka la mtandaoni, na kushirikiana na mashirika ya kimataifa ya mazingira.

Anthony Wambugu (kushoto) na Simon Muturu Karukwa wakionyesha vesi wanazounda kutumia taka. Picha|Labaan Shabaan