Wahudumu wa matatu walivyovuna hela kama njugu msimu huu wa Krismasi
KAMA ilivyo ada na desturi nchini, msimu wa Krismasi unapobisha hodi Wakenya wengi hasa wanaoishi mijini husafiri mashambani.
Aghalabu, husafiri ili kujiunga na jamaa zao wanaoishi mashambani.
Sawa na miaka ya awali, 2024 haikuwa tofauti vituo vya matatu vikijaa abiria.
Idadi kubwa ikiwa inayosafiri kutoka Nairobi kuelekea mashambani, jukwaa la Krismasi wahudumu wa matatu wamelitumia kuvuna hela kama njugu.
Abiria wakifurika kwenye stendi ili kujumuika na wenzao Sikukuu ya Desemba 25, ndiyo kilele cha shamrashamra za maadhimisho ya Krismasi, nauli imepanda mara dufu.
Licha ya siku hii maalum ulimwenguni kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristu, wahudumu wa matatu hawakusaza waliosafiri.
Kwa mfano, nauli ya Nairobi kuelekea Bungoma abiria walitozwa zaidi ya Sh3, 000.
“Kwa kawaida, hulipa nauli isiyopita Sh1, 500,” akasema Benson Wamalwa mkazi wa Nairobi, japo anatoka Kaunti ya Bungoma.
Akiwa alisafiri na mwanawe anayeishi Nairobi, Bw Wamalwa kwenye mahojiano na Taifa Dijitali alilalamikia kukohoa zaidi ya Sh6, 000.
Hiyo ni safari ya kuenda mashambani pekee, hajafanya mahesabu ya kurejea.
Hata hivyo, alisema ni desturi yake kila msimu wa Krismasi kushirikiana na familia yake pana.
Kuelekea Eldoret, taswira ilikuwa ni ile ile.
“Nyumbani tulipatwa na jambo la dharura, na pamoja na wanafamilia wengine hatukuwa na budi ila kusafiri. Ilishangaza kuenda Eldoret pekee walikuwa wanalipisha Sh2, 000,” akasema Nelly Cheptepgeny.
Wanaotoka Mlima Kenya, mjeledi ulikuwa huohuo.
Kuelekea Nyeri, wenyeji wa ngome hiyo ya naibu rais aliyebanduliwa, Rigathi Gachagua, hawakuwa na jingine ila kulipa Sh1, 000.
Nauli hiyo ilikuwa ya kuelekea Nyeri Mjini, huku Embu ikiwa Sh1, 000 na Meru Sh1, 500.
Kwa kawaida, Nyeri ada inayotozwa huwa Sh500.
Nakuru, Jiji jipya lililo karibu kilomita 160 kutoka Jijini Nairobi ambalo huchukua takriban saa tatu na dakika chache kuelekea humo, abiria waliwekelea Sh1, 000.
“Sababu za nauli kuongezeka ni kuwa gari linapofikisha abiria, kurejea ni vigumu kupata watu,” akasema mmoja wa wahudumu wa matatu za kuelekea Eldoret.
Kampuni kama vile Super Metro, inayofahamika kutoa huduma zake Jijini Nairobi, ilivuna pakubwa msimu huu wa Krismasi mabasi yake yakionekana kuelekea Eldoret, Kakamega na hata Bungoma.
Baadhi ya wenye magari ya kibinafsi, kama vile Voxy, walitumia mwanya huo kutoa huduma za usafiri.
Katika baadhi ya vituo vya matatu Nairobi, kwa sababu ya ongezeko la idadi ya abiria lililosababisha magari kuwa haba abiria waliteta kukesha wakisubiri kupelekwa mashambani.
Misongamano nayo haikukosekana katika barabara ya Nairobi – Nakuru, na pia Nairobi kuelekea Mombasa, baadhi ya sehemu.