McCarthy akiri Stars ina mlima kufuzu Kombe la Dunia 2026
MATUMAINI ya Harambee Stars kufuzu Kombe la Dunia 2026 yalififia Jumapili baada ya kupigwa na Gabon 2-1 uga wa kitaifa wa Nyayo
Mechi hiyo ya Kundi F ilikuwa ya kusisimua na ilihudhuriwa na halaiki ya mashabiki wa nyumbani waliovalia jezi ya Stars ikiwemo viongozi wa kisiasa na watu kutoka matabaka mbalimbali.
Aliyekuwa mshambulizi wa Arsenal Pierre-Emerick Aubameyang ambaye kwa sasa anasaka soka ya kulipwa Uarabuni alifunga bao kipindi cha kwanza kisha akaongeza jingine kipindi cha pili na kuwapa Panthers ushindi huo muhimu.
Kenya ilifunga bao la kujiliwaza kupitia nahodha Michael Olunga kipindi cha pili. Hii ilikuwa mara ya kwanza Stars ilikuwa ikicheza kwenye uga uliofurika watu tangu Oktoba 14, 2018.
Mwaka huo walipiga Ethiopia 3-0 kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Afrika 2019 katika uwanja wa MISC Kasarani, Nairobi. Tangu wakati huo, mashabiki ambao wamekuwa wakijitokeza kwenye mechi ya Stars wamekuwa wakipungua huku pia Stars ikichapwa ovyoovyo na hata wapinzani dhaifu.
Kabla ya mechi ya Jumapili, Stars haikuwa imecheza nyumbani tangu Septemba 12, 2023 walipopoteza 1-0 kwa Sudan Kusini kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan Kusini uga wa Kasarani.
Nayo mara ya mwisho Kenya ilicheza Nyayo ni Novemba 15, 2021 walipopiga Rwanda 2-1 kwenye mechi ya Kundi E ya kufuzu Kombe la Dunia 2022.
Kenya haijakuwa ikicheza mechi zake nchini kwa sababu Kasarani na Nyayo zilifungwa ili zifanyiwe ukarabati kwa ajili ya Mashindano ya Soka kwa Wachezaji wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN).
Ubovu wa safu ya nyuma ulifanya Aubameyang afunge kwa shuti ya karibu iliyomlemea Ian Otieno dakika ya 16. Dakika mbili baadaye mnyakaji wa Gabon Loyce Marius aliutema kombora la William Lenkupae na Olunga akafunga lakini bao hilo likakataliwa.
Aubameyang aliongeza la pili dakika ya 51 baada beki Erick ‘Marcelo’ Ouma kunawa mpira ndani ya kijisanduku. Kenya ilipata bao la kujiliwaza baada ya Olunga kuunganisha krosi ya Ouma dakika ya 67.
Kocha wa Harambee Stars Benni McCarthy alisikitika kuwa vijana wake hawakutumia vyema nafasi ambazo walikuwa wamepata hasa kipindi cha kwanza.
“Tulicheza vizuri na kipindi cha kwanza tungekuwa na bao na tukazama baada ya wao kupewa penalti rahisi. Binafsi napendezwa na jinsi wachezaji walivyojituma kwa sababu hawakukata tamaa na walicheza soka safi,” akasema McCarthy.
“Haya hayakuwa matokeo tuliyoyatarajia na nafasi ya kufuzu inaendelea kudidimia. Hata hivyo, bado kuna mechi nne za kucheza na hatujakata tamaa, tutaendelea kupambana na kupigania ushindi kwenye mechi zinazokuja,” akaongeza mchezaji huyo wa zamani wa Bafana Bafana