Kimataifa

Trump aapa kupiga marufuku raia wa nchi maskini kuingia Amerika

Na BENSON MATHEKA November 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS wa Amerika Donald Trump ametangaza mipango ya kupiga marufuku wahamiaji kutoka nchi maskini kuingia nchi yake, hatua ambayo inatarajiwa kuathiri mataifa kadhaa Afrika.

Novemba 28, 2025, Trump alihusisha raia wa nchi hizo wanaohamia nchi yake na changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi ambazo alidai zinaathiri pakubwa maisha ya raia wa Amerika

Alisema kuwa hivi karibuni atatia saini mabadiliko ya sera za uhamiaji yanayolenga kusitisha safari zisizo za lazima za wageni, hasa kutoka mataifa masikini, kuingia Amerika.

“Nitazima kabisa uhamiaji kutoka nchi zote ambazo hazijaendelea ili kupatia Amerika nafasi ya kurejea kwenye utaratibu wa kawaida, na kuondoa maelfu ya wahamiaji walioingizwa na utawala wa Biden,” Trump alisema.
“Nitaondoa yeyote ambaye hana  faida kwa Amerika au asiyeipenda nchi yetu, na kukomesha manufaa na ruzuku zote za serikali zinazotolewa kwa wasio raia.”

Bara la Afrika ndilo linaloongoza duniani kwa idadi ya mataifa yanayotambuliwa kama maskini duniani.

Katika Afrika Mashariki, Burundi, Uganda, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Somalia huwekwa kwenye kundi hilo, ilhali Kenya hutaja kama taifa linaloendelea, lenye nafasi kubwa ya kuingia katika kundi la nchi zinazoinuka kiuchumi.

Kwa hivyo, Kenya haiwezi kutajwa moja kwa moja kama nchi maskini kwa kuwa si taifa la kipato cha chini. Hata hivyo, haijabainika wazi ikiwa tangazo la Trump litaathiri raia wa Kenya.

Katika kauli yake, Trump pia alishutumu vikali wahamiaji kutoka Somalia, akidai wamekuwa chanzo cha ghasia nchini humo.

Alilenga moja kwa moja Gavana wa Minnesota Tim Walz na Mbunge Ilhan Omar, akiwalaumu kwa kile alichokitaja kuwa “magenge ya Wasomali” nchini Amerika.
“Kwa mfano, mamia ya maelfu ya wakimbizi kutoka Somalia wamekuwa wakitawala jimbo la Minnesota. Magenge ya Wasomali yanazurura mitaani yakitafuta mawindo, huku wananchi wetu wakiteseka.”