HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Mackenzie alivyofanikisha vifo Kwa Binzaro akiwa gerezani

Na BRIAN OCHARO October 29th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MFUNGWA katika Gereza la Shimo La Tewa, Mombasa, anayetumikia kifungo cha miaka 50 jela kwa ulanguzi wa bangi, ameeleza mahakama jinsi alivyoingiza kadi mbili za simu ndani ya gereza hilo, zinazodaiwa zilitumiwa na mhubiri Paul Mackenzie kuwasiliana na watu waliokuwa nje ya gereza na kutuma na kupokea pesa akiwa kizuizini.

Akitoa ushahidi mbele ya Mahakama Kuu mjini Mombasa katika kesi ambayo Mackenzie na washukiwa wengine sita wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji kuhusiana na vifo vya watu 52 katika msitu wa Kwa Bi Nzaro, Kalume Kitsao Rimba alieleza jinsi alivyoficha kadi hizo kwenye nguo zake.

“Nilificha kadi hizo kwenye kitambaa cha ndani kilichoshonwa kwenye sehemu ya kiuno. Hata nilipobadilisha na kuvaa sare za gereza, niliziweka katika sehemu hiyo hiyo,” alisema.

Aliambia mahakama kwamba ingawa simu za rununu na vifaa vingine vya mawasiliano haviruhusiwi gerezani, alipokuwa ameanza kutumikia kifungo chake alikuta wafungwa wengi wakivitumia.

Kitsao alisema maafisa wa magereza wanapaswa kuwajibishwa kwa uwepo wa vifaa hivyo, akidai kuwa wafungwa hawawezi kuviingiza gerezani bila usaidizi wa maafisa wanaohusika na usalama.

Hata hivyo, alisema mabadiliko ya uongozi wa gereza yalileta hatua kali zaidi za kiusalama, huku wasimamizi wapya wakifanya upekuzi wa kina na kunasa bidhaa zilizopigwa marufuku.

Kitsao alisema alitoa kadi mbili za Safaricom kwenye simu yake ya mkononi alipokamatwa Machi 6, 2024, kwa sababu zilikuwa na taarifa za siri za kifedha ambazo hakutaka mkewe azipate.

Aliacha simu hiyo nyumbani lakini akabeba kadi hizo alipofikishwa katika Gereza la Shimo La Tewa siku iliyofuata.

Alisisitiza kuwa hakuwahi kutumia laini yoyote kati ya hizo kupiga au kupokea simu, wala kutuma au kupokea pesa akiwa gerezani. Kitsao alisema maafisa wa gereza walipekua seli yake mnamo Septemba 20, 2025, na kuchukua Biblia mbili na kipande cha karatasi kilichokuwa na majina na nambari za simu.

Wakati wa upekuzi huo, maafisa hao walimwambia mojawapo ya nambari zilizosajiliwa kwake ilikuwa imetumiwa kufanya shughuli za ulaghai. Alikanusha kufahamu matumizi yoyote haramu ya laini hiyo.

Siku iliyofuata, maafisa walifanya upekuzi mwingine na kupata kadi mbili, moja iliyosajiliwa kwa jina lake na nyingine kwa jina la mkewe, Tatu Safari.  Alisema alikuwa amekuwa nazo zote mbili tangu alipowekwa rumande.

Baadaye, polisi walimfahamisha kuwa kadi yake ilikuwa imewekwa kwenye simu ambayo ilishukiwa kutumiwa na Mackenzie kuhusiana na makosa ya jinai yaliyokuwa yakichunguzwa.

Kitsao alikanusha kuwa na uhusiano wowote wa moja kwa moja na Mackenzie, akisema hakuwahi kukutana naye, kuzungumza naye wala kushirikiana naye.

Alisema alimfahamu Mackenzie kupitia taarifa za habari kuhusu vifo vya wafuasi wake huko Shakahola.

Hata hivyo, alikiri kwamba mara kwa mara alikuwa akimpa mfungwa mwenzake Charles Kalume mojawapo ya kadi zake. Kwa mujibu wa Kitsao, Charles alikuwa akiomba simu kutoka kwa wafungwa wengine.

“Charles ndiye aliye katika nafasi nzuri zaidi ya kueleza kwa sababu ndiye mtu pekee ambaye nimempa laini yangu ya simu,” aliliambia mahakama.

Sajenti Stanslous Bongo Chikute, afisa anayesimamia upekuzi katika Gereza la Shimo La Tewa, aliliambia mahakama kuwa hakuweza kubaini iwapo maafisa wa gereza walihusika katika kupenyeza SIM kadi hizo, akisema Kitsao ndiye aliyekuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kueleza jinsi alivyoviingiza ndani ya gereza.

Katika seli ya Mackenzie, maafisa walisema walipata kadi tatu za Airtel zilizokuwa zimefichwa ndani ya vijiti vya kunyoa ndevu vilivyokuwa sakafuni.

Polisi walipata daftari lililokuwa na majina na nambari za simu, ambazo baadhi zilikuwa zimeandikwa juu ya maandishi mengine ili kuzifanya zisomeke kwa shida, pamoja na maandishi yaliyoandikwa kwa mkono, yakiwemo karatasi moja iliyokuwa na jina Emily Ayugi, na Biblia.