HabariHabari za Kitaifa

Masaibu hayaishi, Waititu aongezwa miaka 13 jela

Na RICHARD MUNGUTI November 3rd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ameongezewa kifungo cha miaka 13 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya ulanguzi wa fedha zinazohusishwa na zabuni ya ujenzi wa barabara yenye thamani ya Sh588.7 milioni iliyotolewa wakati alipokuwa gavana.

Hakimu Mkuu Harrison Barasa wa Mahakama ya Milimani, jana, alimuamuru Waititu kulipa faini ya jumla ya Sh21 milioni au atumikie kifungo cha miaka 13 kutokana na mashtaka matatu ya ulanguzi wa fedha.

Hata hivyo, kifungo hicho kitaunganishwa na kile cha miaka 12 ambacho tayari anatumikia kutokana na makosa ya ufisadi.

Mkewe, Susan Wangari Ndung’u, alitozwa faini ya Sh18 milioni au kifungo cha miaka miwili iwapo atashindwa kulipa.

Mfanyabiashara Charles Mbuthia Chege, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Testimony Enterprises iliyopata zabuni hiyo naye aliangushiwa adhabu ya miaka 13. Mkewe, Beth Wangechi Mburu, walitozwa Sh6 milioni au kifungo cha miaka sita.

Hukumu hizo zilitolewa baada ya washtakiwa kufika mahakamani kuomba wapunguziwe adhabu. Waititu na Chege waliiomba mahakama kuwaonea huruma wake zao, wakidai hawakuhusika pakubwa katika mikataba iliyosababisha wapatikane na hatia.

Wakili wa Waititu alisema Susan alikuwa mshirika asiyehusika moja kwa moja na shughuli za kampuni hizo.

“Mahakama itatambua kuwa Susan alikuwa mshirika wa kimya katika kampuni hizo mbili. Hakuwa mtu wa kutia saini akaunti za benki wala mshiriki katika kufanya maamuzi ya biashara na jukumu lake lilikuwa dogo,” akasema wakili huyo.

Upande wa Chege ulisema Beth alikuwa na hisa moja pekee katika kampuni na alihusika tu katika kusaini nbarua za awali za usajili.

Mawakili pia walidai kuwa kazi za ujenzi wa barabara zilikuwa zimekamilika na ripoti ya ukaguzi haikuonyesha upotevu wa fedha za umma. Walisisitiza kuwa mgogoro ulihusu utaratibu wa kutoa zabuni.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga ombi la kupunguziwa adhabu, ukisema kila mshtakiwa alipaswa kuwajibika binafsi kwa makosa yake.

Hakimu Barasa alisema mashtaka ya ulanguzi wa fedha yana sheria maalumu zinazotaka adhabu zinazotolewa zifuate viwango vilivyowekwa.

“Kila mtu atawajibika kivyake kwa makosa aliyotenda,” akasema.

Waititu alitozwa Sh10 milioni au kifungo cha miaka mitano katika shtaka la 10, Sh6 milioni au miaka minne katika shtaka la 11 na Sh5 milioni au miaka minne katika shtaka la 12.

Chege alipewa adhabu sawa na hizo, huku Beth akitozwa Sh2 milioni au miaka miwili kwa kila shtaka kati ya matatu. Susan alitozwa jumla ya Sh18 milioni au miaka miwili gerezani.

Kampuni zilizohusishwa na mikataba hiyo pia ziliadhibiwa. Testimony Enterprises ilitozwa Sh36 milioni, Saika Two Estate Developers Sh24 milioni na Bienvenue Delta Hotel Sh4 milioni. Kampuni hizo zilipewa siku 14 kulipa faini zao.

Kesi hiyo ilitokana na zabuni ya Sh588.7 milioni iliyotolewa na serikali ya Kiambu kwa Testimony kwa ajili ya kuboresha barabara za changarawe na kuziweka lami katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo.