HabariHabari za Kitaifa

Washirika wa Sifuna kuvuliwa nyadhifa muhimu

Na KEVIN CHERUIYOT November 4th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wawili wa Bunge la Kaunti ya Nairobi wanaohusishwa na vuguvugu la Linda Mwananchi Movement (LMM) linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna huenda wakapokonywa nyadhifa zao muhimu katika bunge hilo.

Vyanzo vya kuaminika katika City Hall vinasema hatua hiyo inalenga kuwaadhibu madiwani hao kwa kuendelea kumuunga mkono Bw Sifuna licha ya kuchaguliwa na kuteuliwa kupitia chama cha ODM katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Wanaolengwa ni Kiranja wa Wengi Moses Ogeto na Perpetua Mponjiwa Okello, ambaye aliteuliwa kuwa MCA kupitia ODM.

Bw Ogeto anahudumu muhula wake wa tatu kama mwakilishi wa wadi ya Kilimani, eneo bunge la Dagoretti North. Amekuwa akiwakilisha wadi hiyo tangu 2013 na alikuwa mshirika wa karibu wa mwanzilishi wa ODM, marehemu Raila Odinga.

Kwa upande wake, Bi Mponjiwa ni mwenyekiti wa Kamati ya Elimu katika Bunge la Kaunti ya Nairobi. Pia ametangaza nia ya kuwania kiti cha mwakilishi wadi ya Kileleshwa kinachoshikiliwa na MCA wa ODM Robert Alai.

“Ni kweli. Hoja imeandaliwa na inaweza kuwasilishwa wakati wowote. Inawalenga viongozi wawili ambao wamekuwa wakiunga mkono chama hasimu huku wakiendelea kunufaika na nafasi walizopewa kupitia ODM,” kilisema chanzo kimoja kilichoomba kutotajwa.

Akizungumza na Taifa, Bw Ogeto alisema alikuwa amearifiwa kuhusu mpango wa kumuondoa katika wadhifa wake.

Hata hivyo, alidai ODM imepoteza misingi iliyowekwa na Raila Odinga, akisema chama hicho sasa kinatanguliza maslahi ya wanasiasa badala ya wananchi.

“Watu hawa hawafanyi tena yale Baba alikuwa akifanya, ndio maana tumetengana. Baba alikuwa wa wananchi, lakini wao wanajali pesa. Baba alikuwa akinipa maagizo kuhusu jinsi ya kuwatetea wananchi, lakini leo hakuna anayetaka kuwatetea,” alisema.

Bw Ogeto alisema kuondolewa kwake hakutakuwa na athari kubwa kwake kwa sababu bunge linakaribia kuingia likizoni hadi Februari kabla ya mapumziko mengine yasiyo na tarehe maalum ya kurejea.

Alifichua kuwa anamezea mate kiti cha ubunge cha Dagoretti North kinachoshikiliwa na Beatrice Elachi wa ODM.

Alisema hana hofu ya kupoteza wadhifa huo kwa sababu amejijengea uhusiano mzuri na wakazi wa eneo hilo.

Iwapo ataondolewa, nafasi yake kama Kiranja wa Wengi inatarajiwa kuchukuliwa na naibu wake Stazo Omung’ala Elija Ang’ila, MCA wa wadi ya Upper Savannah.

Jitihada za kumpata Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, Peter Imwatok, ili kutoa maoni yake hazikufanikiwa kwani hakujibu simu wala ujumbe.