Mchango wa siasa katika kueneza Kiswahili kupitia kauli mbiu ‘Skiza Wakenya,’ ‘Usawa ni Sawa,’ na ‘Linda Mwananchi’
MATUMIZI mbalimbali ya lugha yamethibitisha kwamba katika siasa za Kenya, mbali na mawasiliano, lugha ni nyenzo muhimu ya ushawishi na uhamasishaji.
Wanasiasa huitumia kueleza sera zao, kujenga taswira zao na kuwavutia wapigakura. Kiswahili kimekuwa chombo muhimu katika kuendeleza mambo hayo.
Kwa mfano, kinatumiwa katika kauli mbiu za vyama vingi, hata pale ambapo majina ya vyama hivyo ni ya Kiingereza.
Kwa mfano chama cha The National Alliance (TNA) kilitumia kauli mbiu “Kazi Iendelee”, Democratic Citizens Party (DCP) kinatumia “Skiza Wakenya”, The Clean Alliance Party of Kenya (CAP-K) nacho kinatumia “Maisha Mapya, Uongozi Mpya”, The Equitable Party kina kauli mbiu “Tusawazishe”, People’s Party of Kenya hutumia “Sauti ya Wakenya”, huku Mwongozo Party of Kenya kinatumia “Sote Pamoja”.
Kauli hizi zinaonyesha jinsi vyama vinatumia Kiswahili kuwasilisha ujumbe kwa wananchi.
Aidha, zinadhihirisha kuwa lugha ni sehemu ya mkakati wa kisiasa unaolenga kujenga uhusiano kati ya chama na wapigakura.
Uamuzi wa kutumia Kiswahili badala ya Kiingereza au lugha za jamii unaeleweka tunapozingatia nafasi yake nchini.
Ni lugha ya taifa na mojawapo ya lugha rasmi inayowaunganisha wananchi wa makabila, maeneo na matabaka mbalimbali.
Hivyo basi, mwanasiasa anayekitumia ana nafasi ya kufikisha ujumbe wake kwa hadhira pana zaidi.
Hili ni muhimu hasa wakati wa kampeni, ambapo viongozi huwasiliana na watu wenye tofauti za kiisimu na kitamaduni.
Faida ya Kiswahili katika siasa haiishii kwenye kura, kwani wanasiasa wanakieneza kila wanapokitumia.
Wanakuwa pia mabalozi wa lugha hii wanapoizungumza katika mikutano ya hadhara, mijadala ya kisiasa, mahojiano ya vyombo vya habari na majukwaa ya kidijitali.
Wanapozunguka nchini kuuza sera zao, wanakieneza Kiswahili na kukifanya sehemu ya mawasiliano ya kila siku.
Kwa njia hii, siasa huipa lugha hii nafasi ya kusikika na kutumiwa na watu wengi katika mazingira tofauti.
Uwezo
Zaidi ya hayo, Kiswahili kina uwezo wa kisanaa unaowawezesha wanasiasa kubeba mawazo mapana kwa maneno machache.
“Kazi Iendelee”, “Sote Pamoja” “Mbele Pamoja” na “Maisha Mapya, Uongozi Mpya” ni kauli fupi, rahisi kukumbuka na rahisi kurudiwa zinazosheheni taarifa muhimu kwa umma.
Kauli za hivi karibuni kama “Usawa ni Sawa,” “Linda Mwananchi” na “Linda Ground” nazo zinaonyesha jinsi maneno ya Kiswahili yanavyoweza kubeba ujumbe wa kijamii na kisiasa kutegemea muktadha.
Maneno kama usawa, haki na mwananchi yanagusa hisia na kuibua mijadala kuhusu masuala yanayowahusu raia.
Matumizi haya yanakipa Kiswahili nafasi katika mijadala ya kitaifa na kuifanya iwe hai na ambayo inatumika kueleza masuala ya uongozi, uchumi na maendeleo.
Pia, yanaondoa lugha hii katika mtazamo ambao unahusu mazungumzo ya kawaida pekee, na kuisawiri kuwa inaweza kubeba hoja nzito za kisiasa na kijamii.
Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha matumizi ya lugha na utekelezaji wa sera.
Kauli mbiu inaweza kuvutia wananchi, lakini haithibitishi kikamilifu kuwa ahadi zitatekelezwa. Wananchi wanapaswa kuchunguza sera, mipango na matokeo ya viongozi.
Kwa hakika, wanasiasa wana nafasi muhimu katika kueneza Kiswahili nchini.
Wanapokitumia kuwasilisha sera na kuwasiliana na wananchi, wanakuwa sehemu ya juhudi za kukikuza na kukipa nafasi katika ramani ya kitaifa na kimataifa.
Kila jukwaa la kisiasa linalotumia Kiswahili ni fursa ya kukitangaza na kukieneza. Wanasiasa wanabeba bendera ya Kiswahili.